Rais Jakaya Kikwete
Utangulizi
Ndugu zangu,
Watanzania Wenzangu;
Ni furaha na
faraja kubwa kuifikia siku hii adhimu ya kuuaga mwaka wa 2012 na kuukaribisha
mwaka 2013. Ni jambo la bahati ambayo hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuumaliza mwaka huu
salama. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao wangependa kuiona
siku hii lakini hawakujaaliwa. Wametangulia mbele ya haki. Tuendelee
kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema. Amin. Nasi
tumuombe Mola wetu atujaalie fanaka tele katika mwaka ujao.
Mapitio ya
Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Mwaka
tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini,
pia, ulikuwa na changamoto zake. Baadhi zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za
kusikitisha na kuhuzunisha.
Ajali za
barabarani na majini ziliendelea kupoteza maisha ya watu wengi na kusababisha
majeraha na ulemavu kwa maelfu. Ajali mbaya kuliko zote kutokea, mwaka huu,
ilikuwa ile ya meli ya MV Skagit iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012 ambapo watu 144 walipoteza
maisha. Ajali za barabarani zilizosababisha vifo nazo ziliongezeka kutoka 3,012 mwaka
2011 hadi kufikia 3,144 na kusababisha vifo vya ndugu zetu 3,714.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia
ajali ya MV Skagit ambayo ilitokea miezi 11 baada ya ile ya MV Spice Islander,
Serikali zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kuhusu masuala ya
usafiri wa majini kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa ajili hiyo
SUMATRA na Zanzibar Maritime Authority zinafanya kazi kwa karibu zaidi na
kanuni za usafirishaji wa abiria na mizigo na za usajili na ubora wa meli
zimewianishwa. Ni matumaini yetu kuwa hatua hizo zitasaidia kumaliza
ajali zinazotokana na makosa ya wanadamu.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa
ajali za barabarani tuliendelea na tutaendelea kuwahimiza madereva kuheshimu
Sheria za Usalama Barabarani, waepuke uzembe na hasa ulevi wakati wa
kuendesha. Tutaendelea kuwakumbusha wenye magari kuhakikisha kuwa uzima
wa magari yao unakuwa wa kiwango cha juu. Hali kadhalika, tumewataka
Polisi waongeze ukali na kuwabana ipasavyo madereva na wamiliki wa magari ili
watekeleze wajibu wao na wasipofanya hivyo wawajibishwe
inavyostahili.
Hali
ya Usalama
Ndugu wananchi;
Tunaumaliza
mwaka huu nchi yetu ikiwa shwari, salama na tulivu. Tuombe Mungu hali hii
iendelee mwaka 2013 na idumu milele. Mipaka ya nchi yetu ipo salama na
uhusiano na majirani na nchi zote duniani ni mzuri. Tunaendelea kutafuta
suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi yetu na Malawi katika Ziwa Nyasa kwa
njia ya mazungumzo. Suala hilo limewasilishwa kwa pamoja na Serikali zote mbili
kwa Mheshimiwa Joaquim Chissano, Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi Wastaafu wa
Afrika kwa ajili kuzisaidia nchi zetu kupata ufumbuzi. Matumaini yetu ni
kuwa viongozi hao watalishughulikia suala hili mapema iwezekanavyo.
Ushirikiano wa
Kanda
Ndugu Wananchi;
Ushirikiano wetu
wa kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC) unaendelea vizuri. Mwaka huu nchi yetu imepewa
heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Chombo cha SADC kinachoshughulikia masuala
ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Jukumu
hilo ni zito na hasa katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto za kisiasa na
kiusalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na
Zimbabwe. Nchi yetu inatarajiwa kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa migogoro
hiyo migumu. Ndiyo maana tulifanya Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi za
SADC hapa Dar es Salaam tarehe 7 na 8 Desemba, 2012. Mwaka ujao, kwa
kushirikiana na wenzetu, tutaendeleza juhudi zetu. Ni matumaini yangu
kuwa tukipata ushirikiano wa viongozi na wananchi wa nchi husika na jumuiya ya
kimataifa tutapata ufumbuzi tunaotaka.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, tumeendelea kushuhudia Jumuiya hiyo na harakati za
utangamano zikizidi kustawi. Jengo la Makao Makuu ya Jumuiya limekamilika
na kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2012. Siku hiyo hiyo kule Athi
River, Kenya, barabara ya kutoka Arusha hadi Athi River ilizinduliwa.
Barabara hii ni moja ya miradi kadhaa inayotekelezwa kwa pamoja na nchi
wanachama wa Jumuiya wa Afrika Mashariki.
Mchakato wa
utangamano wa kiuchumi wa Afrika Mashariki unaendelea kwa kasi. Tanzania
ikiwa sehemu kamili ya mchakato huo, lazima tuhakikishe kuwa tunakwenda nao
sambamba. Tusikubali kuachwa nyuma wala kuwa chanzo cha kuuchelewesha
mchakato huo bila ya sababu za msingi. Utangamano una maslahi kwa nchi
yetu na manufaa yake ni makubwa. Kwa mfano, mauzo yetu katika soka la
Afrika Mashariki yameongezeka sana kutoka dola za Kimarekani milioni 58.6 mwaka
2000 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 409 mwaka
2011.
Jumuiya
imekuwa kichocheo muhimu cha kukuza uzalishaji, ajira na uchumi hapa
nchini. Kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali tulizonazo tuna matumaini
makubwa ya kunufaika zaidi siku za usoni. Naweza kuthubutu hata kusema
kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi kuliko nchi nyingine wanachama wa Jumuiya
hiyo. Kinachotakiwa ni sisi kujipanga vizuri kwa sera na mipango ili
tuzitumie fursa tulizonazo kwa maslahi ya uchumi na maendeleo ya nchi yetu na
watu wake. Tuache woga, tujiamini.
Matishio ya
Usalama
Ndugu Wananchi;
Licha ya
kumaliza mwaka nchi ikiwa shwari na yenye amani na utulivu, yalikuwepo matukio
yaliyotishia usalama wetu. Bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa matukio
hayo yalisababishwa na baadhi ya viongozi wa dini na siasa na wafuasi
wao. Kwa kweli kwa mara ya kwanza nchi yetu ilifikishwa kwenye hatari ya
kutokea mgawanyiko mkubwa wa Watanzania au hata mapigano ya raia kwa misingi ya
dini zao. Bahati nzuri hilo halikutokea na Mungu aliepushe lisitokee
kamwe.
Nimeshalisemea
jambo hili siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwasihi Watanzania
wenzangu kupima athari za kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii
yetu, nchi yetu na watu wake. Viongozi wa dini, waumini na viongozi wa
siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalum wa kuhakikisha kuwa Watanzania
wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini
zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako. Hiyo ndiyo sifa ya nchi
yetu tunayoijua sote ambayo ni njema na watu wengi wanataka kuja kujifunza
kwetu na wale wenye shida wanatamani wawe kama sisi. Hii ni tunu muhimu
ya taifa ambayo tusikubali kuipoteza kwa maslahi binafsi ya watu wachache.
Ndugu Wananchi;
Wakati wo wote,
lazima tutambue umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimiana kwa tofauti zetu za
kidini, rangi, kabila, tutokako na ufuasi wa vyama vya siasa. Lazima pia
tuhakikishe kuwa tunaheshimu sheria na taratibu zinazotawala mikutano na
maandamano. Tukiyazingatia hayo nchi yetu itakuwa haina tishio lo lote
kwa amani na usalama wake. Yasipozingatiwa tunaiweka nchi yetu
hatarini. Sisi katika Serikali tutakuwa hatuna la kufanya bali kutimiza
wajibu wetu wa kulinda usalama wa raia na nchi yetu. Wahusika
watachukuliwa hatua na vyombo vya usalama na kisheria kwa mujibu wa sheria za
nchi. Tulifanya hivyo mwaka huu na hatutakuwa na ajizi kufanya hivyo siku
yo yote kama hapana budi.
Uhalifu
Unapungua
Ndugu Wananchi;
Inatia
moyo kuona kuwa mwaka huu makosa ya jinai yalipungua na kufikia 66,255 yakilinganishwa
na makosa 69,678 ya mwaka jana au94,390 ya mwaka
juzi. Hii inathibitisha kuimarika kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la
Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya usalama. Pamoja
na hayo lazima tuongeze juhudi za kupambana na uhalifu kwani bado matukio ni
mengi mno na upungufu bado ni mdogo. Tutaendeleza kazi tuifanyayo sasa ya
kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu, zana na vitendea kazi husika.
Uhalifu wa
Kimtandao
Ndugu Wananchi;
Tutaongeza nguvu
katika kupambana na uhalifu unaoendeshwa na mitandao ya uhalifu ndani na nje ya
nchi. Mitandao hiyo hasa imekuwa inajihusisha na biashara ya kusafirisha
wanadamu, biashara ya dawa za kulevya na biashara ya nyara za
Serikali.
Mapambano dhidi
ya uhalifu wa kimtandao yametuwezesha kukamata wahamiaji haramu 4,765 na
tayari 1,611 wamerudishwa kwao. Kwa upande wa dawa za
kulevya watuhumiwa 6,929 walikamatwa mwaka huu ukilinganisha
na 209 mwaka 2011. Kilo 55,285 za dawa za
kulevya zilikamatwa mwaka huu ukilinganisha na kilo 17,752.4 mwaka
jana. Kwa upande wa nyara za Serikali, zilizokamatwa ni 1,416 na kati
ya hizo 736 ni meno ya tembo. Watuhumiwa 1,037 walikamatwa
na kesi 746 zipo Mahakamani katika hatua
mbalimbali.
Ndugu Wananchi;
Taarifa hizi
zinathibitisha kuimarika kwa jitihada za kupambana na uhalifu wa
kimtandao. Tutaimarisha zaidi jitihada zetu mwaka 2013 ili tupate
mafanikio zaidi. Tutaviongezea uwezo wa rasilimali watu, zana, vifaa na fedha
za uendeshaji vyombo vyetu vya usalama vinavyoongoza mapambano haya.
Tutaimarisha na
kuendeleza ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi jirani na nyinginezo
duniani. Hii itasaidia kutuongezea uwezo wa kupambana na mitandao ya
uhalifu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa. Pia tutazipitia upya sheria
za kupambana na makosa haya kwa nia ya kuziboresha.
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka
2013, tutapanua na kuimarisha huduma ya matibabu kwa watu walioathirika na dawa
za kulevya kote nchini. Tutakamilisha ujenzi wa kituo cha Dodoma na
kujenga kingine kipya Dar es Salaam. Natoa wito kwa wale wote
walioathirika au watu wenye watoto au rafiki au jamaa walioathirika waende
hospitali kupatiwa matibabu kwani matibabu hayo ni bure.
Hali ya Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka
2012, tunaoumaliza leo, uchumi wa nchi yetu uliendelea kukua na kuimarika licha
ya kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa umeme, kupanda kwa bei za mafuta na
chakula duniani na uhaba wa mvua katika maeneo mengi nchini uliosababisha
kupungua kwa uzalishaji na kupanda kwa bei za vyakula nchini. Pia, licha
ya kuendelea kwa msukosuko wa uchumi wa dunia na hasa katika Bara la Ulaya
ambako ni soko kuu la bidhaa zetu na watalii. Mategemeo yetu ni kuwa,
mwaka huu, uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.8 na mwakani
(2013) utakua kwa asilimia 7.0ukilinganisha na asilimia 6.4 mwaka
2011.
Kwa jumla,
ukilinganisha na makadirio ya IMF ya kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia
3.3 mwaka huu, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri na
kuifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi kubwa.
Hali hii ya
uchumi wetu ina maana kubwa mbili.Kwanza,kwamba uchumi wetu umejenga uhimilivu
dhidi ya misukosuko ya uchumi wa dunia. Na pili, kwamba shughuli za
uzalishaji na huduma zinazidi kukua na mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi
yameongezeka. Kuongezeka kwa mauzo ya nje kumefanya akiba yetu ya fedha
za kigeni kufikia dola za Marekani bilioni 3.9 mwezi Novemba,
2012 kiasi ambacho kinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi minne.
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya
mapato ya Serikali yatokanayo na kodi yalifikia shilingi bilioni 580.3 mwezi
Oktoba, 2012 ikilinganishwa na shilingi bilioni 479.3 mwezi
Oktoba 2011. Matarajio yetu ni kufanya vizuri zaidi mwaka 2013 kwa mapato
yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi ambayo bado ni chini ya
lengo.
Ndugu Wananchi;
Mfumuko wa bei
kuwa juu ni changamoto ambayo tunaendelea kuikabili ili kuleta utulivu
uliokamilifu kwa uchumi wetu na kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa
Tanzania. Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti hali hiyo na
mafanikio ya kututia moyo yameanza kuonekana. Kwa mfano, mfumuko wa bei
umepungua kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia
12.1 mwezi Novemba, 2012. Kiwango hicho bado ni cha juu na
hakikubaliki. Tutaendelea kuchukua hatua zaidi ili tuweze kufikia lengo
letu la mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 10 ifikapo mwezi
Juni, 2013.
Miongoni mwa
mambo tuliyopanga kufanya ili kupunguza mfumuko wa bei ni kuimarisha hali ya
upatikanaji wa umeme na kudhibiti mwenendo wa bei ya mafuta. Kufanya
hivyo kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na uchukuzi wa bidhaa. Aidha,
tutaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kukuza na kuboresha kilimo nchini
kwa lengo la kujihakikishia usalama wa chakula, kukuza pato la taifa na
kupunguza umaskini hasa miongoni mwa wakulima
Utekelezaji wa
Miradi ya Maendeleo
Ndugu wananchi;
Mwaka huu
tunaoumaliza leo ulikuwa na mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa utekelezaji
wa miradi ya kuendeleza miundombinu nchini. Tumeshuhudia miradi ya
barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, bandari, umeme na maji
ikikamilika, au kuanzwa au utekelezaji wake ukiwa unaendelea. Hakika
lengo la kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa barabara za lami siyo
ndoto tena bali ni jambo la uhakika na litatimia muda si mrefu
ujao.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa reli,
mwaka huu tumeendelea kukarabati reli ya kati na kurejesha usafiri wa treni
kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma. Mwaka ujao (2013)
tutaendeleza kazi ya ukarabati wa reli hiyo muhimu na kuzidi kuboresha
huduma. Tumekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mpanda na Songwe na
tunaendelea kuboresha viwanja vya Tabora, Kigoma, Bukoba, Mafia, Mwanza na
Zanzibar. Tumeendelea kujenga na kupanua miundombinu ya maji nchini na
kuboresha upatikanaji wa maji salama kwa Watanzania. Kwa mwaka huu usambazaji
wa maji salama umefikia asilimia 87 kwa watu wa mijini na asilimia
61.5 vijijini. Tutaendeleza kazi hiyo mwaka 2013.
Msongamano wa
Magari Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Katika Jiji la
Dar es Salaam tumeendelea na tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza
msongamano wa magari unaozidi kuongezeka. Barabara mpya zimejengwa na
zinaendelea kujengwa ndani na kuzunguka Jiji. Barabara kadhaa
zimepanuliwa na nyingine zitaendelea kupanuliwa. Ujenzi wa miundombinu
(barabara na vituo) ya mabasi yaendayo haraka umeanza. Mwaka 2013 ujenzi
wa barabara za juu ya nyingine katika makutano ya TAZARA utaanza na matayarisho
ya kufanya hivyo kwa makutano ya Ubungo yatakamilishwa.
Tumetimiza
ahadi yetu ya kutumia treni kusafirisha abiria katika jiji la Dar es
Salaam. Usafirishaji umeanza na unaendelea kati ya Stesheni na Ubungo na
kutoka Stesheni ya TAZARA hadi Pugu – Mwakanga. Mwaka ujao tutaendelea
kuimarisha usafiri huo kwa kuongeza treni na idadi ya safari. Tayari
Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu na kushauri kuhusu
kupanua huduma hiyo mpaka ifike Tegeta, Bunju, Kimara, Luguruni, Kibaha,
Mbagala-Rangi Tatu na Kongowe. Ushauri huo pia utahusu kuwa na huduma
bora ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya aina ya
njia, vichwa vya treni na mabehewa. Tuliamua kuanza na reli na treni
iliyopo, lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa
treni mijini.
Umeme
Ndugu Wananchi;
Mwaka
tunaoumaliza leo haukuwa rahisi kwa upande wa upatikanaji wa umeme.
Mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi, Mtera, Pangani na Nyumba ya
Mungu yameendelea kutokuwa na maji ya kutosha kwa sababu ya uhaba wa
mvua. Hivyo basi taifa limelazimika kutegemea umeme wa kukodi
unaozalishwa kwa kutumia mafuta. Umeme huo umekuwa wa gharama kubwa na
hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa TANESCO na taifa. Serikali imeendelea kushirikiana
na TANESCO na kuisaidia kubeba mzigo huo. Tutaendelea kufanya hivyo mwaka
ujao na mpaka tutakapofikia hatua ya kutokuwa na ulazima wa kutumia umeme wa
kukodi.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa
tulipopata tatizo la ukame na upungufu wa umeme mwaka 2006/2007, Serikali yetu
iliazimia kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine vikiwemo
gesi asili, makaa ya mawe, upepo na jua. Nafurahi kusema kuwa, tangu
wakati ule Serikali imeiwezesha TANESCO kujenga vituo vitatu vinavyozalisha MW
245 kwa kutumia gesi.
Hatukuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi kwa sababu ya
kiasi cha gesi kinacholetwa Dar es Salaam kutoka Songo Songo kuwa kidogo.
Ndiyo maana tukaamua kujenga bomba jipya kubwa la kusafirisha gesi kutoka Songo
Songo hadi Dar es Salaam.
Ndugu Wananchi;
Kwa nia ya kutaka
kuhakikisha kuwa kutakuwa na gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi pale
inapohitajika, ikaamuliwa bomba hilo liendelezwe mpaka visima vya gesi vya
Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo umeanza mwezi Novemba, 2012 na unatarajiwa
kukamilika ndani ya miezi 18. Gesi itakayopatikana ina uwezo wa kuzalisha MW
3,000 za umeme. Tayari mipango inaendelea ya kujenga
mitambo ya kuzalisha MW 900 pale Kinyerezi ili mara gesi
itakapofika umeme uzalishwe. Hatua hiyo itatuwezesha kuung’oa mzizi wa
fitina wa mgao wa umeme na mzigo wa kununua umeme ulio ghali.
Utafutaji wa
Gesi
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka
2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara,
Lindi na Pwani. Utafutaji bado unaendelea na tuna matumaini kuwa gesi nyingi
zaidi huenda ikagundulika. Hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria
mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu. Nia yetu ni kutaka
kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu
na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji.
Napenda kutumia
nafasi hii kuwahakikishia ndugu zetu wa kule gesi ilipogunduliwa au popote
itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika.
Rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika na Serikali inajiandaa hivyo.
Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano, wanajua maelekezo niliyotoa
kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea uchumi wa gesi.
Lakini, sharti
la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao
halikubaliki. Rasilimali inayopatikana po pote katika nchi hii ni mali ya taifa
zima na hutumika kwa manufaa ya taifa. Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika
au pale shughuli hizo zinapofanyika. Jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo
sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika
kuhudumia watu wote po pote walipo.
Ndugu Wananchi;
Huu ni
msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo jema la tunu, tulilorithi
kwa waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi na kulidumisha.
Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye mambo mabaya wananchi tunaodai
kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa agenda zinazopandikiza chuki kwa watu na
kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu mkubwa wa uongozi na uzalendo.
Tuache siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka. Nawaomba
wananchi msiwasikilize, si watu wanaowatakia mema na wala hawaitakii mema nchi
yetu.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio katika utekelezaji wa sera yetu ya kupanua fursa ya elimu
kwa Watanzania katika ngazi zote. Mwaka huu vijana wetu wengi zaidi
walijiunga na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu. Hivi
sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi katika kuongeza ubora wa elimu.
Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi za kupanua mafunzo na ajira za
walimu wa shule za msingi na sekondari. Kwa mfano, mwaka huu walimu 24,621 wapya
waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule za msingi na 13,242 wa
shule za sekondari. Januari, 2013 tunategemea kuajiri walimu 28,746 kati
yao 14,606 wa shule za msingi na 14,060 watakuwa
wa shule za sekondari.
Kwa sababu
hiyo, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi umeendelea kuwa mzuri. Hivi sasa
kwa shule za msingi uwiano umefikia 1:46ukilinganisha na 1:56 mwaka
2005. Uwiano unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa sekondari
uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29ukilinganisha na 1:20 unaostahili.
Kutokana na upanuzi wa vyuo vya kufundisha walimu nchini, bila ya shaka baada
ya miaka mitatu hivi upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari
haitakuwa kilio tena.
Ndugu Wananchi;
Upatikanaji wa
vitabu nao unazidi kuwa bora. Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa
mwanafunzi ni 1:3 kwa shule ya msingi na sekondari 1:3ukilinganisha
na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4 mwaka
2009. Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya
elimu ili kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vingine vya kusomea na
kufundishia. Tunataka katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1.
Kwa upande wa
maabara za sayansi, tarehe 4 Novemba, 2012, nilipokuwa kwenye ziara ya Mkoa wa
Singida, nilitoa agizo la kutaka ndani ya miaka miwili, kuanzia mwaka 2013,
kila shule ya sekondari ya kata nchini iwe na majengo ya maabara
yaliyokamilika. Yawe pia yanatumika kwa maana ya vifaa na mahitaji
muhimu. Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa agizo hili
linatekelezwa kwa ukamilifu. Kuanzia sasa, katika ziara zitakazofanywa
Mikoani na mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tutapenda kupata taarifa ya
maendeleo ya utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa
ufundishaji imedhihirika kwamba mkakati maalum unahitajika kuboresha
ufundishaji wa masomo ya hisabati, kiingereza na sayansi katika shule za msingi
na sekondari. Matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne kwa
miaka mingi sasa yanathibitisha haja hii. Sasa wakati umefika kwa suala
hili kulipa uzito unaostahili. Tutafanya hivyo kuanzia mwaka 2013.
Afya
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2012
ulikuwa na mafanikio mengi ya kutia moyo kwa upande wa sekta ya afya nchini
pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali. Kazi ya kusogeza huduma ya afya
karibu na wanapoishi watu kwa maana ya kujenga zahanati, vituo vya afya,
hospitali mpya na kuimarisha zilizopo iliendelea kutekelezwa kwa mafanikio kote
nchini.
Hali kadhalika,
uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba ya magonjwa makubwa umezidi kuimarika
mwaka huu. Upatikanaji wa dawa, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba umeendelea
kuboreshwa. Aidha, mafunzo na ajira za madaktari, wauguzi na wataalamu
wengine wa afya vimeendelea kuongezwa. Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Moyo
kimekamilika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwaka ujao (2013)
shughuli za upasuaji na nyinginezo husika kutibu maradhi ya moyo zitakuwa
zimeboreshwa sana. Upanuzi mkubwa wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road
umekamilika.
Kwa ajili hiyo,
huduma zitakuwa bora zaidi na msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo utakuwa
umemalizika. Ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa katika Chuo Kikuu cha
Dodoma unaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika mwaka 2014. Hospitali
hiyo itatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari na uuguzi.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
huu pia, tumekamilisha matayarisho ya kuanza ujenzi wa hospitali kubwa na ya
kisasa kabisa kule Mlonganzila, Dar es Salaam. Ujenzi utaanza Februari
2013 na kukamilika Februari, 2015. Hospitali hii pia itakuwa ya
kufundishia wakati Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili
kitakapohamishia sehemu kubwa ya shughuli zake huko Mloganzila. Mchakato
wa ujenzi wa Chuo hicho nao unakaribia kuanza. Kuwepo kwa hospitali hizi
kutaongeza sana uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba. Sasa naweza
kuthubutu kusema kuwa safari ya kupunguza wagonjwa tunawaopeleka nje
tumeianza kwa dhati.
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya magonjwa makubwa yanayosababisha
vifo vingi kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. Maambukizi na vifo
vinazidi kupungua. Pia vifo vya kina mama na watoto vinaendelea kupungua.
Kwa mujibu wa
taarifa za mwaka huu za Shirika la Afya Duniani, vifo vya watoto wenye umri
chini ya miaka mitano hapa Tanzania vimepungua kutoka vifo 81 kwa
kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 hadi kufika vifo
65.2 mwaka 2011 na vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo
51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 na
kufikia vifo 45 mwaka 2011. Mafanikio haya yanaiweka Tanzania
katika orodha ya nchi 10 zinazofanya vizuri duniani katika
kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ndugu Wananchi;
Hatuna
budi kufahamu kuwa haya ni matokeo ya kufanya vizuri kwenye chanjo kwa watoto
ambayo imefikia wastani wa asilimia 90. Pia imechangiwa na
mafanikio yetu katika kupunguza maambukizi ya malaria na UKIMWI kwa
watoto. Naamini tutapata mafanikio makubwa zaidi kuanzia mwaka 2013
tutakapoanza chanjo dhidi ya kichomi (pneumonia) na ugonjwa wa kuharisha kwa
watoto chini ya umri wa miaka mitano. Aidha, tukiendelea kutekeleza kwa
dhati mpango wa kila mtoto kulala kwenye chandarua kilichotiwa dawa na ule Mpango
Kabambe wa Kuzuia Maambukizi ya Mama Kwenda kwa Mtoto niliouzindua kule Lindi
tarehe 1 Desemba, 2012, mambo yatakuwa vizuri zaidi.
Sensa ya Watu
na Makazi
Ndugu wananchi;
Leo asubuhi kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja nilitangaza matokea ya Sensa ya Watu na Makazi
iliyofanyika mwezi Agosti, mwaka 2012. Matokeo haya yanaonyesha kwamba
idadi ya watu nchini Tanzania ni milioni 44,929,002 kati yao
watu milioni 43,625,434 wanaishi Tanzania Bara na milioni
1,303,568 wanaishi Zanzibar. Ukilinganisha na Sensa ya mwaka
2002 tulipokuwa na watu milioni 34.4, hili ni ongezeko la watumilioni
10.5 au wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka.
Matokeo haya
yana maana kubwa kwa Serikali na kwa kila mmoja wetu. Kwa kasi hii ya
ongezeko la watu ifikapo mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni
51.6. Hii ni idadi kubwa sana ya watu inayoleta
changamoto kwa Serikali na jamii. Hatuna budi kutambua maana ya idadi
hiyo ya watu na kujipanga vyema kukidhi mahitaji yao na hasa kuhakikisha kuwa
maskini hawaongezeki na huduma zinatosheleza mahitaji na zina ubora wa
juu. Kazi hiyo lazima ianze sasa na ionekane katika Mipango ya
Maendeleo.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande
wetu, sisi wananchi, taarifa hii inamlazimu kila mmoja wetu atambue kuwa kwa
kasi hii, siku za usoni nchi yetu itakuwa na watu wengi, hivyo ushindani kwa
rasilimali utakuwa mkubwa. Watakaofanikiwa wakati huo ni wale wenye
familia ndogo au zile ambazo zimepanga uzazi. Tukipanga uzazi tunajipa
nafasi ya kutunza na kulea vizuri watoto wetu na kuwapatia mahitaji yao muhimu
ya maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia
nafasi hii kurudia kuwashukuru wananchi wenzangu wote kwa ushirikiano wenu
uliowezesha zoezi zima kufanikiwa kiasi hiki. Aidha, nawashukuru kwa
dhati viongozi, watendaji wakuu na maofisa wote waliopanga, kuratibu, kusimamia
na kutekeleza zoezi la kuhesabu watu. Natoa shukrani maalum kwa Kamati ya
Kitaifa ya Sensa, Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya, Ofisi ya Taifa ya Takwimu
ya Jamhuri ya Muungano na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar na makarani wote
wa sensa. Penye nia pana njia. Tumeweza kushinda changamoto zote na
kuwapatia Watanzania nyenzo muhimu ya kupanga mipango ya maendeleo yao.
Vitambulisho
vya Taifa
Ndugu wananchi;
Mwaka huu
tumeanza zoezi la kusajili watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa
Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013. Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya
Kilombero ambalo lilifanikiwa. Hivi sasa wanaendelea na zoezi hilo
Zanzibar. Maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa vitambulisho nchi nzima
kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri. Napenda kuwasihi wananchi wenzangu
wakati utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa watakaohusika na
kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe ipasavyo.
Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya kujisajili na kupata vitambulisho.
Mchakato wa
Katiba Mpya
Ndugu wananchi;
Mtakumbuka kuwa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba nililiyoiunda tarehe 1 Mei, 2012 ilianza kazi yake
rasmi tarehe 29 Juni, 2012 na inaendelea vyema. Mpaka sasa Tume imekamilisha
hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote
nchini. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza
kwa wingi kutoa maoni. Zoezi linalofuata ni la kukusanya maoni ya makundi
maalumu kuanzia mwezi Januari, 2013. Natoa wito kwa makundi hayo
nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua hiyo
kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari
mwezi Mei, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa
ratiba ya Tume, rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya
Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2013. Tume
itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza hayo na utaratibu
utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba wakati
huo ukiwadia.
Baada ya
kukamilika kwa Vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba
ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya
Sheria. Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.
Mwezi Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na
kupitishwa. Baada ya Bunge Maalum kupitisha Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo
itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Ndugu Wananchi;
Matarajio
yetu ni kwamba kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa nchi yetu itakuwa
na Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka
2014. Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka 50 hivyo hiyo
itakuwa zawadi ya tunu kubwa. Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo,
tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo. Inshallah,
Mwenyezi Mungu atajaalia baraka zake, nia yetu njema itatimia. Pamoja na
hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu kushiriki kwa ukamilifu katika hatua
zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka kuhusu Katiba tunayoitaka.
Marekebisho ya
Sheria
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba
yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, nilieleza kwamba katika
mazungumzo baina ya Serikali na vyama vya siasa na wadau wengine juu ya
marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulikubaliana tushughulikie
marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua. Tulikubaliana kuanza na
mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe
na ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum
na Kura ya Maoni.
Tulifanya hivyo
kuhusu Tume ya Katiba na sasa tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe
iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni. Kama mazungumzo
yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari kwa uamuzi.
Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya
Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni
itatungiwa Sheria yake maalum. Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake
yataanza mapema iwezekanavyo. Nawasihi wananchi wenzangu, viongozi wa
vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee kushirikiana katika
mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali
mwema wa nchi yetu na watu wake.
Mfumo wa
Dijitali
Ndugu wananchi;
Bila ya shaka
mtakumbuka taarifa za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Tume
ya Mawasiliano kwamba kuanzia tarehe 1 Januari, 2013 nchi yetu itahamia katika
mfumo wa mawasiliano unaotumia teknolojia ya dijitali (au kidijiti kwa tafsiri
ya BAKITA) badala ya huu wa sasa wa analojia. Uamuzi huu unakuja kufuatia
uamuzi wa kimataifa kwamba nchi zote duniani ziwe zimeingia kwenye mfumo huu
ifikapo mwaka 2015. Pia unazingatia uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa nchi zetu kuanza safari hiyo tarehe 1 Januari, 2013.
Hapa
nchini zoezi hili litafanyika kwa awamu. Litaanza katika mikoa saba ya
Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza na Tanga na mingine
itafuata kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa.
Ndugu
Wananchi;
Teknolojia
ya dijitali katika mfumo wa mawasiliano hufanya picha za televisheni kuwa nzuri
na hazina chenga chenga. Mawasiliano ya simu yatakuwa mazuri zaidi.
Vile vile, itakuwa rahisi kupata huduma za televisheni kwenye simu za mkononi
na huduma ya intaneti kwenye televisheni.
Ndugu
Wananchi;
Ili kuweza kutumia
teknolojia hii, kila televisheni inatakiwa iwe na kifaa kiitwacho
king’amuzi. Vifaa hivi vipo kwa wingi madukani na wengine tayari wanavyo.
Naomba niwatoe hofu kwamba kwa kuingia katika mfumo huu siyo lazima kununua
televisheni mpya. Televisheni yo yote yenye vitundu vitatu vya rangi za njano,
nyeupe na nyekundu itaweza kufanya kazi kwenye mfumo wa dijitali. Hata wale
ambao hawana televisheni za namna hiyo wanaweza kununua kifaa cha kuunganishia
king’amuzi na mambo yakawa mazuri.
Uhusiano wa
Kimataifa
Ndugu wananchi;
Katika mwaka
2012, uhusiano wetu na washirika wetu wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea
kuimarika. Wote wanaridhika na kusifu kazi nzuri inayofanywa na Serikali
yetu na ndiyo maana wanaendelea kushirikiana nasi na kutoa misaada ya maendeleo.
Aidha, wameonesha nia thabiti ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia
katika harakati zetu za kujiletea maendeleo.
Napenda kutumia
nafasi hii kwa niaba yenu nyote kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa
maendeleo kwa mchango mkubwa wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi
yetu. Nawahakikishia kuwa tunathamini sana ushirikiano wao na misaada yao
na tutafanya kila tuwezalo kudumisha ushirikiano baina yetu.
Mkutano wa Smart
Parntership
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu nchi
yetu ilipata bahati ya kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na
kimataifa. Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Shirika la
Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Mkutano Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Chanjo (GAVI) na Mkutano
wa Wakuu wa Nchi za SADC.
Bahati nzuri
mwaka 2013 Tanzania itakuwa mwenyeji wa mikutano mingine ukiwemo ule wa Global
2013 Smart Partnership Dialogueutakaofanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe
24 – 28 Mei, 2013. Huu ni mkutano unaohusisha nchi nyingi duniani na
kutoka takriban mabara yote. Mkutano huu hukutanisha na kushirikisha
viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta
binafsi wakiwemo wa makampuni makubwa ya kimataifa, wasomi na wawakilishi wa
asasi za kiraia na watu binafsi.
Kwa kawaida katika
mkutano kama huu huwepo agenda maalum, aghalabu kuhusu masuala ya uchumi,
biashara na maendeleo. Mkutano wa mwaka 2013 utazungumzia “Matumizi
ya Sayansi na Teknolojia kwa Ajili ya Maendeleo ya Afrika” (Leveraging
Science and Technology for Africa’s Development). Kwa kweli ni kipaumbele
muafaka kabisa, ndiyo maana na sisi tumefarijika kuukaribisha.
Ndugu Wananchi;
Kuwa mwenyeji
wa mkutano mkubwa kama huu wa watu zaidi ya 500 mashuhuri,
ni heshima kubwa kwa nchi yetu. Ni nafasi nzuri ya kuitangaza Tanzania na
fursa zake za uwekezaji, biashara na utalii. Pia, ni nafasi nzuri kwa
wafanyabiashara wetu kutangaza shughuli zao na fursa za biashara na uwekezaji
wanazotaka kushirikisha wafanyabiashara wa nje. Naomba tuitumie vyema
fursa hiyo adimu kwa manufaa ya taifa na ya waanyabiashara wetu.
Tuwaonyeshe wageni wetu upendo na ukarimu kama ilivyo sifa yetu Watanzania ili
waondoke na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na watamani kurudi tena kutembea au
kuwekeza.
Hitimisho
Ndugu wananchi;
Tunatarajia
kuwa mwaka 2013 utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja
zote kuzidi mwaka 2012. Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa.
Ajira zitaongezeka kwa uwekezaji vitega uchumi kuongezeka na kuwajengea
uwezo wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri
wengine. Kwa ajili hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo,
wanawake na vijana itafufuliwa na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya
Serikali.
Mwaka
2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujituma na
kutimiza wajibu wake. Maisha bora yatakuja kwa kila mmoja wetu kutimiza
wajibu wake ipasavyo. Kama kila mtu atafanya kazi kwa bidii na maarifa,
na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi yake na siyo uhodari wa
maneno yake ya uchambuzi wa hali. Kila mtu achukie uvivu na tabia ya
kulalamika pasipo kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Mimi na
wenzangu Serikalini tunawaahidi ushirikiano wa hali ya juu na kwamba
tutawatumikia kwa moyo wetu wote, kwa nguvu zetu zote na kwa maarifa yetu
yote. Tunataka kukidhi matarajio na imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Tutaendelea kuimarisha utendaji kazi Serikalini na kuhimiza uwajibikaji katika
ngazi zote za uongozi. Tutaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ajizi na
watumishi wasio waaminifu, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma watawajibishwa
ipasavyo. Wananchi pia wanao wajibu wa kuwa raia wema na wazalendo wa kweli kwa
nchi yao. Kila mmoja wetu ajiulize ataifanyia nini jamii yake na nchi yake
badala ya kuuliza itamfanyia nini.
Ndugu
zangu,Watanzania Wenzangu;
Nawatakieni
nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2013. Tusherehekee pamoja kwa
amani na utulivu.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment