WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, September 13, 2013

BUNGE HILI HALIWEZI KUTUPELEKA KWENYE KATIBA YA WATANZANIA

Hivi karibuni tumeshuhudia mikanganyiko, udhalilishaji na lugha chafu bungeni kutokana na mswada wa sheria ya marekebisho ya uundwaji wa katiba mpya.  Hatimaye mswada huo umepitishwa kama ulivyoletwa maana hakuna mbunge aliyeujadili. Wabunge wa upinzani waliususia baada ya kupuuzwa, wakatoka nje. Wabunge wa CCM, baada ya wabunge wa upinzani kutoka nje na kuususia, nao wakaamua kutokuujadili na badala yake wakatumia muda wa kuujadili mswada kuwatukana wabunge wa vyama va upinzani. Naibu Spika, akaruhusu wabunge watumie muda wao kutukana badala ya kujadili mswada.
Kwa watanzania tulio nje, tumeweza kuona kwa uwazi mkubwa kuwa bunge letu la sasa halina uwezo wa kutunga sheria ya kutuelekeza namna iliyo bora ya kupata katiba mpya. Wakati wabunge wa vyama vya upinzani vinapigania ushiriki zaidi wa wananchi katika kutengeneza katiba yao, wabunge wa CCM wanapigania zaidi uundwaji wa katiba ambao utahodhiwa na Chama Cha Mapinduzi, Bunge na Rais.
Wakati wa mijadala ya sheria zinazohusu uundwaji wa Katiba Mpya bungeni, tangu mwanzo, tumeshuhudia kwa kiwango kikubwa kumekuwa na mashindano kati ya wabunge wa vyama vya upinzani na wabunge wa CCM. Wabunge wa CCM wanaonekana kutokukubali hoja yoyote ya mbunge wa upinzani hata kama ni nzuri, na inaonekana, ka upande wao kufanya hivyo ni kama itaonekana kukubali kuwa wapinzani wameshinda na CM imeshindwa. Fikra za namna hii haziwezi kutusaidia kupata katiba iliyo nzuri. Tungeweza kupata katiba nzuri endapo tu wabunge wetu wanapoliongelea suala lolote la katiba, wangekuwa wanaongozwa na utaifa na siyo ushindani wa siasa za vyama.
Kuna mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika sheria zinazotuelekeza kuipata katiba mpya, ambapo kama sheria yoyote au muundo wowote hautupeleki kwenye kuutambua na kukuukubali ukweli huu, basi sheria au muundo huo ni batili:
1.    Katiba ni ya watanzania wote, hakuna mwenye haki zaidi kuliko mwingine
2.    Katiba nzuri itatokana na ushiriki mkubwa wa wananchi wote kupitia uwakilishi wa moja kwa moja au uwakilishi wa asasi na taasisi mbalimbali
3.    Mwungano wetu ulikuwa wa matafa mawili, Tanganyika na Zanzibar, na kwa kuwa katiba ni ya mwungano lazima uwakilishi wake uzingatie ukweli huu
4.    Rais, bunge, serikali, mahakama ni mazao ya katiba si wao wanaotakiwa kuitengeneza katiba bali katiba ndiyo inayotakiwa kuwatengeneza wao
5.    Bunge, serikali, mahakama, Rais, ni wadau wa kutengeneza katiba na wala hawana mamlaka ya kuunda katiba pekee yao au kuhodhi mchakato wa kupata katiba mpya
6.    Wabunge wengi waliopo bungeni sasa, upatikanaji wao umehusisha michakato iliyoendana na hila, udanganyifu, upendeleo, wizi wa kura na rushwa. Tunatengeneza katiba ya kuzuia hayo, hivyo wawakilishi na viongozi waliopatikana kwa njia hizo, kamwe hawawezi kututengenezea katiba nzuri itakayozuia njia ambazo huwa wanapitia kuupata uwakilishi
Kwa kuzingatia hoja hizo 6 hapo juu, si busara na haki hata kidogo kumpa mamlaka makubwa kupindukia Rais katika kupata katiba mpya wakati yeye ni tunda la katiba na siyo kinyume chake. Kwenye hilo, wabunge wa upinzani walikuwa sahihi kabisa kutaka mamlaka ya uteuzi ya Rais katika kupata wajumbe wa bunge la katiba, yapunguzwe sana au kuondolewa ili katiba itakayopatikana iwe ya wananchi na siyo ya Rais. Na hilo ni lazima lionekane wazi kwa kila mtu siyo kwa kufanya kuambiwa. Na ninamtahadharisha Rais Kikwete kuwa akikubaliana na mambo yanayofanyika bungeni sasa na ofisi ya mwanansheria mkuu na waziri wa sheria, atapata aibu kubwa huku mbeleni. Naamini Rais anataka historia imkumbuke kuwa alianzisha na kusimamia mchakato wa kupata Katiba ya kwanza ya wananchi iliyozingatia matakwa ya Watanzania. Lakini kwenye kulifikia hili ana maadui wengi wakubwa ndani ya chama na serikali yake. Na wengine wametamka wazi kabisa kuwa haikuwa ajenda ya CCM. Mwanasheria Mkuu na Waziri wa sheria wa wakati mchakato unaanza waliwahi kutamka wazi kabisa kuwa hakuna haja ya kuwa na katiba mpya. Nilitegmea kuwa baada ya Rais kuamua kuwa ni lazima tuwe na katiba mpya, kwanza angemwondoa Mwanasheria Mkuu ambaye ni wazi anasimamia uandaji wa miswada ya kupata katiba mpya huku yeye mwenyewe akiwa haamini kama kuna haja hiyo. Rais alistahili kuwa na watu wanaofanana na yeye katika kuona umuhimu wa kuwa na katiba mpya. Ikumbukwe kuwa wabunge wengi wa CCM hawataki katiba mpya ingawa wananchi tunaihitaji sana. Rais ni lazima asimame kidete na Watanzania kupata katiba mpya, na yeyote anayelizuia hilo ajulikane wazi kuwa ni adui wa Watanzania na ni adui wa Rais pia.
Kwa kuzingatia ukweli kuwa wabunge tulio nao sasa, wengi wao waliupata huo ubunge kwa ghiliba, wizi wa kura, rushwa na udanganyifu, ndiyo maana kuna kila sababu ya kuzuia bunge hili kuwa sehemu ya bunge la katiba. Tunataka bunge letu hili lichukuliwe kama taasisi mojawapo ambayo itatengewa uwakilishi katika bunge la katiba kama zilivyo taasisi nyinginezo.
Bunge la sasa lifanye kazi moja tu ya kuainisha asasi zinazotakiwa kutoa wajumbe wa baraza la katiba kwa kuzingatia ukubwa wa uwakilishi. Baada ya kupatikana wajumbe wa baraza la katiba, wakutane na kupitisha shaeia zote zitakazotumika katika kusimamia mchakato wa upatikanaji katiba mpya. Kwangu mimi taasisi ambazo zingechukuliwa kuwa ni muhimu katika kutoa wajumbe wa kuunda bunge la katiba zingekuwa kama zifuatazo:
§  Wawakilishi wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania kwa kuzingatia mikoa wanayotoka na vyama wanavyowakilisha (mbunge mmoja toka kila mkoa)
§  Wawakilishi kutoka Bunge la wawakilishi Zanzibar
§  Wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
§  Wawakilishi wa serikali kuu ya Jamhuri ya Mwungano (bara tu kwa niaba ya Tanganyika)
§  Wawakilishi wa serikali za mitaa
§  Madhehebu ya dini mbalimbali yanayotambulika kisheria
§  Taasisi za Elimu ya juu
§  Taasisi za kitaaluma
§  Mahakama Kuu
§  Taasisi za kibiashara, n.k.
Wajumbe hao ndiyo wamchague Spika wao, Naibu Spika na Katibu wa bunge. Spika awe na mamlaka ya kupendekeza wajumbe wengine ambao kutokana au na utaalam wao au uzoefu wao, mchango wao unaweza kuongeza ubora wa katiba itakayotengenezwa au sheria ziatakazoongoza mchakato wa kutengeneza katiba mpya.
Jambo la kusisitiza ni kuwa ni lazima na ni muhimu, kama tunataka katiba ya watanzania wote, katiba iliyo nzuri, tupunguze sana au kuondoa kabisa ushiriki wa bunge tulilo nalo sasa au kututengenezea sheria za kutuongoza katika mchakato wa kupata katiba mpya au kutuandalia sheria za kutengeneza katiba mpya. Bunge hili na Rais, majukumu yao ya mwisho yaishie kwenye kuidhinisha wajumbe watakaounda bunge la katiba, na sheria itamke wazi kuwa Rais jukumu lake kuu litakuwa kutangaza majina ya wajumbe walioteuliwa na asasi zao kuziwakilisha kwenye bunge la Katiba. Na baada ya hapo, sheria nyingine zote zitakazoongoza mchakato mzima ziundwe na kupitishwa na Bunge la Katiba na siyo hili bunge letu la sasa. Bunge letu la sasa limegeuza uundwaji wa katiba mpya ni ushindani wa Kichama, ni ukweli huo ndiyo unaolifanya lisiwe chombo sahihi cha kutupeleka tunakotaka.
source: Bartholomew Mkinga (bmkinga@yahoo.com)

No comments:

Post a Comment