WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, July 2, 2013

Simulizi la ujio wa Obama na Kachero wa Marekani alivyomzodoa wa TanzaniaPicture
Maofisa wa Usalama wa Marekani wakikagua barabara ya Nyerere kabla ya Rais wa Marekani, Barack Obama kupita katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere – TAZARA (picha: BurudaniKilaSiku blog)
Jana saa 8.46 mchana Rais Barack Obama wa Marekani alikanyaga ardhi ya Tanzania na kuweka historia ya kuwa Rais wa tatu wa Marekani kuzuru nchini.

Kuonesha kuwa kiongozi huyo ni kipenzi cha Watanzania, maelfu ya watu walijitokeza kwa wingi kusimama kando ya barabara ya Nyerere kama ishara ya kumkaribisha kiongozi huyo wa kwanza mweusi kuitawala Marekani.

Mara baada ya ndege yake iliyoandikwa United States of America maarufu kama Air Force One,  kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere saa 8.38 mchana ilichukua takribani dakika tisa kwa Rais huyo kujitokeza.

Obama alikuwa anatokea Afrika Kusini na kufika kwake nchini ni sehemu ya  ziara yake ya Afrika, ziara inayomulikwa kote ulimwenguni. Tanzania ni nchi yake ya mwisho na leo saa tano anaondoka kurudi Marekani.

Alilakiwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete ambaye baadaye alimtambulisha kwa viongozi wachache waliokuwa uwanjani hapo ambao ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Dk  Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Idd Seif, Spika wa Baraza la Wawakilishi Omar Pandu Kificho na Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe.

Licha ya ulinzi wa kupindukia uwanjani hapo, shauku ya wananchi waliofika uwanjani hapo ilikuwa ni 
kumwona Rais huyo akitua nchini na ndivyo ilivyokuwa, kwani mara baada ya kujitokeza kelele za shangwe na vigelegele zilisikika.

Huku akiwa ameshikana na mkewe Michelle, nyuma yao walikuwepo watoto wao wawili mabinti Sasha na Malia ambao walikuwa kivutio uwanjani hapo.

Obama ambaye muda wote alionekana mwenye tabasamu alipata fursa ya kukagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kupigiwa mizinga 21. Katika kukagua gwaride aliongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange.

Aidha Rais huyo alionekana kuvutiwa na maonesho ya vikundi vya ngoma za asili vilivyokuwa uwanjani hapo hali iliyomfanya kucheza kidogo baadhi ya ngoma zilizokuwa zinatumbuiza uwanjani hapo.

Tangu saa 3 asubuhi maandalizi ya kumpokea mgeni huyo yalianza na shughuli zote za ukaguzi wa kuingia katika uwanja wa ndege wa zamani zikachukuliwa na makachero wa Marekani na kuwaacha   wa nchini bila kazi.

Kuanzia saa 3 asubuhi jana hakuna gari lililoruhusiwa kuingia katika eneo la uwanja huo na kila gari  lililopeleka wageni lilikaguliwa na makachero wa Marekani ambao walifanya kazi hiyo kwa kutumia mbwa.
Dereva au abiria ambao walikuwa kwenye gari lililokuwa linaingia uwanjani hapo; walitakiwa kushuka   ili ukaguzi ufanyike na hapo ndipo waliruhusiwa kuendelea na safari kwa miguu na gari kuamriwa likaegeshwe au lirudi lilikotoka.

Hata katika lango la kuingilia  uwanjani, shughuli za ukaguzi nazo zilifanywa na makachero wa Marekani huku eneo lote la uwanja wa ndege ndani na nje kukiwa kumetapakaa makachero hao. Baadhi yao walikuwa na mbwa na wengine wakionekana kufunga mitambo kwa ajili ya usalama wa kiongozi wa Taifa hilo kubwa duniani.

Eneo la uwanja ambako ndege ya Obama ilikuwa itue pilikapilika za ukaguzi na ulinzi zilikuwa kubwa kwani magari na mbwa vilikuwa vinafanya doria eneo hilo mara kwa mara kuhakikisha kuwa eneo hilo ni salama wakati wote.
Picture
Makachero wakikagua gari (picha kutoka kwa rafiki via WhatsApp)
Pamoja na wingi wao katika eneo hilo, makachero hao hawakuonekana wasumbufu kwa watu ambao walikuwa wanaingia uwanjani hapo ambao wengi wao walikuwa na waandishi wa habari tofauti na karaha ambazo zimezoeleka kufanywa na makachero wa nchini.

Badala yake makachero wa Marekani walichofanya jana kuanzia asubuhi ni kuhakikisha watu ambao waliwahi wanakuwa huru kupata mahitaji muhimu kama vile maji, chai katika migahawa iliyoko ndani ya jengo la uwanja huo.

Saa 7 mchana ikiwa ni saa moja kabla ya Rais Obama kutua uwanjani hapo; makachero hao walitoa utaratibu kwa waandishi wa habari na wapiga picha wanavyotakiwa kukaa, ili kuona na kupata picha kwa ajili ya vyombo vyao vya habari.

Mara ndege hiyo ilipotua, wapiga picha wanne wa viongozi hao wawili ndio waliokuwa wanaruhusiwa kuhama kupiga picha, lakini wapiga picha na waandishi wengine hawakutakiwa kuhama hali ambayo ilifanya baadhi yao kukosa baadhi ya matukio.

Makachero hao ambao baadhi yao wanajua Kiswahili vizuri, walihakikisha muda mfupi kabla ya ndege ya Obama kutua, waliwaamuru wafanyakazi wote wa ofisi zilizoko ndani ya uwanja huo kutoka nje na kuwaachia kutumia baadhi ya maeneo ya ofisi hasa ya ghorofani kwa ulinzi.

Aidha, walionekana makachero wengine wakiwa kwenye paa la jengo la uwanja wa ndege wakifuatilia shughuli zinazoendelea uwanjani hapo.

Walikuwa wanazungumza Kiswahili fasaha hasa pale walipotoa maagizo yao kwa baadhi ya wananchi waliofika uwanjani hapo wakigundua hawajaeleweka, baadhi yao walizungumza Kiswahili.

"Akina mama tafadhali kaeni sehemu moja tu hadi hapo tutakapowapa maelekezo mengine," alisema kachero mmoja kwa Kiswahili kizuri.

Kachero mwingine ambaye alikuwa karibu na kibanda walichokaa baadhi ya waandishi wa habari ambaye alikuwa anatoa maelekezo mara kwa mara, baada ya Obama kutua na kuondoka uwanjani, alisema "Kazi hapa imekwisha sasa mko huru."

Maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikusanyika kwa wingi kumlaki Rais Obama. Barabara ya Nyerere ilifungwa kwa takribani saa tatu ikiwa ni maandalizi ya kupita msafara wa Rais huyo.

Katika makutano ya barabara za Nelson Mandela na Julius Nyerere inayotoka uwanja wa ndege, kulikuwa na ulinzi  mkali  huku askari Polisi wakizunguka na mbwa na farasi.

Ulifungwa utepe  kwenye makutano hayo wenye  onyo la kutovuka kutoka eneo moja kwenda lingine. Pia katika eneo hilo kulikuwa na gari la Zimamoto na vikundi vya ngoma vyenye sare za vitenge vyenye picha za Obama.

Wananchi walijipanga barabarani kwa matumaini ya kumwona Rais huyo kwenye gari la wazi wakati akitoka uwanja wa ndege, lakini haikuwa hivyo. 
Picture
(picha vi SufianiMafoto.com)
Hamasa zaidi  iliongezeka  baada ya msafara wa Rais Kikwete uliyekwenda kumlaki kiongozi huyo kupita akienda Ikulu na hivyo kushindwa kuvumilia na kuhamia upande wa pili wa barabara wakisubiri msafara wa Obama.

Wananchi waliojawa na shauku  ya kumwona Obama walipanda juu ya magari na pikipiki kabla ya Rais huyo kupita akiwa kwenye gari la kifahari aina ya Cadillac akipungia watu. Gari hilo linaitwa Cadillac One, Limo One au The Beast.

Baadhi ya waliozungumza na mwandishi, walieleza furaha yao kupata fursa ya kumwona na kumpungia na wengine wakitaka ziara hiyo iwe na manufaa kwa nchi na watu wake.

Katikati ya Jiji hususan Posta, baadhi ya watu walitelekeza ofisi zao kwa muda na  kujipanga barabarani kumshuhudia Rais Obama.

Baada ya king'ora cha kwanza kupita, wananchi wengi walionekana kukimbilia kwenye barabara maalumu iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya Rais huyo kupita.

Aidha, wengine walionekana kupanda juu ya majengo marefu na magari wakilenga kuona gari lililombeba Rais huyo. Wananchi hao walijitokeza katika barabara hizo tangu saa 6 mchana. 

Akizungumzia ujio wa Obama, Julius John ambaye ofisi yake iko Posta, alisema  ujio huo ni wa kihistoria na aliamua kufunga ofisi yake kumshuhudia japo gari lake.

"Kwa kweli mimi nimeridhika ingawa sijamwona yeye lakini nimeona gari lake, nilifika hapa saa sita ili niwahi kukaa mbele kwenye mstari,” alisema John.

Hata hivyo, kutokana na msongamano uliokuwapo wapo waliokuwa wakilaumu kushindwa kuona angalau gari lake na kushuhudia kelele za vifijo na nderemo zilizokuwa zikipigwa na watu waliokuwa  wamekaa mbele.

Katika maeneo hayo ya Posta, daladala zilikuwa tupu na makondakta wa magari hayo walionekana wakiita abiria ambao wengi walisikika wakisema wanasubiri kumwona Obama.

Aidha, katika maeneo hayo ya Posta mitaa mingi ilikuwa safi. Mafundi viatu na biashara nyingine ambazo hufanyika mtaani, hususan kando ya barabara hazikuonekana.

Katika maeneo ambayo msafara wa Rais ulipita, polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kudhibiti mamia ya watu waliojitokeza kumlaki.

Hali hiyo ilishuhudiwa kwenye makutano ya barabara za Nelson Mandela na Julius Nyerere eneo la Tazara baada ya watu kujitokeza na kusimama kando ya barabara.

Umati wa wananchi uliokuwa kando ya barabara ya Nyerere ulishangilia msafara huo uliokuwa katika mwendo wa taratibu kuelekea Ikulu tofauti na ilivyozoeleka kwa misafara mingi ya viongozi.

Wakati huo huo, adha ya usafiri ilikumba vyombo vya usafiri na hata waenda kwa miguu waliotumia barabara za Nyerere na Mandela baada ya kuzuiwa kwa takribani saa tatu baada ya barabara hizo kufungwa.

Tangu saa 6:30 hakuna aliyeruhusiwa kuvuka barabara ya Nyerere hadi msafara huo ulipopita saa 9:30 jioni.
Kwa upande wa eneo la Ubungo hasa mahali ilipo mitambo ya Symbion, ulinzi kutoka kwa askari Polisi uliimarishwa tangu jana.

Kulikuwa na utulivu wa aina yake tofauti na siku nyingine baada ya hata pikipiki maarufu kama bodaboda kuzuiwa kupita na kushusha abiria eneo la Tanesco.

Leo kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 5 asubuhi, barabara za Ali Hassan Mwinyi, Sam Nujoma, Morogoro na Nelson Mandela zitafungwa kwa ajili ya kupisha msafara wa Rais Obama anayefanya ziara kwenye mitambo ya kufua umeme ya Symbion, Ubungo kabla ya kurejea nchini kwake.

Barabara za Ali Hassan Mwinyi, Sam Nujoma na Morogoro zinatumika wakati Obama akienda kwenye mitambo hiyo. Wakati wa kutoka Ubungo,  msafara wake utatumia Barabara ya Mandela na Nyerere  kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere tayari kuondoka saa 5:20. 

Hakuna chombo chochote cha usafiri kinachoruhusiwa kuvuka upande mmoja kwenda mwingine wakati barabara hizo zikiwa zimefungwa.  
Wakati huo huo,  mke wa Rais Obama, Michelle na mke wa Rais Kikwete, Salma, walitembelea Makumbusho ya Taifa ambako kuna kumbukumbu ya waathirika wa bomu lililopigwa ubalozi wa Marekani, Dar esSalaam mwaka 1998 na kuua watu zaidi ya 12 na wengine 85 kujeruhiwa.

Michelle ambaye alifuatana na Sasha na Malia waliweka maua katika eneo hilo ambalo mabaki ya vyuma, magari na pikipiki zilizokuwa kwenye eneo la tukio hilo yamehifadhiwa.

Baada ya kuwasili eneo hilo ambalo lilitawaliwa na ulinzi mkali wa makachero wa Marekani huku wa Tanzania wakilinda mlangoni, wake hao wawili wa marais walikabidhiwa maua na wanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari WAMA Nakayana.

Tukio hilo lilitofautiana kwa dakika moja na tukio la bomu la Nairobi Kenya, Agosti 7, 1998 katika Ubalozi wa Marekani na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 85 kujeruhiwa.

Akiwa eneo hilo Michelle alitoa heshima zake kwa majina ya waliokufa katika tukio hilo ambayo yalibandikwa na aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Charles Stith mwaka 1999.

Waliokufa kwenye tukio hilo ni Abdulrahaman Abdallah, Paul Elisha, Ramadhani Mahundi, Abdallah Mnyola, Abbas Mwilla, Yusuf Ndange, Bakari Nyumbu, Mtendeje Rajab, Dotto Ramadhani, Rogath Said, Aimosonia Mzee na Hassan Siad.

Pamoja na tukio hilo, Michelle alilakiwa katika eneo hilo na takribani wanafunzi 300 wa shule za Dar es Salaam ambako pia alitumia muda mchache kushuhudia maigizo, ngoma za asili, dansi na sarakasi kutoka kwa kikundi cha watoto yatima cha baba watoto.

Katika tukio hilo, Mama Salma pia aliongozana na watoto wake wawili ambao ni Rashid na Mwanasha waliofuatana na baadhi ya familia ya Kikwete ambao nao walikutana na kusalimiana na Michelle.

Katika tukio la bomu lililotokea jijini Nairobi, tarehe na mwaka huohuo na kutofautiana kwa dakika moja na lile lililotokea Dar es Salaam, watu 44, kati yao Wamarekani 12 na wafanyakazi wa ubalozi 32 walipoteza maisha.

Awali kabla ya ujio wa wake hao wa marais, almanusura hali ya amani itoweke katika eneo hilo la Makumbusho lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam ambapo kiongozi wa usalama kwa upande wa Tanzania alizua mtafaruku na mlinzi wa Obama. Kisa cha mtafaruku huo, ni baada ya kiongozi huyo kumgomea mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Selina Wilson kuingia ndani kwa kuwa kitambulisho chake kinaonesha amepangiwa eneo la Symbion na si Makumbusho, ingawa kwenye orodha ya waandishi wa Makumbusho jina lake limo.

Pamoja na kiongozi huyo kumgomea mwandishi huo, mlinzi wa Obama aliingilia kati na kumtaka Wilson aingie kwa kuwa pamoja na kitambulisho chake kukosewa, jina lake lilikuwapo, jambo lililomkera kiongozi huyo wa usalama na kuishia kumsukuma Celina huku akifoka na kumtaka aondoke.

"Nimesema ondoka hapa, jina lako sawa lipo lakini kitambulisho kinaonesha umepangiwa sehemu nyingine," alisema na kumsukuma, jambo ambalo lilimuudhi mlinzi wa Obama, ambaye alikwenda na kumzuia kiongozi yule huku akisisitiza mwandishi aingie.

"Hapa sioni tatizo, tulia dada tatizo lako litashughulikiwa. Lakini wewe ndugu yangu, kwa nini unamsukuma huyu dada? Ndivyo mnavyofundishwa?" alihoji askari huyo wa Marekani ambaye baadaye alimruhusu Celina akaingia na kufanya kazi yake.

Nje ya eneo hilo la Makumbusho, umati wa watu ulifurika wakitaka kumwona Michelle huku wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakiwa wananing'inia madirishani.

---
via HabariLeo

No comments:

Post a Comment