Ndugu zangu,
Nchi yetu inapita kwenye kipindi kigumu. Kuna moto unafukuta, tumeshauona moshi mkubwa, ni ishara ya moto mkubwa. Tukikaa chini na kuitanguliza busara na hekima, basi, tuna nafasi ya kuizuia dhahma kubwa inayokuja. Na katika kuifanya kazi hii, bahati mbaya, muda si rafiki yetu. Muda unakwenda haraka.
Kibogyo ni binadamu asiye na meno. Hata hivyo, utafanya kosa kubwa kumdharau kibogoyo, kuwa hana uwezo wa kukudhuru kwa kutumia mdomo wake. Ukweli ni huu, kibogoyo akijawa na hasira, basi, anaweza kukuuma na hata kukuachia alama mwilini.
Kuna hata wanadamu wenzako watakaokuuliza;
" E bwana, hii alama umeumwa na nini?". Na ukweli lazima utajulikana, hata kama utajaribu kuuficha. Kuwa umetiwa adabu na kibogoyo!
Mnyonge mwogope hata katika unyonge wake. Mara nyingi huwa hana cha kupoteza. Ukimkandamiza sana. Basi, hata katika unyonge wake, anaweza kukutemea sumu kali. Ni sawa na mjusi. Ni kiumbe mdogo, lakini, mjusi ukimwandama sana anaweza kugeuka nyoka. Atakudhuru.
Ndugu zangu,
Wanadamu tumeumbwa na mdomo mmoja, macho mawili na masikio mawili. Aliyetuumba alikuwa na maana yake; kuwa tusiongee sana, bali, tuangalie zaidi. Tusikilize zaidi. Na wa kuwaangalia na kuwasikiliza zaidi ni wanadamu wenzako,, bila ya kuwabagua.
Na kwa kiongozi, ni wale unaowaongoza. Hata kama miongoni mwao kuna vibogoyo.
Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
No comments:
Post a Comment