WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, July 16, 2013

Hawawi kama Nyerere, labda kama Mkapa au Kikwete
UMEWAHI kujiuliza swali hili moja tu? Kwamba kuna tofauti gani kubwa ya msingi baina ya marais Benjamin Mkapa na Thabo Mbeki na waliowafuatia madarakani, Jacob Zuma na Jakaya Kikwete?

Au ungerudi nyuma kidogo tu; kwamba ilikuwapo tofauti gani kubwa baina ya marais Nelson Mandela na Julius Nyerere na waliowafuata yaani Thabo Mbeki na Ali Hassan Mwinyi?

Unaweza ukaenda mbali zaidi. Ukajiuliza kuhusu tofauti baina ya Nicholas Sarkozy na Francois Hollande kule Ufaransa, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta  hapo jirani Kenya na Iddi Amin Dada na Prof. Yusuf Lule pale Uganda.

Sizungumzii tofauti za kimwonekano, nguo wanazovaa au matamshi ya lugha mbalimbali. Ninachozungumzia ni tofauti katika utendaji wao wa kazi. Nimejaribu kuwatafiti kidogo na nimebaini kwamba kuna tofauti kubwa baina ya viongozi wa bara letu hivi sasa kulinganisha na enzi za uhuru.

Hebu angalia kuhusu Nyerere na Mandela. Ingawa wameongoza katika nyakati tofauti, Nyerere na Madiba ni watu wa rika lililokuwa pamoja wakati wa harakati za kudai uhuru, ingawa kiongozi huyo wa Afrika Kusini alikuwa mkubwa kidogo.

Nyerere alikuwa mzuri kama msomi (intellectually) na mzuri pia kwa siasa za watu wa hali ya chini (grassroots politics). Ndiyo maana aliweza kuja na kitu kama Azimio la Arusha lililoeleza kinaga ubaga wapi Tanzania inatakiwa kuelekea.

Kisomi pia, Nyerere aliweza kuandika vitabu na maandishi ya kutosha kuhusu msimamo wake wa masuala mbalimbali. Wengi pia wanamsifu kwa namna alivyoweza kutafsiri vitabu vya Kiingereza kwa lugha ya Kiswahili katika namna rahisi kabisa.

Msomi maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Profesa Ali Mazrui, anasema katika Bara la Afrika, mwanasiasa pekee anayeweza kusema alikuwa na kiwango cha usomi wa Mwalimu Nyerere ni aliyekuwa Rais wa Senegal, Joseph Sedar Senghor.

Katika siasa za watu wa hali ya chini, Mwalimu pia alikuwa juu. Mara nyingi akionekana anacheza mchezo wa bao na wananchi ambao wengi wao walikuwa wakulima na wafanyakazi wa kiwango cha chini kabisa.
Hawa ni watu ambao katika hali ya kawaida kabisa wasingetaraji kukaa meza moja na rais. Mwalimu alionekana mara nyingi akiwa amevaa nguo kama mkulima wa kawaida na akilima.

Katika Dar es Salaam ya miaka ile ya 1960 na 1970 ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake walikuwa ni Waislamu, Nyerere alionekana kama mwenzao kwa tabia yake ya kuvaa kofia za aina ya baraghashia.
Nilisoma katika kitabu kimoja cha Mohamed Said kwamba wakati wa msiba wa Abdul Wahid Sykes, 
Nyerere alisimama msibani muda wote kama watu wa kawaida na hata alipoletewa kiti hakukaa. Alitembea pia kwa mguu kutoka Gerezani ulipokuwapo msiba hadi Kisutu kwenye makaburi.

Huyu alikuwa mtu wa watu. Ukimlinganisha na Mandela, kama msomi, Nyerere alikuwa juu kidogo ingawa Mandela alikuwa msomi pia wa kiwango cha kuridhisha.

Harakati zake za kisiasa zilimfanya Mandela kuwa kipenzi cha watu wa chini kama ilivyokuwa enzi za Nyerere. Kwenye kitabu chake cha The Long Walk to Freedom, Mandela anaeleza namna alivyovutiwa na Mwalimu Nyerere kwa vile alimkuta akiwa anaendesha gari mwenyewe wakati tayari alikuwa kiongozi wa juu kabisa wa Taifa la Tanganyika.

Hivyo, Mandela na Nyerere walikuwa wazuri kwa siasa za watu wa chini. Nyerere alimzidi Mandela kama msomi lakini Mandela alimzidi Nyerere kwenye eneo la uadilifu (integrity).

Kwa kiasi fulani Mwalimu alikuwa kipenzi cha wazungu. Mwenyewe pia aliwapenda wazungu na ndiyo maana hata hati (mwandiko) yake ilikuwa ya kizungu kabisa. Mandela alikuwa chukizo la makaburu. Kwa mateso ambayo yeye binafsi na familia yake waliyapata kwa makaburu, ni vigumu kuona aliweza kuwasamehe kabisa.

Hakulipiza kisasi. Kwenye utawala wa Nyerere, kuna hadithi za watu waliowekwa kizuizini bila makosa. Kuna walioharibiwa kabisa maisha yao. Na pia, Nyerere hakutaka kuweka kifungu cha Haki za Binadamu (Bill of Rights) katika Katiba ya Tanzania.

Kwa matendo yake haya, Nyerere amezidiwa na Mandela kwa kiasi fulani kwenye eneo hili la uadilifu. Mandela ni kama vile hakumuonea mtu. Kuna wakati, alimwachia kiti chake cha urais mpinzani wake namba moja wa kisiasa, Chifu Mongosuthu Buthelezi.

Hata hivyo, tunaweza kukubaliana kitu kimoja; kwamba Mandela na Nyerere wote walikuwa wasomi, wanaojali watu wa chini na wenye kiwango maridhawa tu cha uadilifu. Ila walikuwa wakizidiana kidogo kwenye maeneo fulani fulani.

Ukichunguza kwa makini, utabaini kwamba wengi wa waliokuwa viongozi wa Afrika katika zama za kudai uhuru na wakati wa uhuru, walikuwa na sifa zinazofanana na zile za Mwalimu na Mandela.
Tizama kwa Kwame Nkrumah na Milton Obote. Angalia kwa Modibo Keita na Ahmed Sekou Toure. Watazame Gamal Abdel Nasser na Tom Mboya au Jaramogi Oginga Odinga.

Tangu kwa Patrice Lumumba na Augustinho Neto. Wote, kwa ujumla wao, walikuwa na mambo makubwa matatu ingawa kiwango walipishana kidogo; Usomi na Uelewa wa Mambo, Uadilifu na Wafuasi.Tuje kwa waliowafuatia.

Mzee Mwinyi ni msomi wa kiwango chake (ila si kama Nyerere). Kwa bahati nzuri, alikuwa na mapenzi ya dhati kwa masikini. Ndiyo maana sera zake za RUKSA zilisaidia sana kubadilisha maisha ya watu.
Mzee Mwinyi pia alikuwa na uadilifu. Ndiyo maana leo anaweza kupita popote hapa nchini na watu wakamshangilia. Hata hivyo, hakuna anayemkumbuka Mzee Mwinyi kwa usomi wake wala uadilifu wake. Atakumbukwa zaidi kwa kuondoa shida za wananchi zilizokuwapo wakati akirithi madaraka.
Mbadala wa Mzee Mandela alikuwa Mbeki. Mbeki alikulia kwenye mafunzo ya Oliver Tambo.
Nilizungumza na Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe, majuzi tu na akaniambia Tambo alikuwa miongoni mwa viongozi wenye bongo zinazochemka kweli kweli. Alikuwa akimlinganisha na Mwalimu.

Mbeki hakukumbwa na kashfa yoyote ya kifisadi. Alikuwa mwadilifu. Alikuja na mipango kabambe ya kulikwamua bara la Afrika kiuchumi kama vile NEPAD na African Renaissance. Hata hivyo, ni katika siasa za watu wa chini ndipo Mbeki alipokwama kabisa.

Mbeki alikuwa mtu mshaufu. Mwenye majidai na asiyeingilika kwa watu wa chini. Na ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa Jacob Zuma kumpindua. Thabo hakuwa kabisa na watu wa kumpigania.
Zuma naye ana yake. Hakuwahi kumaliza hata sekondari. Hayumo katika kundi la wasomi. Uadilifu wake unatia shaka kutokana na kashfa mbalimbali zilizomkuta hadi sasa. Ila Zuma ana kitu kimoja, watu.
Kwenye siasa za wananchi Zuma hana mfanowe nchini Afrika Kusini. Nilikuwa Johannesburg muda mfupi kabla ya uchaguzi uliomwingiza madarakani na nakumbuka kumsikia aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ANC, Julius Malema (sasa ametimuliwa), akisema yu tayari kufa ali mradi ‘JZ’ aingie madarakani.
Mkapa alikuwa sawa na Mbeki. Mipango mikubwa mikubwa ya kujikwamua kiuchumi na utetezi wa mfumo wa utandawazi ambao wananchi wengi walikuwa hawaujui.  Uadilifu wake unatia shaka kutokana na tuhuma mbalimbali zilizomkabili.

Hata hivyo, sehemu ambayo Mkapa hakufanya vizuri, ukiondoa kwenye uadilifu, ni kwenye suala zima la siasa za watu wa chini. Nina imani, zikipigwa kura leo kati ya Mkapa na Mwinyi, Mzee Ruksa ataibuka na ushindi asubuhi na mapema.

Mkapa hakuwa na nguvu kwa watu. Na ndiyo maana, alishindwa kuwashawishi watu wamchague mtu aliyemtaka yeye amrithi urais. Akaamua kwenda na ‘muvu’ kwa kuchagua mtu ambaye “wenye chama” walimtaka.

Kikwete naye ni msomi (ingawa si wa kiwango cha Nyerere na Mandela) na ana uadilifu kama wa Mzee Ruksa. Alicho mahiri Jakaya ni kwenye siasa za chini. Kwenye kipindi cha kuelekea mwaka 2005, kuna watu ninaowafahamu ambao walikuwa tayari kupoteza kazi au kufa ili Jakaya aukwae urais.
Kwa hiyo, hana usomi wa kiwango cha Mwalimu. Hana uadilifu wa kiwango cha Mwalimu lakini ana ufuasi unaokaribiana na aliokuwa nao Mwalimu. Mkapa alisogelea kwenye usomi na uelewa lakini akafeli kwenye uadilifu na wafuasi.

Kama Mkapa angeendeleza ile taswira yake ya Mr. Clean aliyokuwa nayo kabla hajapata urais na kwa kiwango chake cha usomi na uelewa wa mambo, huenda angepata wafuasi wengi sana. Na naamini angeweza kufikia walau nusu ya mafanikio ya Mwalimu.

Iddi Amin hakuwa msomi lakini katika miaka yake ya mwanzoni, alikuwa akipendwa sana na wananchi. Profesa Lule alikuwa msomi mzuri lakini hakuwa na wafuasi.
Sarkozy alikuwa msomi mzuri na mwenye mipango mikubwa. Huenda alikuwa na uadilifu mzuri tu. Hata hivyo, alishindwa kwa sababu hakuwa na wafuasi. Kwa upande wake, Hollande anaonekana atapata wafuasi wengi.

Ana sera nzuri za kuvutia masikini. Matajiri wanaanza kumchukia. Anaweza asiwe msomi mzuri kama Sarkozy lakini ana wafuasi.

Katika kinyang’anyiro cha kuwania kumrithi JK mwaka 2015, naona majina mbalimbali yakitajwa. Kwenye upembuzi wangu, naona wengi wana hili lakini hawana lile.

Sioni mtu ambaye ana sifa zote tatu. Mwenye usomi na uelewa wa kutosha wa masuala muhimu, mwenye wafuasi wa kutosha na mwenye uadilifu usio na shaka.
Mambo ni yaleyale… Hatuwezi kumpata Nyerere mwingine. Ni ama tumpate kama Mkapa au kama Kikwete.

Ni mara chache miungu wanakupa vyote kama ilivyokuwa kwa Mwalimu. Hata hivyo, ni mara nyingi wanakupa hiki au kukunyima kile.
Wanasema Mungu hamnyimi mja wake.

No comments:

Post a Comment