WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 8, 2014

Kificho: Warioba alinilisha maneno



Wakati bado msimamo wa Wajumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Ukawa ukiwa haufahamiki kama watarejea bungeni kuendelea na vikao hivyo mwezi Agosti au la, mjadala wa katiba mpya umechukua sura mpya, baada ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, kuungana na viongozi wa CCM kukibeza kikundi hicho.

Kwa kauli hiyo, Spika Kificho anaungana na Mawaziri wa SMZ katika kubeza uamuzi huo wa Ukawa, ingawa yeye akaenda mbali zaidi na kumtupia lawama Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akieleza kuwa alimlisha maneno.
Kificho kwa mara ya kwanza amechomoza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Uwanja wa Kwamabata eneo la Magogoni na kusema hakukuwa na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kupendekeza Serikali tatu. Akasema dai hilo lilichomekwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyokusanya maoni ya watu kuhusu katiba.
Kificho amewaeleza wananchi kuwa yeye amezaliwa ndani ya Afro Shiraz (ASP), akalelelewa na kukulia CCM, hivyo hathubutu, hatathubu na hakuthubutu kusaini waraka wa kutaka mamlaka huru ya Dola ya Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mara nyingine Kificho anaonekana kusafisha upepo mchafu uliokuwa ukivuma na kutaka kumpeperusha ndani ya chama chake huku baadhi ya wanachama na viongozi wenzake, wakimtaja kama mtu aliyeshiriki kutaka kuwasaliti na kuwazunguuka mbuyu.
Madai ya awali ya viongozi wenzake akiwemo Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar upande wa CCM Salmin Awadh Salmin, yanamtupia lawama Kificho na kumpasha hakukuwa na kikao chochote kilichoketi na kupitisha azimio la BLW kutaka Serikali tatu au mamlaka kamili ya Zanzibar nje Muungano uliopo.
Mvutano huo ulioibuka nje ya Bunge la Katiba, huenda ndiyo ulioambukiza mipasho, piga nikupige ya maneno na kutupiana vijembe vikali kati ya wabunge wa Bunge la Katiba wa CCM na CUF kabla ya kundi la Ukawa halijaamua kuliacha bunge na kusema wamechoshwa na matusi, kejeli na ubaguzi.
Kificho akihutubia mkutano wa hadhara, akasema amekuwa Mwakilishi wa CCM Jimbo la Makunduchi kwa miaka saba, akawa spika miaka 19, akijinasibu kuwa ni spika mzoefu baada ya Chifu Adam Sapi Mkwawa, kufika kwake alipo sasa kumetokana na nguvu za CCM, hivyo hana jeuri ya kusaliti sera za chama chake.
Akizungumza kwa kujiamni na kujiosha, akamtupia shutuma Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba akisema kuwa ndiye aliyemwandalia fitina hiyo.
Hata hivyo, waraka ulioandikwa na kusainiwa na Spika Kificho umeandikwa na kutaja bayana kuwa Azimio la BLW Zanzibar ni kuhitaji mamlaka huru ya Dola, jambo ambalo limechukuliwa na wengi kama linalohitaji serikali yenye mamlaka kamili Zanzibar.
Kificho anasema kilichomo kwenye waraka huo ni hitaji la kufanyika marekebisho na mageuzi makubwa ya msingi ili kuipa Zanzibar nyenzo za kujijenga kiuchumi na kujitegemea ijiendeshe kwa kusimamia mambo yasiokuwa ya Muuungano kwa uwazi na si kupigania mamlaka huru ya Dola .
Pia ameeleza kuwa katika moja ya waraka huo kulikuwa na kosa la kitaalamu katika uandikaji na tafsri ya kila anayeusoma kutoa fasiri aitakayo, lakini si kusudio la BLW au lake kutaka mamlaka huru ya Dola.
Imeelezwa kuwa wawakilishi watano ndiyo waliojadili na kutia saini zao kwenye waraka huo na Kamati ya Kudumu ya Uongozi ya BLW ikakwepwa.
Wajumbe hao ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Abuboubakary Khamis (Mgogoni) ,Spika Kificho, Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), Katibu wa BLW Zanzibar Yahya Khamis Hamad na Mgeni Hassan Juma (Viti Maalum).
Hata hivyo Mwakilishi Hamza Hassan Juma (Kwamtipura) Makame Mshimba Mbarouk (Kitope )Asha Bakari Makame( Viti maalum), Mwakilishi Mohamed Raza (Uzini), aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki (amefukuzwa CCM) Mansour Yussuf Himid, Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee ni kati ya vigogo wa CCM waliosimama kidete kukosoa masuala kadhaa ndani ya Muungano kabla ya Bunge la Katiba kuanza na Ukawa kuzaliwa.
Katika semina iliyoitishwa na Baraza la Wawakilishi, wajumbe hao kwa kiasi kikubwa walisimama na kueleza kuwa kimsingi hawakuridhika na waraka huo.
Hayo na mengine wakati yakijiri na kupita katika siasa za Zanzibar, Msemaji wa CUF Salum Abdallah Bimani, ameeleza kuwa haikuwa mwafaka kwa Spika Kificho kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa na kuzungumzia msimamo wa BLW na kumtupia lawama Jaji Warioba.
Bimana anasema kama ataendelea kupanda majukwani na kukanusha msimamo wa BLW, hawatasita kumrushia paka wa kisasa na kuweka kila kitu hadharani ikiwa ni pamoja na kuanika waraka wake aliousaini kwa niaba ya taasisi anayoiongoza.
Analitaja Baraza ni moja kati ya mihimili mitatu inayounda Serikali hivyo hakupaswa kiongozi wa mhimili kusimama na kutoa msimamo wa kitaasisi na kusema hatua hiyo inaweza kutafsiariwa ni ukiukaji wa taratibu za kidsemokrasia na uvunjaji wa mipaka yake.
Hata hivyo wakati tuhuma hiyo wa Bimani ikoinekana kumponda na kumbeza Spika Kificho kwa madai hayo ya taasisi anayoiongoza ni kinyume na miiko ya demokrasia na mgawanyo wa madaraka, Naibnu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka, amemtaka Bimani kwaanza aondoe boriti kwenye jicho lake ndipo atoa kibanzi kwenye jicho la mwenzake.
Shaka anasema ingefaa sana kama Bimani angekuwa jasiri wa kumnyamazisha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ana dhamana ya taasisi ya serikali lakini akituimia kofia ya kisiasa kama Katibu Mkuu akizungumzia masuala ya kisiasa na kuafiki msimamo wa Ukawa.
Vyovyote itakavyokuwa, kimsingi na kiuhalisia kuna umuhimu pande mbili za kisiasa kati ya wabunge wa bunge la katiba chama tawala na kundi la Ukawa kukaa kitako , kutafakari, kuafikiana na kuridhiana ili Taifa lipate katiba mpya mwakani.
SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment