WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, July 7, 2013

Angalia tofauti hii kati ya Marekani na Tanzania


 


Vumbi la ujio wa Barack Obama limeshatua. Ni ziara iliyokuwa na mafanikio makubwa. Kwa nchi ya Kiafrika kutembelewa na Rais wa Marekani aliye madarakani ni tukio kubwa. Ndipo nchi humulikwa ikaonekana na kusikika kila pembe ya dunia.

Hata hivyo ni fursa kwa nchi inayotembelewa na Rais wa Marekani kujimulika yenyewe pia. Kwetu kama nchi, ujio wa Obama unaacha tafsiri nyingi.

Sijapata kuona nchi yetu ikimpokea Rais wa taifa la kigeni kwa staili ya alivyopokewa Obama. Bila shaka, hamasa ile kubwa juu ya ujio wa Obama inatokana na ukweli pia, kuwa kwa wengi, wanamwona Rais wa Marekani wa sasa, Barack Obama kama ’ Ni mmoja miongoni mwetu’. Ni kutokana na historia yake hususan asili ya baba yake. Kwamba baba wa Obama ametoka Kenya. Hivyo basi, kwa wengi, Obama angeweza pia kuwa na asili ya Tanzania.
Hata hivyo, kubwa zaidi, katika hili la ujio wa Obama ni kujiuliza; Tunajifunza nini?

Angalia sasa tofauti hii kubwa kati ya Marekani na Tanzania; ni ukweli, kuwa katika saa 20 na zaidi Rais Obama alipokuwa katika ardhi ya Tanzania, binafsi sikupata sikusikia mahali popote Obama akitamka jina la chama chake cha ‘Democrat’. Obama ametamka ‘ AMERIKA!’ mara zisizohesabika.

Ama kwa hakika ujio wa Obama umetusaidia Watanzania kupumzika na kelele za vyama, maana kwa siku kadhaa, kabla na wakati wa ujio wa Obama, Watanzania tumepata kupumzika na kusikia habari za vyama vya siasa na malumbano yasiyo na hoja za msingi, mara nyingi yasiyo na tija kwa nchi na maendeleo yake. Hakika, siasa ni kitu kizuri sana kwa nchi. Lakini siasa za ‘ ovyo ovyo’ ni kitu kibaya kwa nchi. Na mara nyingi, siasa za ‘ ovyo ovyo’ ni kitu cha hatari kwa nchi na mustakabali wake. Tuliona magazetini, picha ya Obama akiwa na Rais Mstaafu wa Marekani, George Bush wakiwa wamesimama pamoja kwenye kumbukumbu ya waathirika wa tukio la ugaidi kwenye Balozi zao za Dar es Salaam na Nairobi mwaka 1998. Picha ile ilikuwa na mengi ya kutufundisha; kuwa siasa siyo uhasama. Uchaguzi ukiisha watu mnarudi kwenye kufanya kazi. Kupigania maslahi ya taifa. Kufanya siasa za kistaarabu na siyo kuendeleza migogoro ya kisiasa na hata kuwepo kwa vurugu. Hayo hayana tija kwa nchi.

Unapomwangalia Obama na Bush kwenye picha ya pamoja wakiwa Dar na kwenye kutoa heshima kwa wahanga wa ugaidi kwenye mlipuko ulitokea kwenye Ubalozi wao mwaka 1998, inadhihirisha ukomavu wa kisiasa.

Unachotumainia hapa, kuwa ifike siku, hata hapa kwetu Tanzania kwa Rais aliye madarakani na Rais Mstaafu kutoka vyama viwili tofauti, tuone picha yao wakiwa wamesimama pamoja kwenye makaburi ya kumbukumbu ya mashujaa wetu wa Vita Vya Kagera kule Uganda.

Ndio, picha ya Obama na Bush wakiwa pamoja ni somo kwetu. Hawa wawili Bush na Obama, ndiyo tuliowaona kwenye kampeni zao wakipambana kiasi huwezi kufikiri wanaweza kusimama pamoja kama ndugu wa taifa moja. Maana, Obama kimsingi alipewa nafasi ya kuingia Ikulu kwa kuzipondaponda sera za Bush. Na aliwaambia Wamarekani, kuwa mpizani wake, John McCain alikuwa ni fotokopi ya George Bush!

Lakini kwa wenzetu Marekani, siasa siyo uhasama wala mambo ya kuwindana. Wanachogombania kwenye siasa ni kupewa heshima ya kuitumikia Marekani. Heshima hiyo akipata mpinzani wako, basi kwa wenzetu wanachofanya ni kuungana mkono kwenye kazi ya maslahi ya Marekani bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Na ndicho tunachofundishwa kwenye picha hiyo.

Alipokuwa Tanzania, Obama alitamka pale Ikulu Dar es Salaam; ” Waafrika waijenge Afrika yao, kwa ajili ya Afrika!” . Ni dhana njema, lakini, unafanyaje pale Waafrika wenyewe wanagombania fito katika kuijenga Afrika yao?

Naam, Afrika wajenzi walio juu kwenye paa wanapokea fito kwa kuangalia imeletwa na nani. Inahusu ubaguzi wa kisiasa. Hapa ndipo pia ilipo changamoto kubwa ya maendeleo ya bara hili.

Kwa nchi yetu, ili tupige hatua za maana za maendeleo, Watanzania na hususan viongozi, waifanye sasa kazi ya kuondokana na ubaguzi wa kisiasa katika nchi yetu. Ubaguzi huu wa mathalan, ’ Hawa ni wenzetu’ na ’ Wale ni maadui zetu’ umejengeka katika misingi ya kulindana katika maovu. Wenye kuendekeza ubaguzi huu ndiyo wenye kudhihirisha kile Rais Kikwete mwenyewe alipata kukitamka mwaka 2005- kugombania fito wakati tunajenga nyumba moja.

Nimepata kuandika kuwa kiongozi anapaswa kuwa na maono ya anakotaka kuipeleka nchi. Kiongozi wa nchi ataangalia sana juu ya uchumi wa nchi. Kinachofuatia ni kwa kiongozi kuitumia siasa kama nyenzo katika kutimiza maono na malengo ya kiuchumi kwa nchi.
Swali linabaki, Watanzania tuko tayari kubadilika kifikra kwa maslahi ya taifa letu? Nahitimisha.
source:mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment