Gesi yetu na ya kujifunza kutoka Norway
ZAMANI
sana kule Kilwa, Mwarabu aligundua kisiwa cha kuvutia sana; Kilwa Kisiwani.
Akakitamani, na kwa hila, akamdanganya mtawala wa Kilwa akiuze kisiwa hicho kwa
thamani ya shuka iliyokuwa na urefu wa kutosha kuzunguka kisiwa chote!
Mtawala
wa Kilwa akaona ni kitu cha thamani sana. Akakiuza kisiwa cha wananchi. Na
katika Tanzania ya sasa wanaoitwa wawekezaji wakati mwingine hawatofautiani
sana na Mwarabu yule aliyenunua kisiwa kizima kwa shuka tu.
Mikataba
ya hila wanayoingia na tuliowapa dhamana za uongozi inaweza kuwa kujengewa
nyumba ya fahari, gari la fahari na watoto kusomeshwa Ulaya na Marekani. Hayo
tu yanaweza kutosha kumfanya Mtanzania kusaini mkataba wa mwekezaji kuvuna gesi
yetu kwa miaka 25.
Kule
Norway walipogundua gesi yao hawakuwa na wataalamu wa kuvuna gesi. Lakini,
walihakikisha, wawekezaji waliokuja walipewa masharti magumu ikiwamo mikataba
mifupi na kuhakikisha kampuni ya kigeni inaajiri raia wa Norway kwa idadi ya
kuridhisha hata kwenye nafasi za uongozi wa kampuni za gesi, si vibarua tu.
Kwa
mantiki hiyo, WaNorway wale walilenga, kuwa baada ya miaka 15 tu, wawe na
watalaamu wao wenyewe na waanzishe makampuni yao ya kuvuna gesi na mafuta. Na
leo Norway ina kampuni kubwa ya gesi na mafuta inayofahamika kimataifa, inaitwa
StatsOil, imefika mpaka Kilwa, kuvuna gesi yetu. Wanatulipa nini? Ndipo hapa
unakutana na ulimbukeni wetu.
Na gesi
hii ya Mtwara na Lindi haitakuwa na zaidi ya miaka 100 kabla haijaisha. Juzi
hapa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kaweka wazi akiwa
Arusha, kuwa hazina ya kiwango cha gesi kilicho katika miliki ya Tanzania ni
asilimi 15 tu. Asilimia nyingine 85 ya gesi iliyogunduliwa iko mwambao wa
bahari ya Hindi kwenye Pwani ya Tanzania, lakini, kwenye eneo la Kimataifa.
Hivyo, Tanzania kama nchi haina hati miliki ya eneo hilo la bahari. Makampuni
ya kigeni yana ruhusa ya kutafiti na kuanza kuvuna, kutengeneza faida na bila
kuinufaisha Tanzania.
Naam,
Tanzania si nchi ya kwanza kugundulika gesi katika dunia hii. Lakini, kwa
ulimbukeni wetu, tuko katika hatari ya kuipoteza nafasi muhimu kabisa ya
kutumia rasilimali yetu kwa manufaa ya wengi katika jamii. Tutaendelea
kulumbana na kubaki masikini.
Na siku
zote, historia ni mwalimu mzuri, lakini, bahati mbaya kabisa, wanadamu tumekuwa
wavivu sana kujifunza kutokana na historia.
Leo
tumeingia kwenye malumbano ya gesi bila wengi wetu kuwa na ufahamu wa nini hasa
kinaendelea. Hakuna elimu ya kutosha iliyotolewa juu ya gesi yetu.
Leo
Kampuni ya Statoil kutoka Norway ikishirikiana na Exxon Mobil imegundua gesi
katika Visiwa vya Zafaran na Lavan vilivyopo Kitalu 2, Ukanda wa Pwani ya
Tanzania, hususan Pwani ya Kilwa.
Mradi
huo una gharama kubwa pia utafanywa na wageni ambao wana utalaamu wa miaka
mingi katika biashara ya gesi duniani. Lakini, mikataba inasemaje? Na sisi
watatuachia nini inapohusu utalaamu?
Haitoshi
tu kutarajia wageni hao watujengee Hospitali ya kiwango cha Appolo na halafu
tuwe tumeridhika. Ni yale yale ya mtawala na kipande cha shuka. Kwanza hao
wakubwa wanaotibiwa Hospitali ya Appolo Kilwa watakwenda kufanya nini?
Na
tukumbushane pia juu ya kashfa ya gesi ya Songosongo kule Kilwa, imeishia
wapi?
Ikumbukwe,
kampuni ya Pan African Energy iliyosajiliwa kwenye visiwa viwili;
Mauritius na Jersey inaendelea kuvuna gesi ya Songosongo nchini Tanzania huku
ikiwa imeingia mkataba wa miaka 25 na TANESCO kupitia Shirika la Taifa la
Maendeleo ya Petroli , TPDC.
Ni
mkataba wenye kuifanya kampuni hiyo kutokulipa kodi ya faida ya mapato
wanayopata kutokana na mauzo ya umeme unaotokana na gesi asilia wanayovuna Songo
Songo.
Kwa
mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid iliyotolewa mwezi Mei mwaka juzi,
tangu Pan African Energy waanze kuvuna gesi asilia kule Songo Songo mwaka 2004,
kampuni hiyo imevuna faida ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 60. Nusu ya
faida hiyo ilipatikana mwaka 2009 na kampuni hiyo ilitarajiwa kuongeza
uzalishaji. Hivyo, kuvuna zaidi gesi yetu asilia ya Songosongo.
Mpaka
kufikia mwaka juzi, Pan African Energy imefanikiwa kukwepa kodi inayokadiriwa
kufikia dola za Kimarekani milioni 10. Hiki ni kiasi cha fedha
kinachotosha kusomesha watoto wa Kitanzania 175,000 ( Laki moja na sabini na
tano elfu) kwa mwaka kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Action Aid la nchini
Sweden.
Na
tujiulize, je, wananchi wa Kilwa na Watanzania kwa ujumla tunataka kujengewa
hospitali ya kiwango cha Appolo au tunataka wawekezaji tuingie nao mikataba ya
haki na yenye maslahi ya muda mrefu kwa Taifa na yenye kuhakikisha inatuingizia
kodi ya kutosha kutujengea uwezo wa kuijenga nchi yetu wenyewe.
Na
hakika, maswali ni mengi, lakini, hayo machache yanatutaka tukae chini
kama Taifa na kujadili kwa uwazi suala la rasilimali zetu na usimamizi wake kwa
manufaa ya kizazi kilichopo na vijavyo. Nahitimisha.
Source: Raia Mwema: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment