WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, July 31, 2013

Mwenge juu ya Kilimanjaro, umulike hadi nje, ulete kitu gani?Tunachokishuhudia hivi sasa ni hangaiko kuu lililotukumba kutokana na kushindwa kwetu kujiletea maendeleo tuliyojiahidi sisi wenyewe yapata miongo mitano iliyopita.

Nafsi zetu zinatusuta, na zinapotusuta tunakataa kukubali kwamba tunastahili kusutwa, na badala yake tunatafuta kila aina ya visingizio ili tuepuke uwajibikaji. Hebu turejee historia yetu kwa ufupi.

Tulipopata Uhuru tuliiahidi dunia, huku tukijiahidi sisi wenywe (hapa nazungumzia Watanganyika) kwamba tutafanya kazi kwa bidii na maarifa kuijenga nchi yetu na kuweza kuonyesha matunda mazuri zaidi kuliko yote waliyofanya Waingereza katika kipindi cha miaka arobaini waliyotutawala.
 Mwenge juu ya mlima Kilimanjaro
Mwaka 1958, muasisi wa Taifa la Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere alitamka, kwa niaba yetu, kwamba tungependa kuwasha mwenge na kuuweka juu ta Mlima Kilimanjaro, umulike nje ya mipaka yetu na ulete tumaini kila kusiko kuwa na tumaini, upendo kulikojaa chuki, na heshima kulikojaa dharau.

Haya ni maneno yaliyofanana sana na yale ya Mtakatifu Francisco wa Asissi, ambaye aliyafunga maisha yake katika utumishi na huduma kwa masikini ingawaje alitokana na familia tajiri ya mjini Assisi na katika ujana wake alishiriki katika biashara na kukuza ukwasi wa baba yake.

Baada ya “kuona mwanga,” Francisco aliukana ukwasi wa familia yake na akajikita katika utumishi wa watu na viumbe hai wengine. Ni kwa heshima yake ulianzishwa utawala wa Wafransiska (Franciscans) ambao itikadi yao inakumbatia umasikini na unyenyekevu katika utumishi wa Mungu na watu wake.

Mwaka 1961, Mwalimu aliwaambia Waingereza (kupitia Richard Turnbull, gavana wa mwisho) kwamba angewaalika baada ya miaka kumi waje wajionee maendeleo ya Tanganyika waliyokuwa wameiacha masikini, hio,  hahehahe, baada ya utawala wao wa miaka arobaini.

Na kweli, miaka kumi baadaye, aliwaalika na wakaja kulikuta Taifa lililojiamini na lililokuwa linaonyesha kila dalili ya kupiga hatua za kusonga mbele. Desemba 1971 nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu na nilikuwa mwongozaji (guide) wa wageni mashuhuri (VIP) wa kitaifa. Nilishuhudia binafsi ari na fahari iliyokuwepo wakati wa maadhimisho hayo, pamoja na hali tete ya usalama iliyosababishwa na kile kilichoelezwa kuwa njama za Wareno na vibaraka wao wa ndani.   

Wakati huo Tanganyika ilikwisha kuungana na Zanzibar kuunda taifa jipya la Tanzania, na hatima ya nchi yetu ilikuwa inaandikwa kwa ustadi mkubwa. Tulikuwa na viwanda vyetu vya nguo, vifaa vya kilimo na kadhalika, tulikuwa na asasi zetu za fedha na biashara, tulikuwa na uhuru wetu wa kuwaambia wakuu wa dunia wakome na wakakoma.

Tulijenga msingi, angalau mwanzo tu, na matumaini yalikuwa makubwa juu ya mustakabali wa nchi yetu. Tulikuwa ni nguzo kuu ya mapambano ya kulikomboa bara la Afrika, na vita ya ukombozi ilikuwa inarindima Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Namibia na kwingineko.  Ilikuwa fahari kubwa kuwa Mtanzania.

Miaka hamsini baada ya Uhuru, tumekuwa wanyonge zaidi. Sababu kubwa ya unyonge huu ni kwamba hatujafanikiwa kufasiri ndoto za zama zile kwa kuwapa wananchi wetu, hasa masikini kabisa miongoni mwao, matumaini, angalau matumaini tu, ya maisha bora kwa wao wenyewe au kwa uzao wao. Badala yake, katika medani kadhaa, tumewapa sababu za kukata tamaa kabisa.

Naomba nieleweke vyema hapa. Hali ninayoieleza haikuanza leo hii wala jana, wala juzi. Tunaweza kuonyesha ni jinsi gani tulivyoanza kuteleza taratibu tangu awamu ya kwanza kabisa, chini ya uongozi wa muasisi tunaye muenzi. Hili nimeliandika mara nyingi mno, na sidhani kwamba yupo yeyote anayeweza kushuku dhamira yangu.
Tatizo ninaloliona ni kwamba hatutaki kuyajadili matatizo yetu, na badala yake tunaona faraja katika kuyafunikiza, kama vile tunaamini kwamba yasipoonyeshwa hadharani, yasipoonekana na kujadiliwa, yatatoweka.  Mawe!

Hayatoweki, na badala yake kila siku  yanakua na kuchukua sura mpya, mbaya zaidi na ya hatari zaidi. Kila unapotokea mlipuko watawala wetu wanadhani kwamba ni tatizo jipya, kwa hiyo wanaushughulikia mlipuko huo kwa nguvu zao zote (nguvu zao zote kwa maana halisi ya nguvu zisizo kiasi, nguvu za “kupiga,” si kwa umahiri wowote wa tafakuri na utafiti wa utatuzi wa suluhu).
Tofauti na tafakuri, kupiga ni rahisi kwa watawala, kwa sababu wakati tafakuri inawahitaji wao ndio watafakari, kupiga hakuwahitaji wao wafanye lolote zaidi ya kutoa amri, “Piga!” Wapigaji wapo wa kutosha.

Kwa bahati mbaya (nzuri kwa wengine), historia inatuonyesha (pale tunapotaka kuona) kwamba kila kipigo cha uonevu huzaa uadui usioisha, uhasama wa kudumu na ghadhabu za masafa marefu. Aidha historia inatufundisha (pale tunapokuwa tunafundishika) kwamba jamii haziburuzwi kwa maguvu ili zipate maendeleo; jamii hujenga utashi wa maendeleo taratibu, kila kizazi kikijenga juu ya msingi ulioachwa na kile kilichotangulia, kwa kudunduliza (incrementally).

Ule msemo wa zamani, kwamba mchungaji mmoja anaweza kuwaswaga ng’ombe mia kwenda mtoni, lakini wachungaji mia hawana uwezo wa kumlazimisha ng’ombe mmoja tu kunywa maji, unahusika hapa.

Naamini kwamba haya yote tunayajua, hata kama kwa sababu fulani, zilizofichika na zilizo wazi, hatutaki, au hatuwezi kuyaishi (kwa maana ya kuyatafsiri katika maisha yetu na kazi zetu).
Kwa mfano, tuchukue “ukorofi” wa baadhi ya wananchi wa Mtwara kuhusu gesi. Wanapigwa. Ikija kutokea “ukorofi” wa wananchi wa Kigoma kwa gesi hiyo hiyo, watapigwa. Wananchi wa Dodoma wakiandamana kuhusu madhara ya urani, watapigwa. Halafu wananchi wa Mbeya wakihoji juu ya makaa ya mawe, wapigwe, na kadhalika.

Ni dhahiri kwangu kwamba nchini humu, na katika maeneo mengi yaliyotofautiana kwa maumbile, wananchi wanazo sababu lukuki za kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa na watawala. Ikiwa kila watakapoandamana, kulalama au kukataa kutii amri wanazoziona kama za kuwaumiza watapigwa, kipigo kitakuwa ni kila mahali nchini.

Tayari, katika maeneo kadhaa, kipigo kimekuwa ni jambo la kawaida. Tayari tumeona wazi wazi ambavyo watu wameumizwa kwa vipigo nje ya hukumu ya sheria. Bado tunasema watapigwa zaidi?

Ule mwenge tuliosema tutauweka juu ya Mlima Kilimanjaro (hadi leo tunaimba wimbo huu) ni wa kueneza vipigo kila ambako hakuna vipigo, vilio mahali pasipo na vilio na simanzi kwa wote wasio na simanzi?

No comments:

Post a Comment