NA WAANDISHI WETU
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana jioni, Pinda aliondoka jijini Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa ziara ya ghafla nia ikiwa ni kutafuta suluhu ya tatizo hilo ambalo limeanza kutishia amanai nchini.
Taarifa zinasema kuwa Pinda alianza mazungumzo na maimamu wa mjini Mtwara nia ikiwa ni kupata mwafaka wa hali ilivyo mkoani humo.
Mbali na maimamu, Waziri Mkuu pia alikutana na viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta). Hata hivyo hadi gazeti hili linakwenda mitamboni mkutano huo ulikuwa unaendelea na hakuna kiongozi yeyote aliyekuwa tayari kuzungumza mwafaka uliofikiwa katika mgogoro huo ulioanza tangu mwaka jana kwa maandamano ya Desemba 27, mwaka jana.
Waziri Nchimbi naye aenda Mtwara
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, amekwenda mkoani Mtwara kuangalia hali ya usalama kufuatia vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali wilayani Masasi. Dk. Nchimbi hakupatikana jana kuthibitisha ziara hiyo, lakini Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, alithibitisha Dk. Nchimbi kwenda mkoani Mtwara jana kwa ajili ya kuangali hali ya usalama.
“Ameondoka ghafla hata mimi nimeshindwa kuongozana naye na amekwenda huko kuangalia hali ya usalama baada ya kutokea vurugu mwishoni mwa wiki huko Mtwara,” alisema Nantanga.
Alisema kuwa leo taarifa kamili juu ya hali halisi ya vurugu hizo mkoani Mtwara itatolewa pamoja na Dk. Nchimbi alichokiona huko.
Mwishoni mwa wiki, watu wanne walikufa na wengine 12 kujeruhiwa kufuatia vurugu kubwa katika mji wa Masasi zilizoambatana na uchomaji moto wa majengo ya serikali, magari na nyumba za viongozi.
Kwa mujibu wa polisi kati ya watu waliojeruhiwa alikuwamo askari mmoja ambaye amelazwa katika Hospitali ya Ndanda mkoani Mtwara.
Majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Ndanda na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Crisprin Sapuli, alithibitisha kupokea majeruhi hao ambao kati yao wanne hali zao ni mbaya akiwamo polisi.
Habari zinasema kuwa vifo hivyo vilitokana na risasi zilizokuwa zikipigwa hewani wakati polisi wakijaribu kutuliza vurugu hizo baada ya mabomu ya machozi kushindwa kuwatanya wananchi hao.
Vurugu hizo zinadaiwa kusababishwa na maandamano ya kundi la vijana lililokuwa likielekea Ofisi ya Kamanda wa Polisi baada ya askari aliyekuwa akiendesha pikipiki kumgonga mtembea kwa miguu na kumvunja mguu.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa baada ya mtu huyo anayedaiwa kuwa ni dereva wa bodaboda kugongwa kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam -Tunduru, askari huyo aliondoka bila kutoa msaada.
Hali ya usalama katika mkoa huo imezorota kufuatia mgogoro wa gesi ambao wakazi wake wanapinga ujenzi wa bomba la kusafirisha nishati hiyo kwenda Dar es Salaam.
Tayari yameshafanyika maandamano, mikutano ya hadhara na mihadhara ya dini kupinga mpango huo.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro leo litaanza kuchambua majina ya watuhumiwa 19 waliokamatwa na katika vurugu zilizotokea Dumila wilayani Kilosa mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Jeshi hilo limesema baada ya mahojiano, waliobainika kuhusika na vurugu hizo watafikishwa mahakamani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment