WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 29, 2014

Karibu tena Maximo kama unaijua Yanga

Maoni ya katuni

Kocha wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo ambaye aliigawa nchi katika siku zake za mwishoni madarakani baadhi wakimuona kikwazo cha maendeleo na wengine wakidhani ndiye muarubaini wa kudumaa kwa soka letu, aliwasili nchini juzi kuwafundisha mabingwa mara 23 wa Bara timu ya Yanga.

Baada ya kuiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, CHAN, 2009 lakini timu ikakosa chupuchupu kwenda fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, CHAN, za Ghana ilikuwa ni lazima pawe na kambi mbili zenye mawazo tofauti kuhusu Maximo.

Lakini ambalo halikuwa na ubishi, kimsingi, Maximo ni kocha mzuri miongoni mwa wana taaluma hiyo ikiwa nia ya mafanikio ya haraka itawekwa pembeni.

Kwa sababu Maximo ni kocha mzuri miongoni mwa wana taaluma hiyo ndiyo maana, basi, haikushangaza kuona Yanga ikikamilisha jitihada za muda mrefu za kumrudisha nchini Mbrazili huyo ambaye aliondoka baada ya mkataba wake na shirikisho la soka, TFF, kutoongezwa.

Ni kuondoka kwa Maximo huko, baada ya mkataba wake kutoongezwa, ndiko ambako kumetusukuma leo, Nipashe, kuwa na wasiwasi na hatma ya taswira ya heshima aliyoacha mwalimu huyo nchini sasa anapokwenda kuwa muajiriwa wa Yanga.

Ni siri iliyo wazi kwamba Yanga haijapata kuachana na mwalimu bila migogoro ya kifedha, hata pale ambapo makocha hao waliiwezesha kupata mafanikio barani Afrika achilia mbali kwenye ligi kuu ya Bara.

Lakini ni siri iliyo wazi pia kwamba Yanga haijapata kuheshimu taaluma ya ukocha, na hasa walimu wenye wepesi wa kutetea falsafa zao ndani ya klabu hiyo.

Tumesema, Nipashe, kwamba ambalo halina ubishi, kimsingi, Maximo ni kocha mzuri miongoni mwa wana taaluma hiyo ikiwa nia ya mafanikio ya haraka itawekwa pembeni. Kwa nini?

Kwa wanaokumbuka utawala wake Taifa Stars, wanajua kuwa ni mwalimu ambaye anaamini mno katika ukuzaji wa vipaji vya chipukizi ambao wapo ndani ya mipaka ya mfumo wa eneo la soka analoliongoza.

Wengi wa wachezaji walioko Botswana ambao nchi inajivuania sasa wakati Stars ikijaribu kwenda kule ambako Maximo alishindwa kutupeleka kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980, ama waliibuliwa na kocha huyo ama walikuwa kwenye mipango yake 2009 kabla ya TFF kumgeukia Jan Poulsen na kisha Kim mwenye ubini kama huo pia.

Na wanaokumbuka utawala wake Taifa Stars, pia, wanajua kuwa ni mwalimu ambaye anaamini mno katika nidhamu ndani na nje ya uwanja kiasi kwamba yupo radhi kutofautiana hata na nusu ya taifa kama ilivyokuwa katika migogoro na Juma Kaseja, Haruna Moshi na Athumani Iddi kuliko kupindisha maadili.

Tuachane na yale yaliyo katika uwezekano wa kugongana na falsafa yake Yanga, kama kupangiwa wachezaji wa kucheza na baadhi ya viongozi ama kuingiliwa katika masuala ya udhibiti wa nidhamu dhidi ya wachezaji mastaa wenye kuchelewa kambi za mazoezi ama vipindi vya mazoezi hayo.

Je, Maximo anafahamu kwamba hakuna mwalimu, wakiwemo marehemu Tambwe Leya na marehemu Tito Mwaluvanda, ambaye hakuacha deni katika klabu hiyo ambayo haina subira linapouja suala la ubingwa wa Bara?

Kama Maximo anayajua yote hayo, ikiwemo ukweli kuwa Mbelgiji Tom Seintfeit alifukuzwa baada ya mechi tatu za kwanza za msimu na kwamba wazungu wengine si chini ya wawili wameishitaki FIFA, shirikisho la dunia, wakililia mafao yao, basi tunamkaribisha Yanga Nipashe.  

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment