TUNAUANZA mwaka mwingine ‘mpya’ tukiwa na matatizo yetu yale yale ya zamani, isipokuwa tu kwamba yanazidi kuwa magumu kutokana na udhaifu wetu katika kuyashughulikia. Yatazidi kuwa magumu na mazito zaidi kadri tunavyokaribia kile ambacho tumekifanya kiwe ndiyo Alfa na Omega: Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, mwaka 2015.
Ni mwendelezo wa upuuzi ambao nimekuwa nikiujadili katika safu hii, upuuzi unaotokana na jamii kukataa kujisumbua kufikiri. Hivi sasa wapo mamia ya Watanzania ambao wamekuwa wakihaha, na watahaha zaidi mwaka huu kuliko walivyohaha mwaka jana, kuuza majina ya watu wanaowaona kama marais wa mwaka 2015.
Kila kinachotendeka hivi sasa katika medani ya hicho kinachoitwa ‘siasa’ ni kuhusu nani atakuwa Rais mwaka 2015. Hakuna jingine. Kila kinachofanyika, kila kauli inayotolewa, hata kama juu juu, inaelekea kujadili suala la kawaida la maendeleo, inaashiria anayehusika yuko upande upi kuhusu uchaguzi wa 2015.
Tumekwisha kugeuza kuwa taifa la uchaguzi, na uchaguzi umetufanya wajinga wa kufikiria mipangilio ya madaraka mahali pa kufikiria kazi tunayotakiwa kuifanya kuwaondoa wananchi wetu katika lindi la ufukara. Kinachogombewa hivi sasa ni kundi gani, lililoegemea kwa nani, linyakuwe nafasi ya kula, na katika hili watu wanataka kutoana macho.
Katika nchi jirani ya Kenya hivi sasa, zipo harakati kubwa na nyingi za kutafuta makundi yatakayokula baada ya uchaguzi utakaofanyika miezi miwili ijayo. Nao wamo katika homa ya kujipanga na kujipangua katika jitihada za kupata nafasi ya kula kwa kundi hili na lile.
Kwa kiwango kikubwa kuliko hapa kwetu, Wakenya wanafanya hesabu zao kwa msingi mkuu wa ukabila na miungano ya makabila, kila mgombea mtarajiwa akijaribu kuska kwa pamoja muungano wa makabila utaipiku miungano mingine ya makabila.
Angalau Wakenya wanaungana kwa msingi wa makabila, kwani makabila ndiyo mataifa yaliyokuwapo kabla ya Wazungu kutuingilia na kutufanya tuwe kitu kimoja. Kwa maana hii, kabila ni asasi ya utambulisho, inayojitosheleza kwa sababu iliweza kututambulisha kwa karne kadhaa kabla ya ujio wa wakoloni.
Kilichotarajiwa na kilichojaribiwa na baadhi ya viongozi wetu baada ya uhuru, ilikuwa ni kujaribu kuyafanya makabila yetu yaliyokuwa yamefungwa pamoja kutokana na matakwa ya wakoloni, sasa yaungane na kutengeneza taifa kwa manufaa ya makabila yenyewe kwa pamoja.
Majirani zetu Kenya, hawakupata bahati ya kuwa na viongozi wa kulifanya hivyo kwani mtu kama Jomo Kenyatta, alichokifanya ni kuhakikisha kwamba kabila lake ndilo linahodhi kila kitu, na waliofuata baada yake hawakuwa tofauti sana na yeye. Hii imejenga utamaduni nchini Kenya kwamba anayechukua nafasi ya uongozi popote, hata katika kampuni binafsi, anakuwa ni njia ya watu wa kabila lake ‘kula.’
Hivyo ndivyo ilivyo nchini Kenya, na leo hii tunashuhudia namna wanasiasa wa nchi hiyo wanavyohangaika kukusanya makabila, huku wakiambiana kwamba wote wanaweza ‘kula.’ Katika harakati hizo tunazozishuhudia leo nchini Kenya, tunapata uthibitisho halisi kwamba ‘umalaya’ wa kisiasa, ni shughuli iliyohalalishwa na inayoendesha siasa za nchi na utawala wake.
Nchini kwetu, kwa sababu za kihistoria, hatuna ukabila kama uliopo nchini Kenya, au nisema bado hatujawa wakabila kama walivyo wenzetu wa Kenya, kwa sababu hata sisi tunaweza tukawa kama wao iwapo tu tutaenda tunavyoenenda leo.
Nimesema angalau Wakenya wana ukabila wao, hata kama tunasema kwamba ukabila ni mbaya. Nina maana kwamba angalau wao wanao utambulisho waliokuwa nao kabla ya Wazungu kuwavamia, na utambulisho huo ndio ulikuwa msingi wa mataifa yao.
Sisi ambao tulifundishwa kuachana na ukabila ili tujenge taifa moja, tulifundishwa pia kuzingatia misingi ya utaifa huo mmoja. Na baadhi ya mafunzo tuliyopewa na tuliyopeana, ni mshikamano, upendo, kutendeana haki, kukemea ulafi, wizi na rushwa na kadhalika. Lakini yote hayo tumeyaacha, na mahali pake tumejenga jamii ya watu waonevu, wezi, walaghai, waongo, washirikina na wapuuzi!
Halafu, katikati ya hayo yote tunataka kujua ni nani atakuwa kiongozi wetu. Tu wapuuzi wakubwa. Ni heri Wakenya na ukabila wao kwa sababu angalau ukabila una msingi wa kihistoria, wakati upuuzi wetu hauna msingi wowote, isipokuwa watu kujipanga ili waweze kutafuna nchi na wananchi wake.
Tunaingia mwaka ‘mpya’ tukiwa na malumbano ya kila aina ambayo hatujawahi kuyashuhudia. Majadiliano kuhusu Katiba Mpya ni uwanja wa malumbano kwa sababu kumekurupushana kujadili Katiba wakati hatujatafuta mwafaka wa kisiasa; rasilimali zetu kubwa mno hazionekani kuwanufaisha wananchi, ila zinaporwa na wageni; ugomvi unazidi kukua baina ya wananchi na watawala kuhusu matumizi ya rasilimali za taifa.
Elimu yetu ya pamoja ni kama haipo na kila anayeweza, anajitafutia elimu anayodhani itamfaa mtoto wake; athari za elimu ya hovyo zinajitokeza katika ujinga, upuuzi na ushirikina; mamilioni ya vijana wanaranda mitaani bila kazi, uhalifu unaongezeka; msigano unazidi kupanuka kati ya walionacho na wasionacho, na uhasama wa kitabaka unazidi kuongezeka; uonevu umekuwa ni jambo la kawaida, kutoka polisi mwenye silaha dhidi ya raia asiye na silaha, hadi raia mmoja dhidi ya raia mwenzake aliye dhaifu kidogo, na kadhalika na kadhalika.
Katikati ya mapungufu haya, na katikati ya mparaganyiko wa kitaifa ninaouona, watawala wetu wanashindana kujitangaza kwa kufanya kazi mbele ya kamera za TV ili wajulikane kama wachapa kazi. Yeyote anayejua namna Serikali inapaswa kufanya kazi, anajua kwamba huo nao ni upuuzi, ni ubarakala usiokuwa na maana kwa sababu kazi ya Serikali hufanyika kupitia makaratasi na si kupitia amri zinazoelekezwa kwa kamera ya TV.
Lakini wanafanya hivyo ili wapate sifa, na wananchi baadaye waseme kwamba fulani ndiye anafaa kuwa kiongozi kwa sababu alitoa amri nyingi, hata kama hakuna uhakiki wa utekelezaji wa amri hizo wala tathmini ya tija iliyotokana na utekelezaji wake. Hivi tunavyoenenda, hata tukisaka kupendwa na kuchaguliwa, hatuendi kokote.
source Raia mwema: Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment