Dk. Stephen Ulimboka.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini,
|
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, umetoa tamko kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kuagiza watendaji wake kulifungulia gazeti la Mwanahalisi.
Tamko hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Marcos Albanie, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, jana jijini Dar es Salaam.
Albanie alisema tangu serikali itangaze kulifungia gazeti la wiki la Mwanahalisi ni jana siku 175 sawa na kipindi cha miezi mitano na siku 24, wadau wa habari na wananchi wamekuwa wakipaza sauti kuiomba serikali kulifungulia gazeti hilo lakini imekuwa kimya.
Aliongeza kufungiwa kwa gazeti hilo kulitokana na taarifa kuhusiana na kutekwa, kuteswa na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka.
Dk. ulimboka ambaye aliwaongoza madaktari nchini katika kudai maslahi yao bora, vitendea kazi pamoja na mazingira bora ya kazi, kwa hiyo basi wanahoji ni lini serikali litafungulia gazeti hilo ili wasomaji wake wapate haki yao kikatiba ya kupata habari bila kizuizi.
“Ni lini serikali itakuwa na huruma na wafanyakazi wa kampuni ya Hali halisi, inayochapisha gazeti hilo ili kupunguza wimbi la waliokosa ajira nchini,” alisema Albanie.
Aliongeza “Kwa namna yoyote hakuna taifa linaloweza kusema linapinga ukandamizaji wa uhuru wa kupata habari na kutaka iheshimiwe katika jamii ya kimataifa wakati taifa hilo linapendekeza ukandamizaji wa haki nchini mwake.”
“Tunasema hivyo kwa sababu miongoni mwa viashiria vikuu vya udikteta popote duniani ni pamoja na kunyima uhuru kwa vyombo vya habari na kuwatishia wanaharakati wanapodai haki za raia dhidi ya ukiukwaji wa haki unapofumbiwa macho na serikali iliyoko madarakani,” aliongeza.
Kutokana na mazingira hayo mtandao huo umeisihi serikali kuurejea uamuzi wake wa kulifungulia fazeti hilo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment