WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, September 14, 2013

Kuku wetu wa elimu tunakutana nao Arusha




NIMESEMA kwamba kila tendo tunalofanya huzaa tendo-rejea, na kwamba kuku tuliowaachia asubuhi ni wale wale wanaorejea nyumbani mwisho wa siku. Kwa hiyo tusishangae.

Tumezembea sana kuwekeza katika elimu ya taifa letu, tukaichukulia elimu kama kitu cha mzaha kinachoweza kuongozwa na yeyote miongoni mwetu. Tumeifanya wizara inayosimamia elimu isiwe na jina linalotambulika, tukiibadilisha majina kila tunapounda serikali, ikiunganishwa na hiki leo na kile kesho.

Walimu wanalalamikia mishahara yao midogo na isiyolipwa kwa wakati, mazingira mabovu na ukosefu wa vitendea kazi, tunawaona ni wakorofi, wenye uroho wa fedha, wasiokuwa wazalendo. Tunawatolea vitisho mpaka wanalazimika kuacha mgomo wao, wanarudi kufundisha shingo-upande.

Wala hakuna asiyejua kwamba walimu waliolazimishwa kurudi madarasani kwa nguvu za dola hawatafundisha kama wanavyotakiwa kufundisha. Tunajua kwamba walimu wamerudi darasani shingo-upande, tunajua kwamba hawaridhiki kuifanya kazi yao katika mazingira yale, tunajua kwamba  wataifanya “bora liende,’ lakini bado tunawaachia waendelee kuwalea watoto wetu na wala hatuonyeshi kuwa na wasiwasi. La msingi kwetu ni kwamba hakuna mgomo tena, walimu wamo darasani na watoto (eti) wanasoma.

Wakati haya yanaendelea tunawasikia na kuwaona wanasiasa wetu wakiendelea kujiongezea malipo haramu kila wanapohisi haja ya kufidia matumizi yao yasiyo na kikomo. Mwenye akili timamu angeweza kujiuliza, hasa hawa wanasiasa tunawalipa kwa kazi gani wanayotufanyia? Je, kati ya mwalimu na mwanasiasa nani hasa ni muhimu kwa taifa hili?

Lakini tunaendelea kama tulivyo: Walimu wanadharauliwa, hawalipwi stahili yao, wakigoma tunawatisha, “wanasiasa” wababaishaji walio bungeni na kwingineko wanalipwa wasivyostahili, watoto wanapita shuleni kama wanaotembea usingizini, tunaendelea kujenga taifa la wajinga.

Kuku wetu wanaanza kurudi nyumbani magharibi pale tunapopata matokeo ya kutia hofu ya mitihani ya kidato cha nne. Karibu wanafunzi wote wameshindwa, kisha tunatahayuri, tunatapatapa, tunataharuki kutafuta kisa na mkasa. Hivi hatukujua kwamba tuliwekeza katika ujinga tangu mwanzo?

Halafu tunaongeza vichekesho vingine visivyochekesha, mzaha na upuuzi wa hali ya chini kabisa. Eti kuna watu wanaodhani kwamba watoto wakichapwa viboko watapata akili hata kama hawana walimu wenye sifa, na hata kama wazazi wao ni wapuuzi wa aina niliyoieleza.

Tunaiua elimu hivi hivi tukiona. Tunajua, ama tunatakiwa tujue, kwamba matendo yetu wenyewe ndiyo yaliyotufikisha katika matokeo haya ya kutisha, tunatakiwa tujue kwamba tumelinyang’anya taifa letu mustakabali wake kwa kuwanyima watoto wetu elimu iliyo bora, lakini suluhisho letu ni viboko.

Kama si viboko ni kurejea matokeo na kuyapaka wanja ili yapendeze, tunapunguza alama za ufaulu, kisha tunatangaza kwamba kile tulichokitangaza awali kama kushindwa kubaya kwa watoto wetu, kihalisia ni ufaulu mkubwa uliozidi hata miaka iliyotangulia.

Sasa huu ndio ule ujuha ambao aliueleza rafiki yangu marehemu Seithy Chachage, aliyeuita “collective imbecilisation,” ama kufanywa majuha kihalaiki. Jambo la kushangaza ni kwamba, kwa sababu hakuna mgomo tena, hakuna tatizo, na maisha yetu yanaendelea “kama kawaida.”

Lakini tatizo bado lipo, tena kubwa, ila linakuja katika sura nyingine. Tumo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tena kwa hiari yetu, si kwa kulazimishwa na mtu yeyote. Katika mikataba tunayosaini imo mikataba inayotutaka tufungue milango katika maeneo kadhaa ili kuruhusu majirani zetu waingie nchini mwetu, na bidhaa zao, na huduma zao pia, sawa sawa na vile ambavyo na wao wanatakiwa wafungue mipaka yao ili nasi tuweze kuingia kwao.

Tukifika hapo tunagota, kwa sababu tunagundua (kama vile ndiyo tunashituka usingizini) kwamba wale kuku wetu wanarejea nyumbani. Vijana wetu wanagundulika kwamba hawana elimu ya ubora wa kuweza kushindana na wenzao kutoka nchi jirani. Suluhisho linakuwa ni kuzuia au kupiga breki dhidi ya muendelezo wa ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa sababu tunayo hofu kwamba majirani zetu watatuzidi kete.

Suluhisho letu hatulioni katika kuketi chini na kujiuliza kwa dhati ni nini tunatakiwa kufanya kuhusu elimu yetu iliyokufa, hapana; suluhisho tunaliona katika kuzuia maendeleo ya Jumuiya kwa kukataa wanachopendekeza bila sisi kusema tunataka nini, kimsingi kwa sababu hatujui tunachotaka.

Tunajikuta katika kona ya ajabu. Kutoka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki hatutoki; kushiriki katika muendelezo wa Jumuiya kama tulivyokubaliana hatushiriki; hatusemi nini hatutaki na kusema nini tunataka; tunaonekana kama kikwazo kwa wenzetu.

Kuku wetu wanazidi kurudi nyumbani. Wenzetu wanaona kama kikwazo hawako tayari kutusubiri hadi tuamue kama tunataka kwenda kushoto, kulia ama nyuma; wanaamua kwenda zao huku wakituambia kwamba tunaweza kujiunga nao tutakapokuwa tayari. Sisi tunashangaa, tunataka watuambie wanapokutana wanajadili nini, na kwa nini hawatushirikishi. Ni kuku wetu wote hawa.

Tunapozungumza masuala ya Afrika Mashariki tungetakiwa turejeee nyuma kidogo tu, wala si sana. Tungerejea katika malalamiko ya walimu wetu, na migomo yao inayozimwa kwa vitisho na matumizi ya mabavu, tungetambua kwamba matatizo tunayoyashuhudia leo hii kati yetu na ndugu zetu wa Afrika Mashariki yanatokana, kwa kiasi fulani, na jinsi tunavyowatendea walimu wetu.

Hivyo ndivyo kuku wetu wanavyorudi nyumbani, halafu tunawatazama kama vile hatuwajui. 

Source:www.raiamwema.co.tz: Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment