WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, September 19, 2013

Tambwe apiga 4 Simba ikiua 6, Yanga hoi

 
Mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe akishangilia goli alilofunga dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Tambwe alifunga magoli manne katika mechi hiyo ambayo Simba ilishinda 6-0.
Mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi Tambwe Amisi, jana alifanya ambacho hakijafanyika kwa miaka mingi nchini baada ya kufunga magoli manne peke yake na kuisaidia timu yake kutoa kipigo kikubwa zaidi msimu huu cha magoli 6-0 dhidi ya ya Mgambo JKT, wakati mabingwa Yanga walidondosha pointi nne katika mechi mbili za mjini Mbeya baada ya jana pia kushikiliwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Prisons.
Washindi wa pili mwaka jana, Azam nao walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Ashanti, ambayo ilianza ligi hiyo vibaya kwa kipigo cha 5-0 kutoka kwa Yanga, ambacho ni kipigo cha pili kwa ukubwa katika rekodi mwaka huu Bara.
 
Ushindi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliwaweka Simba kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 10, wakiwashusha waliokuwa vinara wasiotarajiwa JKT Ruvu (9), ambao jana walikumbana na kipigo cha 1-0 kutoka kwa ndugu zao wa Ruvu Shooting.

Shujaa wa siku ya jana, Tambwe alisema baada ya mechi hiyo kwamba kazi sasa imeanza baada ya kuuzoea mfumo wa timu huyo lakini akasisitiza kuwa bado ligi ya Tanzania Bara ni ngumu kuliko ya kwao Burundi.

Tambwe alisema licha ya kuwafunga Mgambo idadi hiyo kubwa ya magoli, timu hiyo ya tanga ni ngumu na kamwe hataidharau timu yoyote.

Mrundi huyo, mfungaji bora wa ligi kuu ya Burundi ambako alifunga magoli 21 katika mechi 18, na kisha kuwa mfungaji bora wa Kombe la Kagame ambako alifunga magoli sita katika mechi sita za michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika mjini Darfur, Sudan na kuisaidia timu yake ya zamani ya Vital'O, sasa ndiye kinara wa mabao wa ligi kuu ya Bara akiwa na magoli manne baada ya mechi nne.Anafuatiwa na Jerry Tegete wa Yanga mwenye magoli matatu. 

Hata hivyo, Tambwe si mchezaji pekee kuwahi kufunga idadi kubwa ya magoli peke yake katika mechi moja.

Licha ya magoli yake manne ya jana kuvunja rekodi iliyowekwa misimu miwili iliyopita na mshambuliaji wa Polisi Dodoma, Juma Semsue ambaye alikuwa mchezaji wa mwisho kufunga 'hat-trick' katika Ligi Kuu ya Bara 2011-12, rekodi ya juu kabisa bado inashikiliwa na Edibily Lunyamila aliyefunga magoli sita peke yake wakati Yanga ilipoisambaratisha RTC Kagera kwa magoli 8-0 kwenye ligi hiyo ya juu zaidi nchini mwaka 1998.  

Tambwe aliiandikia Simba goli la kwanza akimalizia kwa kichwa krosi murua ya Issa Rashid 'Baba Ubaya'. Hilo lilikuwa goli la kwanza Mrundi huyo kuifungia Simba ligi kuu msimu huu. Hakufunga katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Oljoro JKT na Mtibwa ambazo alicheza dakika zote 180.

Haruna Chanongo alifungia Simba goli la pili katika dakika ya 33 kwa juhudi binafsi akimlamba chenga kipa Kulwa Manzi wa Mgambo lakini mpira ukambabatiza beki Lufunga akapiga tena 'kishuti mtoto' kikatinga wavuni.

Tambwe, ambaye ni mfungaji bora wa ligi kuu ya Burundi, alithibitisha makali yake baada ya kumalizia mpira wa shuti kali la Chanongo lililotemwa na kipa Manzi na kuiandikia Simba goli la tatu katika dakika ya 42.

Dakika moja kabla ya mapumziko, Tambwe alikamilisha 'hat-trick' yake ya kwanza kwenye ligi hiyo mpya kwake na kuwa 'hat-trick' ya kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara tangu msimu wa 2011-12, wakati alipofanya hivyo, Juma Semsue wa Polisi Dodoma, ambayo hata hivyo ilishuka daraja mwaka huo huo. Alifunga goli lake la nne kwa njia ya penalti katika dakika ya 77.

Kikosi cha kocha Abdallah Kibadeni 'King' kilichoanza jana kilikuwa na beki wa kulia Miraji Adam aliyekosa mechi ya Jumamosi walioshinda 2-0 dhidi ya Mtibwa.

Pia kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki ambao waliingia kipindi cha pili katika mechi ya Jumamosi, walianza katika mechi ya jana huku beki wa kulia Nassoro Masoud 'Chollo', viungo Twaha Ibraham na Said Hamis walioanza Jumamosi, walikuwa benchini jana.

Beki Novat Lufunga wa Mgambo alikuwa na bahati kwa kutoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko Tambwe ambaye hakuwa na mpira katikati ya uwanja. Refa Jacob Adonyo kutoka Mara hakumuonyesha kadi yoyote licha ya mfungaji bora wa Kombe la Kagame Tambwe kulazimika kugangwa kwa dakika moja ndani ya uwanja.

Dakika 4 baadaye mshambuliaji Betram Mwombeki, aliyesajiliwa msimu huu akitoka Pamba ya Mwanza, alifanya kosa kama hilo dhidi ya beki Bakari Mtama aliyelazimika pia kugangwa uwanjani lakini hakuonyeshwa kadi yoyote.

Jerry Tegete aliifungia Yanga goli la kuongoza katika dakika ya 41 akimalizia krosi iliyochongwa na Simon Msuva.

Hata hivyo, Prisons walisawazisha goli hilo katika dakika ya 77 kupitia kwa Ibrahim Isaka aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na nyota wa zamani wa Yanga, Omega Seme.

Kabla ya sare ya jana, Yanga pia ilishikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City Jumamosi kwenye uwanja huo huo wa Sokoine mjini Mbeya. Yanga sasa ina pointi sita baada ya ushindi mmoja na sare tatu. 

Katika mechi nyingine za jana, Kagera Sugar ilishinda 2-0 nyumbani dhidi ya JKT Oljoro, Coastal ilitoka 1-1 dhidi ya Rhino Rangers, Mtibwa ilitoka 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Vikosi vilikuwa;

Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Henry Joseph, Betram Mombeki, Amisi Tambwe, Haruna Chanongo.

Mgambo: Kulwa Manzi, Francis Anyosisye, Salum Mlima, Bakari Mtama, Novat Lufunga, Salum Kipaga, Nassoro Gumbo, Peter Mwalianzi, Mohamed Neto, Fully Maganga, Salum Gila.

Yanga: Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Salum Telela/ Frank Domayo (dk.68), Didier Kavumbagu, Jerry Tegete/ Said Bahanunzi (dk. 72) na Haruna Niyonzima.

Prisons: Beno David, Beno David, Salum Kimenya, Laurian Shabani, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issa, Jimmy Shoji, Fredy Chudu, Ibrahim Isaka, Six Ali, Jeremia Juma, Lugano Mwagomba.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment