WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, July 1, 2013

Kwani siasa ni nini?
MARA nyingi hatujiulizi swali hili. Kwenye kitabu chake cha mwaka 1962;  TUJISAHIHISHE, Mwalimu Julius Nyerere  anaandika; “Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi.”

“Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tunzo! Anasahu kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa  ujumla.

“Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuiya, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi.

Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakiuhukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama.”

Mwalimu Nyerere anaendelea; “Dalili nyingine ya ubinafsi na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema; nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko. Lakini bado tunao wanachama   ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua.” 

Miaka 50  baadaye, yaani leo hii, bado aliyoyaandika Mwalimu yanahitaji kusomwa na kufuatwa na kila aliye makini ndani na nje ya chama alichoshiriki kukiasisi, CCM. Hakuna ajuaye na aliye hodari kwa kila jambo.

Hata Mwalimu alikuwa tayari kujisahihisha, nasi hatujachelewa. Tunayaona makosa yakitendeka. Tusione aibu ya kujisahihisha.

Maana, chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye itikadi, madhumuni, shabaha na malengo yenye kufanana. Ni chama kilichojiwekea kanuni za kufuatwa kwa viongozi na wanachama wake. Ni vigumu kukawa na chama cha siasa kitakachodumu muda mrefu kikiundwa na watu wenye itikadi tofauti na wasiokubaliana katika madhumuni na malengo ya msingi.

Kikishindwa kuwa na hivyo muhimu, hakiwezi kuwa na kanuni zitakazofuatwa. Hicho ni chama kwa nadharia, lakini kimatendo, ni mkusanyiko wa vikundi vya watu wenye malengo, madhumuni na shabaha tofauti chini ya kivuli cha “chama nadharia”.

Tunahitaji uwepo wa utamaduni wa vyama vya siasa vyenye kuendesha mambo yake kwa uwazi na ukweli. Katika siasa, ukweli na uwazi ni vitu muhimu sana, na hivi kamwe visipuuzwe kwa kujali maslahi ya mtu  badala ya jumuiya. Kwani, siasa ni mapambano ya hoja. Siku zote, kinachopingwa iwe ni hoja na si mtu aliyetoa hoja. Tusizihukumu hoja kabla hazijawasilishwa.

Tujenge utamaduni wa kujifunza kusikiliza hoja zinazotolewa, tuzijibu hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali uhusiano wetu na mtoa hoja.

Tujifunze kujenga hoja na hata kubomoa hoja za wengine, kwa nguvu za hoja, si kunyume chake. Hayo ndio mambo ya siasa na hufanywa na wanasiasa. Tusijifunze kujenga fitna, mizengwe na majungu. Hayo ni mambo ya umbeya na hufanywa na wambeya, hayaendani na ustaarabu wa kisiasa.

Na tutafakari madhara yanayotokana na wanasiasa  wenye malengo binafsi ya  kuwania madaraka bila kuwa na misingi ya kiitikadi na malengo yaliyo bayana. Wanasiasa wasioweka bayana kanuni za kuwaongoza. Hawa hujali sana maslahi yao, watakuwa tayari kufanya lolote, ilimradi waingie au wabaki madarakani. Hawaamini katika siasa kwa maana tunayoifahamu.  Kwao wao, itikadi, malengo, madhumuni na shabaha ya chama yatabaki kuwa ya chama, na wao wanayo ya kwao wenyewe! “Kila mtu na lwake!”

Na siasa ni nini? Siasa ni hatua za majadiliano endelevu. Majadiliano yasiyokoma. Hakuna kitu kibaya katika siasa kama kutafuta njia za mkato katika kufikia malengo, njia hizi zina gharama kubwa kwa jamii. Njia za mkato uhusisha hoja za nguvu, hila na hata vitisho.

Ni kweli,  kuwa demokrasia na amani katika jamii huenda isiwepo bila wachache kukubali matakwa ya wengi. Matakwa ya wengi hujulikana kwa njia ya mazungumzo ya wazi wazi, kwa mbinu za wazi kisiasa. Vivyo hivyo, kinyume chake, yaani matakwa ya wachache. Hata baada ya majadiliano, baada ya uchaguzi, wachache walioshindwa wanapaswa kukubali kushindwa. Wanapaswa kufanya hivyo kama kulikuwepo na uhuru na haki katika majadiliano na hata uchaguzi.

Hata hivyo, kukubali kwao kushindwa hakuwanyimi haki yao ya kuendelea kuamini katika kile walichokiamini. Hapa demokrasia inawapa haki watu hawa, na ukweli unawapa wajibu wa kuyaendeleza mawazo yao, hadi pale walio wengi wayakubali. No comments:

Post a Comment