WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, September 16, 2013

Mbowe, Lipumba, Mbatia wambana JK

mbowe 23301

Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita "utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi" hivyo wanaitaka Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.

Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.

"Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona ila aurejeshe bungeni,"alisema Lipumba na kuongeza:

"Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko."

Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala yake unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa Katiba katika msingi wa maridhiano.

Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.

Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.

Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.

Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.

Mbowe na MbatiaKwa upande wake, Mbowe alisema: "Amani itavurugwa kama mchakato wa Katiba Mpya utahodhiwa na chama kimoja cha siasa, ikiwa hivyo sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani ni lazima haki iwepo."

Alisema fursa ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na watu wachache ndani ya CCM, na kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea, ili washiriki katika kuidai Katiba iliyotokana na mawazo yao.

Mbowe alisema wapinzani hawatarudi nyuma na hawatakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa Katiba ya sasa.

"Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika katika kitabu chake kwamba, 'kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini'. Amani itaharibiwa na wale wenye dola, sio vyama vya upinzani" alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Mbatia alisema: "CCM ndio nini... Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubaki."

"CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao. Katiba Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa sio kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka pembeni."

Mbatia alimtaka Rais Kikwete kusimamia kikamilifu mchakato wa Katiba ili historia isije ikamhukumu. "Yeye ndio ameanzisha mchakato huu wa kupata Katiba Mpya, aweke masilahi ya taifa mbele sio masilahi ya chama chake cha siasa, CCM haiwezi kuwa juu ya dola na Serikali, asisaini marekebisho ya Katiba yaliyofanyika bungeni,"alisema Mbatia na kuongeza: "Mkono wa Rais usilitumbukize taifa la Tanzania katika machafuko, kwanza hagombei tena urais wala uongozi ndani ya chama chake, sasa anamwogopa nani."

Vyama hivyo pia vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa ni 'hujuma dhidi ya upatikaji wa Katiba Mpya'.

Mikutano hiyo itaanzia Septemba 21 mwaka huu, katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.

Makundi mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.

:CHANZO MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment