WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, June 16, 2014

AWAMU YA PILI YA MAJADILIANO YA KATIBA MPYA TANZANIA- WAJUMBE WEKENI UBINAFSI WENU PEMBENI





  • ILETEENI TAIFA KATIBA MPYA


  • MSIPOFANYA HIVYO DHAMBI HII ITAWATAFUNA MPAKA MNAINGIA KABURINI;

 

LAKINI: BADO TUNAHITAJI BUSARA ZAIDI KUTOKA KWA WAJUMBE HASA WALE WANAOTOKANA NA VYAMA;

  • Tukumbuke kuwa “Siasa si mchezo mchafu, ila wachezaji wake ndiyo wachafu.”


  • Je wajumbe wa bunge la katiba wanapofanya maaumuzi kuhusu katiba mpya wanaangalia, dhana  ya “wao” na “sisi”



  • Ni kweli kuwa  Siasa hutafasiriwa kuwa ni fikra, busara na mipango ya kuendesha nchi au ya kujinufaisha wao wenyewe?


  • Litakuwa ni jambo la kuheshimiwa ka viongozi wetu kama Waheshimiwa wajumbe wa bunge la katiba  watakuwa wakweli na wenye Uzalendo wa kweli ndani ya mioyo kwa faida ya wananchi wao.


  • Confucius aliwahi sema kuwa  ‘Utajiri na vyeo ndivyo vitu ambavyo kila bianadamu anavitamani; lakini ikiwa njia ya kuvipata ni kwa kwenda kinyume na misingi yake, anapaswa ajiepushe navyo.



  • Rudolph Giuliani aliwahi sema kuwa ‘Kiongozi huchaguliwa kwa kuwa yeyote anayemuweka pale huwa anaamini maamuzi, tabia na uwezo wa maarifa yake – siyo ujuzi wa kufuata maoni. Ni wajibu wa kiongozi kuchukua hatua kufuatana na sifa hizo.’



  • “kiongozi ajiulize ni vipi atalitumikia Taifa na si Taifa kumtumikia yeye Kiongozi Umashuhuri na uzuri wa Kiongozi unatokana na hekima, busara, uchapakazi, ufanisi, ufuatiliaji, uimara, uungwana, uwajibikaji na unyenyekevu wake. Ama fikra endelevu na upeo wa kuongoza ni muhimu na si kauli tamu za kuwafurahisha viongozi wengine”


 
  • Tamaa ya kujilimbikizia mali huo ni udhaifu wa mwanadamu ambao hapaswi kuupa nafasi iwapo unazingatia uadilifu wa uongozi kama wajumbe wetu hizo ndizo fikra zao hawatufai hao.



Demokrasia kama falsafa ya Plato ambayo inahusiana na uendeshaji wa shughuli za kisiasa inalenga zaidi katika  utumishi kwa umma na uendeshaji wa jamii na taifa. Wananchi wote hawawezi ongoza nchi kwa mara moja; Katika msingi huu wananchi kutokana na wingi wao waliridhika itakuwa sio rahisi kwa wao wote kukutana, kufanya maamuzi na kuyasimamia moja kwa moja maamuzi hayo yanayowahusu wao kama jamii; dhana ya kuwachagua viongozi wachache huzaliwa kwa chimbuko hili na kuruhusiwa kuunda serikali. Ambayo huendesha kulingana na katiba ya nchi ambayo imetokana na wananchi.


Tatizo kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi. Kwani inatupasa kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu. Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana, kwamba waongozi watatekeleza dhamana  na wajibu  wao kwa makubaliano na maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na maadili fulani yanayoitambulisha na kuiongoza jamii husika. 


Kwa kauli zinazotofautiana na misimamo inayotofautiana kuhusu ukamilishaji wa uandikaji wa katiba mpya kufuatia mgomgano wa mawazo na itikadi; zoezi la uandikaji wa katiba mpya unaishia kwenye  fursa na ushawishi kwa malengo ya chama au itikadi Fulani ndio iwe kinara wa katiba mpya. ikumbukwe kuwa kiongozi muadilifu hakubali kufuata  au kutoa maamuzi bila kufanya ukadirifu wa hoja na hali husika.


Uongozi ni kujitolea na kuweka matwakwa na maslahi ya wengine kuwa mstari wa mbele na si matakwa binafsi na kujinufaisha. Marehemu John Kennedy rais wa Marekani alitoa kauli moja maarufu iliyosema kuwa. Tuchague viongozi si kwa kuangalia vyama au sura, bali tuangalie uwezo wao wa kuongoza, kuhamasisha na kufanya kazi. Tupime kauli zao na matokeo ya kazi zao kama wanavyojinadi.


Serikali ni watu, inaundwa na watu tuliowachagua na tunawapa watu hawa na Serikali mamlaka makubwa ya kutuongoza, kupanga na kulinda Taifa na Katiba yetu. Dhamana hii imefanywa kwa kuaminiana kuwa Serikali itafanya kazi kwa manufaa ya Wananchi wake na kwa matakwa na utashi wa Wananchi wake.


  • Kuna amani gani na utulivu gani katika nchi yetu wakati mioyo yetu sisi kama wananchi imevimba kwa kujaa hasira za ubinafsi wa hoja na matusi ya wajumbe waliopewa dhamana ya kutuwakilisha?


Uadilifu wa wajumbe wa bunge la katiba umeporwa na wachache kwa manufaa binafsi nap engine kujiwekea matumaini makubwa ya utajiri kwa baadae. Je mijadala ya hivi sasa kuhusu katiba mpya nje ya bunge yataimarisha hoja za ufanisi wa katiba mpya au kuleta zaidi mgawanyo? Je kuhusu amani yetu?


Kama ilivyo kwa umoja wa kitaifa, kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye magomvi na hasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi


Uadilifu wa uongozi unadai kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara misingi ya kidemokrasia.


Bado binadamu si mkamilifu na kwa vyovyote vile hufikia mahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa kuyakubali na kuliomba radhi Taifa. Hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha uadilifu wa uongozi katika siasa. Kukubali kubeba dhamana kwa madhara yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako.

Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila hatua anayochukua.


Je kama baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba watasusia kikao ambacho kinatarajia kuanza mwezi wa Nane je watakuwa wame  kurupuka katika kufanya maamuzi hayo bila kuyafanyia kazi vizuri na kukiuka msingi mkubwa sana wa demokrasia? Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni kukubali kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja katika hoja na maridhiano.


Wajumbe wa bunge la katika 2014 mnapaswa kujitafakari wenyewe na kuona mzigo mzito ambao uko mbele yenu leo hii kwa faida ya Taifa na sio kundeleza matusi, vijembe, ubabe shindaneni kwa hoja na hatimaye mkubaliane kwa maridhiano.


Wananchi tunasubiri kilicho bora bila kuathiri amani na umoja wetu wa kitaifa.



MUNGU IBARIKI TANZANIA

No comments:

Post a Comment