WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, July 17, 2013

Nyuma ya ushujaa wa huyu Mandela yupo Kambarage!
UKIZUNGUMZIA mashujaa wa Afrika ni lazima kutaja majina ya Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa Kongo, Benjamin Nnamdi Azikiwe na Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria, na wengine wengi, orodha inaweza kuwa ndefu lakini si ndefu kiasi hicho, na bila shaka juu ya orodha hiyo yuko Nelson Rolihlahla Mandela na Julius Kambarage Nyerere.

Katika orodha hiyo ndefu, dunia na hata baadhi ya Watanzania wanamjua au kumsikia zaidi Mzee Mandela au Madiba kama wanavyopenda kumuita watu wake. Mzee Madiba yuko taabani hospitalini, bila shaka si rahisi tena kuona tabasamu lake, haitakuwa kazi rahisi kuona macho yaliyobeba uchungu wa mateso makali ya serikali ya kibaguzi lakini yanayohubiri amani na msamaha, walau  kitu kimoja kiko dhahiri popote na kwa yeyote anayetaka kukiona, ni jinsi historia ilivyomuandika, maandishi yako wazi kwa kila mwenye macho ya kuona, na akili ya kuelewa, yu aelekea kuvikwa taji ya haki.

Ni vigumu kweli kuandika au kumzungumzia mtu wa kiwango cha Madiba,  lakini inaweza kuswihi kuanza na mchapuo huu. Mapema mwaka  2005 wakati huo akiwa Seneta, Barack Obama, alipata fursa kuhudhuria kipindi cha television cha Oprah Winfrey na katika mazungumzo, Oprah alimpatia fursa  Obama ya kumpa ujumbe wowote anaotaka ampelekee Mzee Nelson Mandela.

Obama aliingia chumba cha nyuma ya studio ya Oprah kuandika ujumbe huo kwa Mandela, ilipoonekana amechukua zaidi ya muda uliotarajiwa katika kuandika ujumbe huo, msemaji wake Roberts Gibbs alimfutata kumwangalia ni kitu gani kimemchukulia muda namna hiyo.

Akiwa bado anatafakari nini kuandika, Obama alimwambia msemaji wake; "Ni lazima mnipe muda wa kutosha, huwezi ukaandika ujumbe mwepesi mwepesi tu kwa Nelson Mandela". Anaandika  mwandishi Michael D. Shear wa New York Times, toleo la Juni 27, mwaka 2013.

Hakuna ubishi juu ya ushujaa wa Nelson Mandela na heshima anayopata duniani, yeye ni ishara ya amani na maridhiano, ni alama ya ushirikiano dhidi ya chuki na visasi. Ni Mwafrika pekee mwenye sanamu katika eneo maarufu jijini London la Parliament Square, sanamu yake ikiwa sambamba na sanamu za watu maarufu duniani kama Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, Waziri Mkuu Uingereza Winston Churchill.

Lakini huyu Mandela amefikaje hapo? kama Waswahili wasemavyo ukiona vyaelea ujue vimeundwa, bila shaka Nelson Mandela wa leo asingekuwa Mandela huyu tunayemfahamu bila kuwepo juhudi za watu waliokuwa na fikra na misimamo thabiti ya kupambana dhidi ya ubaguzi rangi wakati akiwa gerezani kwa miaka yote 27 na hata kabla ya hapo.

Miongoni mwa watu muhimu waliomfanya Mandela huyu awe hivi alivyo leo, anayeweza kuchukua nafasi ya kwanza ni Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza Tanganyika na Tanzania, msimamo wa dhati na usioyumba wa Nyerere dhidi ya aina zote za dhuluma ndiyo umejenga msingi ushujaa wa Mandela unaojulikana duniani leo.

Kwa maneno yake mwenyewe, Nelson Mandela, katika dhifa aliyoandaa kwa heshima ya Mwalimu Nyerere, Oktoba 17 mwaka 1997, alimwelezea Mwalimu kama mtu aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Jumuiya ya Madola kuitenga Afrika Kusini ya kibaguzi, baada ya mauaji ya Sharpville.

"Huyu ni mpigania Uhuru ambaye aliitika wito wa Chifu Luthuli kuungana na Trevor Huddleston kuanzisha vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi nchini Uingereza mwaka 1959, kiongozi ambaye juhudi zake katika mkutano wa Jumuiya ya Madola zilisababisha Afrika Kusini ya kibaguzi kutengwa, baada ya mauaji ya Sharpville.
Nilipata bahati kukutana naye miaka mingi iliyopita, mwaka 1962, nilipozuru Tanzania kutafuta msaada tulipoanzisha mapambano ya silaha. Wakati huo, kama ilivyo sasa, nilishangazwa na msimamo wake, hamu yake ya kutaka haki na usawa popote, na dhamira yake kwa maslahi ya Afrika"

Wakati tukielekea kupata Uhuru, Mwalimu pamoja na kuwa kiongozi wa taifa changa hakusita kuweka wazi msimamo wake ambao bila kuwa na ujasiri wa kipekee, viongozi wachache sana wangeweza kuwa na msimamo wa namna hiyo hasa msimamo wenyewe unapowawekea wale wanaotarajiwa kuwa wahisani wako.
Mei mwaka 1961 kuelekea mkutano wa mawaziri wakuu wa Jumuiya ya Madola, huku Waziri Mkuu wa Afrika Kusini akitarajiwa kuhudhuria mkutano huo, Mwalimu aliandika makala kwenye gazeti la London Observer ikiweka wazi msimamo wa Tanganyika akisisitiza kuwa Tanganyika haitajiunga Jumuiya ya Madola kama Afrika Kusini wataendelea kuwa wanachama.

Makala hiyo iliyohitimishwa kwa maneno mazito yenye msisitizo; "To vote South African in, is to vote us out" kwamba kuwakubalia Afrika Kusini uanachama ni kutukataa sisi, iliamsha hamasa kubwa dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Mwandishi nguli wa masuala ya Jumuiya ya Madola ambaye pia ni mwasisi mwenza wa Umoja wa Waandishi wa Habari wa Jumuiya ya Madola (CJA), Derek Ingram, anazungumzia hatua hiyo ya Mwalimu kuwa ilisababisha shinikizo kubwa kwa Afrika Kusini mpaka ikajitoa; "His move stepped up the pressure on South Africa and led to its withdrawal a few days later."

Mchango wa Mwalimu katika harakati za ubaguzi hauishii hapo, Juni 26, 1959 Kamati ya Jumuiya za Kiafrika (CAO) iliitisha kikao katika ukumbi wa Holbourne jijini London, kuwataka Waingereza wasusie bidhaa za Afrika Kusini, hasa matunda yaliyokuwa yanauzwa kwa wingi katika miji mbalimbali ya Uingereza katika vuguvugu lililoitwa Boycott Movement, Askofu Mkuu Trevor Huddleston, Mwalimu Nyerere na Kanyama Chiume wa Malawi ndiyo walikuwa wasemaji wakuu katika hadhara hiyo na waasisi wa vuguvugu hilo lililokuja kujulikana baadaye kama Ant - Apartheid Movement (AAM).

Tangu mwanzo wa miaka ya 1960 mchango wa AAM katika kuutokomeza ubaguzi wa rangi ulikuwa hauna kifani, lakini pia ikumbukwe kuwa vuguvugu hilo halikuwahi kuwafurahisha wakubwa kwa sababu ya maslahi yao Afrika Kusini.

Pamoja na Chama cha Labour cha Uingereza, kuahidi kuacha kuiuzia silaha Afrika Kusini kama kingeshinda uchaguzi lakini hata baada ya kuingia madarakani kwa Waziri Mkuu wake, Harold McMillan, ahadi hiyo ilishindwa kutekelezwa kwa vitendo.

Hata alipozuru Afrika Kusini na kutoa hotuba yake maarufu katika Bunge la Afrika Kusini; “The wind of change is sweeping across Africa,” pamoja na kuona huo upepo wa mabadiliko uliokuwa unalikumba Bara la Afrika wakati huo, McMillan siyo tu hakuunga mkono shughuli za AAM lakini alilaani harakati hizo.

Hili halishangazi kwa vile kwa mujibu wa mtandao wa South African History on line (SAHO), katika miaka hiyo ya 1950 Uingereza ilikuwa mshirika mzuri wa biashara wa Afrika Kusini, zaidi ya asilimia 30 ya bidhaa zilizoingizwa Afrika Kusini zilitoka Uingereza, asilimia 28 ya mauzo ya bidhaa za nje za Afrika Kusini ziliuzwa Uingereza. Ukiondoa uhusiano huo wa kiuchumi, kati ya mwaka 1946 na 1959 kulikuwa na Raia wa Uingereza zaidi ya 113, 000 waliokuwa wakiishi Afrika Kusini.

Hizi ndizo juhudi zilizoweka msingi wa mapambano ya dhati dhidi ya aina zote za dhuluma ambazo kwa hakika zisingeweza kufika mbali au kufanikiwa kwa kiwango hicho bila kuwa na nguvu ya Mwalimu Nyerere ambaye, msimamo wake dhidi ukandamizaji wa aina yoyote ile ulikuwa dhahiri hata kwa wasiokubaliana naye.

Kujitolea kwake kulikoifanya Tanganyika na kisha Tanzania kuwa kimbilio na ngome ya kutumainiwa na wapigania uhuru wa Kusini mwa Afrika katika mazingira hatari kama vita baridi vya wakati huo, kwa kiwango cha juu kabisa pamoja na mambo mengine yamechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Afrika Kusini ya Mandela na hata Madiba mwenyewe kuwa jinsi walivyo leo. Na ni uungwana tu kusema kuwa nyuma ya fahari aliyonayo Mandela leo, yuko Julius Kambarage Nyerere aliyeongoza kuwapinga makuburu si kwa sababu ya rangi yao bali matendo yao.

1 comment:

 1. Suggest one of the girls is thinkking of dancing for money. The gods will cut her time severely if she does that.
  Normally they would fight it, provide that temptation of denial, but they share they don't, and it's because she doesn't have much coming anymore. With all the lifetimes of hedonism and deviacy this individual needs to clean herself up and live a life of decency and respectability. But being born as mom's children should show them they're near their ends already.
  The theory is the English Monarchy provided for a killer who hunted the prostitutes of London, protecting men and the families of the city. JAck the Ripper was a hero.
  Men are weak. Women are traditionally the enforcers of dececy. When they abandon this role and become corruptors of men may god have mercy on their souls. Expect this is the primary reason of the deterioration and decay of mankind.
  Slipping slow away.

  ReplyDelete