Na Clara Alphonce (email the author)
UZEMBE wa kushindwa kukamilisha ipasavyo taratibu za uhamisho wa kimataifa wa mchezaji Kabange Twite, umelifanya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa) kumzuia kucheza Yanga msimu huu.
Yanga ilimsajili Twite kutoka timu ya FC Lupopo ya DRC wakati wa dirisha dogo, lakini hata hivyo kwa mujibu wa Fifa, taratibu zake za uhamisho hazikukamilika.
Fifa imetoa taarifa za kuliondoka jina la Twite kwenye orodha ya usajili Yanga, ikiwa maana mchezaji huyo ataishuhudia timu yake akiwa jukwaani mpaka mwishoni mwa msimu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura alisema, uhamisho wa Twite una makosa ya kiutendaji ndiyo maana umezuiwa na Fifa.
Wambura alisema hati yake ya uhamisho wa kimataifa (ITC) haikukidhi mahitaji husika wakati ikiombwa na Yanga kupitia njia ya mtandao.
Wambura alisema usajili wa dirisha dogo kwa wachezaji wa kigeni, ulimalizika Desemba 15 mwaka jana, lakini Yanga walimwombea mchezaji huyo ITC kupitia mtandano (TMS) Desemba 15.
“TFF ilimwombea Twite usajili Fifa Januari 7, baada ya tarehe hiyo waligundua kuwa nyaraka walizotumiwa hazikukamilika,” alisema Wambura.
Akifafanua, alisema: “Katika maombi ya mkataba kati ya Twite na Yanga, hakukuwa na saini ya mchezaji pande zote mbili. Hili ni tatizo.”
Aliongeza: “Tatizo lingine ni kutokuwapo makubaliano ya kumtoa mchezaji huyo kwa mkopo (Loan Agreement) kati ya Yanga na FC Lupopo.”
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alishangazwa na uamuzi huo akidai walifuata taratibu zote kama inavyotakiwa.
“Nachofahamu taratibu zote zilifuatwa, aulizwe Abdallah Bin Kleb (Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili) yeye anaweza kutoa ufafanuzi,” alisema Sanga, ambapo hata hivyo alipotafutwa Bin Kleb hakupatikana.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako aliitupia lawama TFF kwa madai ya kuchelewesha taratibu za uhamisho wa Kabange.
Mwalusako alisema walituma maombi yakiwa na saini za pande zote mbili, yaani mchezaji na klabu, lakini ameshangazwa na taarifa za Fifa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment