NA SOMOE NG`ITU
Mshambuliaji mpya wa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Emmanuel Okwi, amesema kwamba kusajiliwa kwake na klabu hiyo ambayo ni moja ya klabu vigogo barani Afrika ni dalili njema na anaamini kuwa sasa amebakiza hatua chache kuufikia mlango wa kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Simba imemuuza kwa Etoile mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda kwa dau la dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 470). Etoile ni mabingwa wa Afrika mwaka 2007.
Akizungumza na NIPASHE jana, Okwi alisema kwamba sasa anaiona Ulaya iko karibu zaidi kwake na kwamba, anachotakiwa kufanya ni kuendelea kucheza soka kwa kiwango cha juu na kuzingatia nidhamu ya mchezo huo.
Okwi alisema kuwa baada ya kukosa timu Austria mwaka jana, kamwe hakuweza kukata tamaa na anamshukuru Mungu kwamba ubingwa wa mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyomalizika mwaka jana jijini Kampala ulimsaidia kuimarisha kiwango chake na kwenda kwenye majaribio akiwa fiti.
"Ewe Mungu, nakushukuru kwa kuniwezesha kutimiza malengo yangu katika kiwango cha juu, bila ya wewe nisingeweza kufika hapa nilipo sasa," aliongeza Okwi, akirejea kile alichoandika juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook.
Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 25 mwaka 1992, aliongeza kwamba kila anachokifanya na hatua anazizifikia katika kucheza kinatokana na juhudi zake na maombi anayoyafanya kila anapomaliza mazoezi.
"Kama ulivyosikia, nimeshapata timu lakini nitakuja kuwaaga Simba ,ni timu iliyonisaidia kufika hatua hii na bado nitaendelea kucheza kwa bidii ili nifikie ndoto zangu," alisema Okwi, mfungaji wa bao la kwanza la Uganda katika ushindi wao wa 3-0 dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kwenye mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Chalenji jijini Kampala ambapo mwishowe Uganda walitwaa ubingwa.
Okwi anaondoka Simba akiwa ameweka historia ya kufunga magoli mawili na kusababisha penati zilizozaa magoli mengine matatu wakati ‘Wekundu wa Msimbazi’ wakipata ushindi wa kishindo wa 5-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga. Mechi hiyo ilichezwa Mei 6 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, ndiye aliyekwenda Tunisia kukamilisha mazungumzo ya kumuuza mchezaji huyo na kusema kwamba tayari taratibu za uhamisho zimekamilika.
Rage alisema kuwa katika mkataba ambao Okwi amesaini, Simba itaendelea kufaidika ikiwa Mganda huyo atauzwa kwa klabu nyingine.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment