WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, January 17, 2013

Madaraka ya Rais kaa la moto




Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amependekeza kuwapo umakini katika kupunguza madaraka ya rais katika uundaji wa Katiba mpya.

Amesema iwapo maamuzi yoyote juu ya suala hilo yatachukuliwa kiholela, kuna hatari rais akashindwa kuwashika Watanzania pamoja kama taifa.

Aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kuongoza makatibu wakuu wa wizara, katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa ajili ya kutoa maoni juu ya uundwaji wa Katiba mpya.

Hata hivyo, makatibu wakuu walioshiriki mkutano huo jana, isipokuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, walikataa kueleza mapendekezo waliyoyatoa, ikiwa ni sehemu ya maoni yao kwa Tume kuhusu uundwaji wa Katiba mpya.

Badala yake, kila mmoja alisema hawawezi kuzungumza wakati bosi wao, Katibu Mkuu Kiongozi yupo.

Balozi Sefue alisema madaraka ya rais wa nchi kama Tanzania yenye mifumo changa, hayapaswi kudhoofika kwa namna yoyote, badala yake yanatakiwa kuwa imara kwa kuwa ndiye anayehodhi mamlaka.

“Hivyo, tusije kumpunguzia madaraka rais kiasi ambacho akashindwa kutushika pamoja kama taifa. Tusiwe wepesi kusema punguza, punguza madaraka ya rais,” alisema Balozi.

Kabla ya Balozi Sefue kusema hayo, tayari baadhi ya makundi katika jamii, wakiwamo wanasiasa, wanaharakati, wafugaji nakadhalika, wamekuwa wakipendekeza kuwapo kwa udhibiti mkubwa wa mamlaka ya rais.

Katika mapendekezo yao, makundi hayo yanataka pamoja na mambo mengine, asiwe na mamlaka ya kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola peke yake na asiruhusiwe kusamehe wafungwa na watuhumiwa.

Pia kila atakayeteuliwa na rais, lazima aombe kazi husika kwenye tume huru za kitaalam na athibitishwe na Bunge, pia rais asiteue Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na asiwe na mamlaka ya ardhi.

MUUNGANO
Kuhusu Muungano, alisema muundo wake ulivyo sasa Watanzania wamedumu nao kwa miaka 50 sasa, hivyo ni mzuri.

“Pale penye matatizo tuyashughulikie,” alisema Balozi Sefue.

MIHIMILI YA DOLA
Kuhusu mihimili mitatu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama), alisema kazi ya katiba ni kuweka sawa mambo, hivyo akasema Katiba mpya inapasa kuhakikisha kila mhimili hauingilii mihimili mingine.

UTEUZI WA MAKATIBU WAKUU
Balozi Sefue alisema utaratibu wa sasa wa uteuzi wa makatibu wakuu wa wizara ni mzuri, hivyo unastahili kuendelea.

MUUNDO WA SERIKALI
Alisema Tanzania ni kubwa, hivyo si ajabu muundo wa serikali kuwa kama ulivyo sasa. Hata hivyo, alisema pia suala hilo linaweza kutazamwa upya. “Lakini tusiseme tu. Kama tunaona ni kubwa basi tubadilishe.”

MAWAZIRI KUWA WABUNGE
Alisema suala la mawaziri kutokana na wabunge ni hoja inayoweza kutazamwa.

Awali, Balozi Sefue aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika mkutano wa jana na Tume, kama Ikulu hawakupeleka waraka wowote bali kila katibu mkuu aliwasilisha maoni yake kwa niaba ya wizara. 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Haule alisema anaona katika Katiba mpya kuwapo na elimu ya lazima au ya kujitegemea katika shule za msingi na sekondari. 

WAKUU WA MIKOA
Katika hatua nyingine, wakuu wa mikoa hapa nchini, wamependekeza kwamba Katiba mpya ijayo itamke suala la umoja na uzalendo kwa wananchi.

Akizungumza katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema viongozi hawapaswi kutoa maoni ya kulalamika, badala yake kazi hiyo ifanywe na wananchi.

Alisema wamependekeza Katiba mpya ijayo, itamke na kutambua utawala wa sheria kwa wananchi wote bila kujali hali ya mtu aliyonayo.

Aidha, mapendekezo mengine ni pamoja na kutaka Katiba itamke na kuwatambua wakulima na wafugaji wote hapa nchini na kuwapa haki sawa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment