WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, January 30, 2013

MGOGORO WA GESI MTWARA:Pinda azima uasi



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda 

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amefanikiwa kutuliza jazba za wakazi wa Mkoa wa Mtwara baada ya kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia amewaomba radhi wananchi wa mkoa huo kutokana na kauli Desemba 21, mwaka jana akiwakebehi baada ya kumwomba apokee maandamano yao ya kupinga mpango wa kusafirisha gesi hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho uliofanyika jana baada ya kusikiliza madai ya wananchi hao kwa siku mbili mfululizo, Pinda alisema hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirisha kwa njia ya bomba na kusema kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa katika Kijiji cha Madimba, mkoani humo ili mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda.
“Wataalamu wanasema gesi haiwezi kwa namna yoyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu… kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba. Gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo,” alisema Pinda na kuongeza:
“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa… gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme… tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme.”
“Gesi lazima isindikwe Mtwara, haitoki hadi viwanda vije… nadhani hili ni jambo jema lazima tuliwekee utaratibu. Nikawauliza wataalamu wangu kwani kiwanda cha kusafisha gesi kinajengwa wapi, wakanijibu Madimba… nikasema kumbe tatizo kubwa ni kutowaeleza vya kutosha wananchi suala la gesi.” alisema Waziri Mkuu huku akipigiwa makofi... “Nafikiri tatizo ni sisi Serikali hatukuwa na mpango mzuri wa kuwaelimisha wananchi.”
Awali, madai ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara yalikuwa ku pinga usafirishaji wa gesi ghafi kwenda Dar es Salaam wakieleza kuwa mpango huo utafukuza uwekezaji wa viwanda mkoani humo ambao ungechochewa na upatikanaji wa malighafi baada ya kusafishwa kwa gesi.
Pia wananchi walipinga uje nzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi, Dar es Salaam wakiitaka Serikali kujenga mitambo hiyo mkoani Mtwara.
Alitoa wito kwa wabunge wa Mkoa wa Mtwara kufuta tofauti zao za kisiasa ili waweze kuharakisha maendeleo ya mkoa huo... “Purukushani hizi ndani ya chama hazina tija, tuseme basi… wabunge hawaelewani, sasa bungeni wanakwendaje... kila mtu na lake … hebu tuseme watu kwanza mimi badaaye,” alisema Pinda huku akishangiliwa.
Katika siku hizo mbili mkoani Mtwara, Waziri Mkuu alikutana na viongozi wa vyama vya siasa, dini, wafanyabiashara, madiwani na wenyeviti wa mitaa na wanaharakati mbalimbali.
RC aomba radhi
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa, Simbakalia aliwaomba radhi wakazi wa Mkoa wa Mtwara akisema alipotoka kuwaita wananchi hao wapuuzi na baadaye wahaini kauli ambazo ziliwaudhi wengi
“Kupitia hadhara hii nawaomba radhi kwa kuwakwaza, nimesikitishwa kwa kauli yangu ambayo imepokewa kwa hisia kwamba niliwadharau,” alisema Simbakalia.
Baadaye Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wa Mtwara kumsamehe Mkuu wao wa Mkoa wa Mtwara kwa kauli hiyo aliyoitoa 21 Desemba, mwaka jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa, (RCC), pale alipoombwa kuyapokea maandamano ya wakazi wa mkoa huo Desemba, 27, mwaka jana.


  
 0
inShare
 “Binadamu kukosea lazima, lakini kubwa zaidi ni kuomba msamaha… amefanya hivyo, sasa tusahau yaliyopita tugange yajayo,” alisema Pinda.
Mawaziri wazungumza
Akizungumzia hali ya usalama mkoani huo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema wizara yake imejipanga vyema kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza kuanza sasa.. “Hali ni shwari, tumejipanga vya kutosha kwa watu na vifaa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa alisema wizara yake imeamua kuifanya Veta Mtwara kuwa kituo cha umahiri ili wahitimu wake waweze kuajiriwa katika sekta ya gesi huku Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akisema wizara yake imekamilisha mipango miji kwa Mji wa Mtwara uendane na mabadiliko ya kiuchumi.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alisema Bandari ya Mtwara haijauzwa na kwamba inapanuliwa ili iweze kukidhi mahitaji ya baadaye huku akiahidi kufika Mtwara kila baada ya miezi mitatu ili kutoa taarifa ya maendeleo ya bandari na uwanja wa ndege kwa wananchi.
“Tulikuwa na eneo la hekta 70 tu za Bandari ya Mtwara, sasa tumepanua na tunazo hekta 2,994. Tumetenga hekta 110 ili tuweze kuwa na bandari huru itakayowezesha kuongezeka kwa matumizi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Wenyeji waridhika
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa vyama tisa vya siasa mkoani Mtwara, Uledi Abdallah alisema madai ya wananchi yalikuwa mitambo ya kusafisha gesi ghafi ijengwe Mtwara na kwamba iwapo Serikali imeamua kufanya hivyo madai yao yatakuwa yamekwisha.

“Kama gesi itakayosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa, sisi hatuna tatizo,” alisema Abdallah
Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji alimpongeza Waziri Mkuu kwa hatua yake ya kuwasikiliza wananchi na kwamba mzozo huo uliodumu kwa takriban mwezi mmoja sasa umefikia tamati.

Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mtwara Mjini, Saidi Kulaga alimpongeza Waziri Mkuu kwa hatua aliyoichukua na kumwomba awaachie huru wale waliokamatwa kutokana na vurugu zilizotokea Mtwara na Masasi ili kujenga mwanzo mpya wa uhusiano baina ya Serikali na wananchi, ombi ambalo Pinda alilipokea na kuahidi kulifanyia kazi ndani ya wiki mbili.

Wataalamu wa gesi
Awali, kutokana na vurugu hizo, zaidi ya wataalamu 50 waliokuwa mkoani Mtwara kwa ajili ya kusimamia mradi wa ujenzi wa bomba la gesi waliondolewa mkoani humo, Mwananchi limebaini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa watalaamu hao wapo Dar es Salaam tangu Jumamosi iliyopita na wamefikia katika Hoteli ya JB Belmont kupisha vurugu za wananchi waliokuwa wakipinga ujenzi wa bomba hilo kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.

Mmoja wa viongozi wa hoteli hiyo, ambaye alikataa kutaja jina lake kwa maelezo kuwa si msemaji alikiri kuwapo kwa watalaamu hao katika hoteli hiyo… “Wapo ila walisema kuwa hawa taki kuzungumza na vyombo vya habari.”

Bunge laingilia kati
Spika wa Bunge, Anna Makinda ameunda kamati itakayokwenda Mtwara kuzungumza na kada mbalimbali kuhusu vurugu na mustakabali mzima wa gesi.

Makinda alisema hayo jana muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha kwanza katika Mkutano wa 10 wa Bunge… “Bunge ni chombo cha amani, tutawatuma wabunge kwenda kuzungumza nao…suala hili linahitaji busara sana.”

Habari hii imeandikwa na Abdallah Bakari (Mtwara), Fidelis Butahe (Dar), Ibrahim Bakari na Habel Chidawali (Dodoma)

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment