WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, July 7, 2013

Tujiulize; Je, Watanzania Tuna Hulka Ya ‘ Kupiga!’?


4 f6000

Ndugu zangu,

Jana nikiwa mahali fulani hapa Dar nilikutana na kaka na mwalimu wangu kwenye tasnia ya habari, ni ndugu yangu Mobhare Matinyi. Huyu alianza kuhariri kazi zangu tangu nikiwa Sweden miaka ya 90. Wakati huo Matinyi alikuwa Mhariri gazeti la Majira.
Nilimkuta kaka Matinyi kwenye mazingira ya kulalamika, tena kwa sauti. Kaka Matinyi alikuwa akilalamikia taratibu za mahali hapo. Zilikuwa ni taratibu za hovyo.
Nilimwacha Matinyi alalamike kwanza kabla sijamsalimia, maana,
wakati akilalamika hakujua, kuwa nami pia  nipo mahali hapo.

Kaka Matinyi akatulia. Nikamfuata kumsalimu na kumpongeza pia kwa kutoa sauti yake juu ya kile kilichokuwepo hapo. Nikamwambia; kuwa hiyo ndio demokrasia, kama ya Marekani vile! Maana, Matinyi wala hakugombana na mtu, alikuwa akiyasema ya moyoni mwake, kwa sauti, basi!
Baada ya hapo Matinyi na mimi tukajikita kuzungumzia  fikra zetu kama Watanzania. Matinyi anasema;

“ Unajua Maggid, zamani Watanzania tulikuwa wazalendo sana, na sasa kama vile tunalipizia, kuwa tunafanya yale yasio ya uzalendo. Ona, kila mahali utasikia watu wanatumia nafasi zao kupiga! ( Kuiba)
Hapo Matinyi akanikumbusha kauli ya Waziri  Emmanuel Nchimbi alipokuwa bungeni. Nilimwona na kumsikia Nchimbi akitamka;

“ Jamani Watanzania tuache mambo ya  wizi wa mali za umma, yaani, kuna mtu hata kama ni mradi wa ujenzi unaotumia  mifuko sita ya sementi bado anataka kupiga, tubadilike!”  Anasema Emmanuel Nchimbi na kuasa.

Hakika wizi ni tatizo. Na hatari ni pale wizi unapopewa majina mengine wakati wenye kuiba ni wezi kama wezi wengine. Ni wahalifu.  Leo utasikia  mwenye hali nzuri anasifiwa mitaani kwa kusemwa “ Jamaa kapiga hela ndefu!”

Naam, mhalifu anasifiwa badala ya kulaaniwa. Na tabia hii ya wizi inaongezeka, hasa kwa kutumia vibaya ofisi na mamlaka tulizokabidhiwa. Inakuwaje basi ofisini wakubwa wanaposhiriki ‘ kupiga!’ mali ya umma.  Bila shaka walio chini wataiga hivyo hivyo.
Na majaribu yako mengi, lakini, Watanzania hatuna hulka ya wizi. Na kama tutasimamia  kwenye kanuni na kuongozwa na maadili, hatuwezi kuiba mali za wananchi. Ni dhambi, ni kukosa uzalendo. Watu wamekalia kufoji risiti za manunuzi, mafuta ya magari mpaka risiti za teksi.

Kuna wakati nilikuwa kituo cha mafuta pale Morogoro.  Niliendesha gari la ofisini, Dada mhudumu nikamwambia anijazie mafuta ya laki na nusu. Hayo yalikuwa kwa gharama ya ofisi. Nikamwambia anipe risiti pia. Kisha nikamwambia  anijazie mengine ya shilingi hamsini elfu. Hayo ni kwa gharama yangu na ya safari zangu binafsi. Anipe risiti pia.

Alipomaliza kunijazia mafuta dada yule mhudumu akaniuliza; “ Sasa kaka na mimi nitakula wapi?”
Nikampa shilingi elfu mbili, kisha nikamwambia; “ Hiyo inatoka mfukono mwangu, ikusaidie kwa chakula!”
Hakika, katika kazi zetu hizi, na maisha ya kila siku, tunakumbana na changamoto nyingi. Hulka ya wizi imekuwa  tatizo. Wengi wanatamani  ‘kupiga’  kwa vile tu mwingine ‘ anapiga’ na kwamba mambo yake yanakwenda vizuri.

Tunatafuta njia za mkato katika kupata mafanikio. Hatutaki kuumiza vichwa na kuongeza juhudi za kazi ili tupate zaidi. Ni tatizo. Sasa kama kila anayekabidhiwa ofisi atafanya kazi ya ‘ kupiga’ nchi itabaki na nini? Na wananchi watakuwa katika hali gani?

Na shida ni pale wanaojitahidi kuishi maisha adilifu wanaposhushwa majukwaani na kufanywa kuwa wahalifu! Maana, katika sehemu nyingine wenye kujitahidi kuishi maisha adilifu hata kwenye kazi wanaambiwa; “ Wanajifanya wazalendo sana”

Na sehemu nyingine huwa ni mwanzo wa kuundiwa zengwe na hata kutengenezewa kashfa za kutungwa.
Na nahofia, kuwa kauli ya Mizengo Pinda ya kusema; ‘ Pigeni Tu!’ inaweza kutafsiriwa vibaya kwa wenye hulka ya ‘ kupiga’ kwa maana ya kuiba. Kwamba Pinda amewaambia ‘ kupiga ni ruksa!’ – Kwa maana ya kuiba!

Hapana, ni kweli maisha ni magumu, lakini, tuifikirie pia nchi yetu na watu wake. Ni wakati sasa wa kuwaundia zengwe wale wenye hulka ya ‘ kupiga’ kwa maana ya kuiba. Kwamba jamii iwaite kwa majina yao halisi- WEZI WA MALI YA UMMA. Full Stop!

Maggid,
Dar es Salaam.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment