“Yesu alianza huduma yake akiwa na miaka 30; lakini wakati anaondoka hakuliacha kanisa mikononi mwa kijana. Alimuachia Petro kuliongoza – mzee. Khalifa wa kwanza wa Umma wa Waislamu Abu Bakr alipokea uhalifa akiwa na miaka 59.”
TUTAFANYA makosa sana kama tutaanza kuangalia uongozi bora na kuuhusisha na jinsia, rangi, kabila, dini au hata umri. Tanzania inahitaji viongozi wenye uwezo kuliko kitu kingine chochote kama kweli tunataka kujenga taifa la kisasa, ambalo watu wake wanafurahia maisha bora ya kisasa. Uwezo wa viongozi ni kama injini ya gari; injini mbovu itakuwa na matatizo kwenye gari na injini nzuri itakuwa ni nzuri kwa gari. Injini isiyo na uwezo haitakiwi kuwekwa kwenye gari.
Februari 11, mwaka 2009, katika toleo la 68 la gazeti hili niliandika makala ambayo ilikuwa na kichwa cha habari “Tatizo la uongozi wetu ni uwezo”. Niliandika haya kabla ya watu wengi kuanza kuhusisha uongozi na umri na hivyo ninaporudia leo japo kwa upande mmoja ninajibu wale wanaoamini kuwa viongozi wazuri ni vijana, vile vile najaribu kuendeleza mada yangu ile ambayo nimeandika kwenye gazeti hili mara kadhaa sasa.
Katika makala ile nilikuwa najaribu kupangua hoja za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, ambaye kwa kila kipimo alikuwa ni miongoni mwa viongozi vijana ambao walikuwa wanachipukia kiasi cha kudhaminiwa kuongoza wizara nyeti ya Mambo ya Ndani.
Ilikuwa ni baada ya barua yake kwenda kwa Waziri Mkuu kujaribu kuingilia mchakato wa mradi wa vitambulisho. Barua yake ile ilinifanya nihoji uwezo wake; si kwa sababu ya umri wake, rangi yake, kabila yake au kitu kingine chochote isipokuwa uwezo wake kuongoza.
Niliandika katika makala ile wakati nahitimisha kumhusu Masha na kusema “Mifano mingine ya nyuma ambayo nimewahi kuandika juu yake bado inasimama kama ushahidi kuwa Waziri Masha hastahili kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Si kwa sababu hajasoma, si kwamba si mwanasheria, si kwa sababu hana sura nzuri! Ni kwa sababu hana uwezo wa uongozi unaotakiwa katika nafasi nyeti kama hiyo ambayo inahusu utawala wa sheria, usimamizi wa amani na utulivu na zaidi ya yote unahusu usalama wa raia wa taifa letu.”
Nikaendelea na kusema kuwa “Kwa vipimo vyote, Masha hana uwezo wa kuongoza. Kuanzia kuingilia kati na kuzungumza kwa niaba ya kampuni ya Deep Green (iliyochotewa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu), kuzungumzia suala la ajira ya mtoto wa Rais kwenye kampuni yake ya kisheria wakati yeye yuko likizo na kampuni hiyo ina uongozi mwingine, suala la yeye kutembelea gerezani saa chache baada ya kina Mramba (Basil) na Yona (Daniel) kutupwa Keko na hata sakata la vitisho dhidi ya Reginald Mengi”
Leo hii tunashuhudia mojawapo ya hoja mbovu kabisa ikijengwa mbele ya jamii yetu ambayo inataka kutufanya tuamini kuwa urais unahusiana na ujana; kwamba mtu akiwa kijana basi atakuwa kiongozi mzuri na –by extension – vijana wapewe nafasi mbalimbali za kuliongoza taifa kwa sababu wao ni vijana.
Sina tatizo kabisa na kijana yeyote mwenye uwezo kupewa madaraka yoyote katika nchi yetu. Sina tatizo hilo kama vile nisivyo na tatizo na mzee yeyote mwenye uwezo kupewa madaraka au mwanamke mwenye uwezo kupewa madaraka kama vile nisivyo na tatizo na mtu wa dini yeyote kupewa madaraka. Sina tatizo na mtu ambaye amewahi kushika madaraka ya Uimamu kupewa uongozi wa nchi kama ana uwezo wa kufanya hivyo kama vile nisivyo na tatizo na mtu aliyewahi kuwa mchungaji kupewa madaraka kama ana uwezo wa kufanya hivyo.
Sina tatizo kama kuna Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu, au Kihindi ambaye ana uwezo akitaka kushika madaraka yoyote nchini kama vile nisivyo na tatizo na Mtanzania Mzigua, Mmatengo au Mndali kushika madaraka hayo kwa kadiri ya kwamba ana uwezo wa kushika madaraka hayo.
Ujana si kigezo, haupaswi kutajwa kama kigezo na wala hautakiwi kabisa kuhusishwa na mtu kupewa madaraka. Kusema kuwa mtu akiwa kijana basi atakuwa ni kiongozi mzuri au kuwa nchi ikipewa vijana basi itakuwa inaongozwa vizuri haingii akilini. Wote ambao leo wanaitwa wazee ndio hawa hawa walioingia madarakani wakiwa vijana. Anne Makinda alianza kushika madaraka akiwa dada mdogo tu. Aliingia bungeni akiwa na miaka 26 na akiwa na miaka 28 aliingia Kamati Kuu ya CCM ambako yupo hadi leo! Leo hata hivyo anastahili kuitwa mzee kwani ana miaka zaidi ya 60!
Hoja hii ya “vijana tuachiwe nchi” ni hoja isiyoingia akilini; inadharau uzee na kwa kweli kabisa inatokana na kiburi kisicho na msingi. Kwani vijana wa zamani (kina Lowassa, Warioba na Wassira) hawakuwa na akili sana. Baadhi ya hawa tunaowaita wazee ndio walikuwa “vichwa” enzi zao. Walipokuwa vijana ukitaja majina ya Salim watu walikuwa wanajua miongoni mwa vijana wenye akili sana. Sasa tunataka kuambiwa kuwa leo hii wazee hawa akili yote imepotea kwa sababu sasa wameota mvi na hawazungumzi kama zamani?
Hivi kweli kama kila profesa duniani na msomi mwenye umri mkubwa angeamua kujiuzulu na kuwaachia vijana kweli mnafikiri dunia ingepiga hatua ya haraka ya maendeleo? Leo hii baadhi ya watu wenye matokeo makubwa zaidi katika sayansi duniani ni wazee! Maprofesa wengi tu ni wazee na wanajitahidi kila kukicha kupitisha ujuzi wao kwenda kwa vijana; sasa vijana waamue tu leo na kusema “well, we can teach ourselves, you old people you need to retire now”! Kweli vyuo vyetu vingekuwaje? Siyo vya Tanzania tu pote duniani elimu bado inatoka kwa wazee kwenda kwa vijana na siyo kinyume chake.
Ni kweli hata hivyo wazee wanapofikia umri fulani wanaanza kupunguza kazi mbalimbali ili wapumzike na kufurahia maisha baada ya kazi ya miaka mingi. Na wengine kutokana na umri miili inaanza kuchoka zaidi na kukaribisha matatizo ya afya. Hili ni kweli kwa kila mwanadamu anayeishi sana – ataazeeka na hata kuugua. Lakini haya si sababu ya kufunga mlango kwa wazee wote na hasa wale ambao bado wana uwezo, akili, na nia ya kutumikia nchi yao.
Tutafanya makosa makubwa kama katika kiburi chetu tutaamua kuwaweka wazee pembeni.
Lakini nyuma ya hili inawezekana kuwa ni hofu; hofu ya vijana kutoweza kushinda mbele ya wazee. Binafsi ningefurahi kusikia vijana wanasimama na kutaka wale wenye uwezo wote wapewe nafasi ya kugombea. Wasisimame na kutaka “wazee watupishe”; kwa nini? Kama vijana wana uwezo na wana uzoefu wa kuweza kuongoza waje na kushindana na wazee wenye uwezo na uzoefu na wananchi waamue nani anawafaa. Lakini haya ya kutaka kuachiwa nafasi ni dalili mbaya; yawezekana wapo vijana ambao wanaamini kuwa hawawezi kushindana na wazee wenye uwezo?
Kama wapo vijana wana uwezo haraka ya nini? Kusema ukweli kwa kijana kusubiri zaidi hakumdhuru kunamsaidia yeye zaidi. Ni kwa sababu hiyo, sioni sababu ya kupunguza umri wa kugombea urais kwa sababu hakuna sababu ya msingi. Kijana anayetaka kuja kugombea urais anaweza kugombea urais akipita miaka 40 kwani atazidi kupata muda wa kujipambanua kiuongozi, na kujionesha kuwa ana uwezo. Vijana wote wanaotaka kuja kugombea urais baadaye wajifunze mbele ya wazee na kukaa miguuni pa wazee kujifunza.
Yesu alianza huduma yake akiwa na miaka 30; lakini wakati anaondoka hakuliacha kanisa mikononi mwa kijana. Alimuachia Petro kuliongoza – mzee. Si kwa sababu hawakuwapo vijana – Yohana alikuwa ni kijana na aliishi kufikia miaka 100 lakini Yesu aliamua kumpa Simon Petro. Khalifa wa kwanza wa Umma wa Waislamu Abu Bakr alipokea uhalifa akiwa na miaka 59. Lakini ikumbukwe wakati Khalif Abu Bakr anaanza Umar Al Khattab alikuwa na miaka 42 (kijana). Umar ndiye aliyemrithi Abu Bakr! Ujana peke yake siyo hoja ni uwezo na Umar alikuwa na uwezo kupita kiasi.
Viongozi wanaotaka kuja kutuongoza watuoneshe uwezo wao katika maono, katika hukumu, katika kujisahihisha, katika kupambanua, katika kuchagua, katika kupima, katika kusema, katika kunyamaza, katika kukataa na katika kukubali. Tutawapima kwa uwezo wao tu si kwa sura, sauti, rangi, dini, kabila au umri au kitu kingine chochote ambacho peke yake hakimpi uwezo wa pekee wa kuongoza. Tutawapima kwa uwezo wao wa kuongoza kwani bado tatizo letu siyo rangi, kabila, au jinsia bali ni uwezo.
source: Raia Mwema: Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment