DK. Mahathiri Mohammed alikuwa Waziri Mkuu wa Malaysia kwa miaka 22. Hata hivyo, haikuwa ni kazi nyepesi kwake kufikia nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini humo, alipitia mitihani mingi na mikubwa.
Nitaieleza kidogo. Mahathir alikuwa muumini mkubwa wa usawa wa kiuchumi kati ya watu wenye asili ya China na wenyeji wa Malaysia wanaoitwa malays.
Wenyeji walikuwa wanaishi maisha magumu ya ufukara uliokithiri. Alichaguliwa kuwa mbunge katika Bunge la nchi hiyo, mwaka 1964 na akaamua kuwa sauti ya wanyonge wa Malaysia ndani ya Bunge na nje ya Bunge.
Mwaka 1968 aliandika makala kwenye gazeti moja la nchi hiyo na kusema ‘malaysia imevimba hasira za wengi na anahisi patatokea vurugu dhidi ya wachina’.
Wachina ndiyo waliokuwa wakishikilia uchumi wa Malaysia. Akaonya chama chake na serikali kuchukua hatua haraka bila kuchelewa. Hawakusikia. Akaitwa kwenye vikao vya chama chake cha UMNO ajieleze, akafukuzwa uanachama.
Mwaka mmoja baadaye yakatokea maafa makubwa nchini humo, zaidi ya watu 153 waliuawa jijini Kuala Lumpur. Mauaji hayo yanaitwa “matukio ya Mei 13, 1969”.
Hata hivyo, matukio hayo ya Mei yalibadili kabisa mwelekeo wa uchumi wa Malaysia. Mahathir alirudishwa kwenye chama mwaka 1974, akagombea tena ubunge, akashinda, akawa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Elimu, kisha Waziri wa Viwanda na Biashara (wizara yenye hadhi kuliko zote nchini humo). Mahathir Mohamad alichukua madaraka ya Uwaziri Mkuu wa Malaysia Julai 16, 1981, miaka 12 tangu afukuzwe uanachama wa chama chake kwa kusimamia yale anayoyaamini.
Historia itamwandika Mahathiri kama kiongozi pekee katika sura ya dunia aliyeweza kufuta umasikini wa nchi yake katika kipindi cha miongo miwili. Mwaka 1976 wakati anashika madaraka ya unaibu waziri mkuu, Malaysia ilikuwa na watu masikini asilimia 56 ya watu wake wote. Wakati anaondoka madarakani mwaka 2003, asilimia tatu tu ya watu wa Malaysia ndio walikuwa masikini. Rekodi hii haijawahi kufikiwa na nchi yoyote duniani.
Mahathiri alifanikiwa kuzungumza kama mwananchi wa kawaida, kiongozi wa kitaifa na mpinzani wa serikali na chama chake kwa wakati mmoja. Ni watu wachache sana wenye talanta ya namna hii na mara zote hupata misukosuko mingi, lakini hatimaye hushinda mitihani hiyo iwapo misukosuko hiyo haitamaliza maisha yao.
Mama Indira Gandhi aliyekuwa Waziri Mkuu wa India alipata misukosuko mingi, mingine aliishinda. Mingine ilimwangusha kwa muda na hatimaye maadui zake walimuua.
Naelewa kwamba mauaji ya Indira Gandhi yalisababishwa na chuki za watu wa kabila la sikhs nchini humo kutokana na ‘operation BlueStar’, hata hivyo vita ya mwaka 1971 na hali ya hatari aliyotangaza mwishoni mwa miaka ya sabini ilimfanya ajenge maadui wengi sana. Hata hivyo, kuna masuala kadhaa ya kujifunza kutoka katika maisha ya kihistoria ya mama huyu.
Baada ya baba yake Mzee Nehru kufariki na miaka michache baadaye wazee wa chama cha Congress kuamua kumteua Indira kuongoza chama chao, walitaraji kuwa watamtumia mwanamama huyu kufanya mambo yao watakavyo, akiwa hana msimamo wake au mwono wake wa India anayoiongoza.
Walikosea kumsoma. Indira aliungana na viongozi vijana wa chama cha Congress kufanya mabadiliko makubwa yenye mrengo wa kushoto dhidi ya mawazo ya wazee kama Morarji Desai aliyekuwa Waziri wa Fedha na mwenye mrengo wa kibepari katika kuendesha uchumi wa India.
Wakati Indira Gandhi na vijana walioitwa ‘young turks’ walikuwa wanasimamia misingi ya asili ya uanzishwaji wa chama chaCongress, msingi wa mabadiliko makubwa ya kijamii (‘prime instrument of social change’), wazee ambao waliitwa kwa kiingereza ‘syndicate of bosses’ walitaka kuendelea na hali ilivyo ambapo wenye nacho wanaendelea kufaidi matunda ya uchumi na watu masikini wanaendelea kuwa katika dimbwi la ufukara. Indira alichukua uamuzi wa kutaifisha benki zote na njia kuu za uchumi.
Wazee hawa wakamfukuza uanachama wa chama cha Congress. Indira Gandhi alianzisha chama kipya The Congress Requisitionistsambayo baadaye ilikuja kujulikana kama The Congress (I) ambapo watu waliita I kuwa inasimama kwa Indira!
Aliwashinda, akaendelea kuwa Waziri Mkuu wa nchi yake, akashindwa uchaguzi wa mwaka 1977.
Waliomshinda wakamkata na kumfunga jela hali iliyoleta taharuki nchi nzima, serikali mpya ikapoteza umaarufu kabisa kwani ajenda yao ilikuwa moja tu ‘chuki dhidi ya Indira’ na hawakuwa na ajenda ya kuijenga India. Mwaka 1979 chama cha Congress kilirudi madarakani. Indira aliuawa mwaka 1984 Oktoba, akiwa Waziri Mkuu wa India.
Tofauti ya Indira Gandhi na Mahathir ni kwamba Mahathir aliishi kuona mabadiliko makubwa aliyoyafanya kwa ajili ya nchi yake. Mama Indira hakuweza kuona lakini uamuzi wake wa miaka ya sabini kuhusu kilimo na maendeleo ya viwanda ndio umeipandisha India leo kuwa moja ya taifa lenye uchumi imara duniani.
Kwa nini leo nimeandika kuhusu watu hawa? Wasomaji wangu watakuwa wanahisia zao ambazo siwezi kuzizuia. Ujumbe wangu ni mwembamba sana kwamba mitihani kwenye siasa ni suala la kawaida.
Nchi yetu na vyama vyetu vya siasa vinapita kwenye vipindi vigumu sana. Hata hivyo, wachambuzi wetu wa masuala ya kisiasa hawayaweki haya mapito kwenye muktadha wa historia ama ya nchi yetu au ya mataifa mengine.
Vyama na nchi yetu imekuwa na vimekuwa ni mahala ambapo mawazo tofauti, maono tofauti na mitindo tofauti ya kufanya siasa au kuongoza imekuwa ni uadui na usaliti. Ni aghalabu sana kuona mtu ana mawazo tofauti bila kuonekana ametumiwa au amenunuliwa.
Mwanasiasa akisema jambo kinyume cha mawazo ya wenzake kwenye chama chake siku zote anaonekana ni mwanasiasa mkorofi na mipango inasukwa kumshughulikia mwanasiasa huyo.
Mwananchi akitoa mawazo tofauti na mawazo ya watawala anaonekana anatumika na watu wasiotajwa hata siku moja. Kiongozi wa kitaifa akionya kuhusu masuala fulani fulani ya nchi, atashambuliwa kwa kuonekana ni mbinafsi au anatafuta umaarufu. Hata kama mambo hayo hayo aliyoyasema yanakuja kusemwa baadaye na watu hao hao.
Nimesema hapo mwanzo, kwamba Mahathir Mohammad aliweza kuunganisha majukumu ya mwananchi wa kawaida, kiongozi wa kitaifa na mpinzani wa serikali kwa wakati mmoja. Mazingira ya kisiasa ya mwaka 1969 nchini Malaysia ndio yaliyopo hivi sasa nchini.
Mwanasiasa anayejaribu au kuthubutu kuwa mwanasiasa huru mwenye maono yake na mwenye uhuru wa kuweka mawazo hayo waziwazi, haishi kushambuliwa na kuitwa kila aina ya majina.
Mazingira ya ‘zidumu fikra za Mwenyekiti’ bado hayajaisha katika nchi yetu. Inafikia wakati hata kumpinga Rais wa nchi ni amani zaidi kuliko kumpinga kiongozi wa chama chako cha siasa, hii ni kwa vyama vyote.
Ukisoma maoni ya watu kuhusu suala la ‘matukio ya Mtwara Desemba 27, 2012’ utaona namna ambavyo taifa na uongozi vina uvundo wa uongozi mbovu na kuendeleza tabia ya ‘kutafuta mchawi’.
Mara moja viongozi walianza kusema watu wanatafuta umaarufu. Hata ndani ya vyama vya siasa ilionekana hivyo hata kama misimamo ya vyama hivyo ni dhahiri kabisa kuhusu suala la rasilimali za taifa.
Watu wa Mtwara walihitaji sauti ya kuwalinda, watawala wakaanza kushambulia sauti hizo kwa madai ya kipuuzi kabisa kama vile ‘kutafuta umaarufu’ ‘kununuliwa na wawekezaji’ nk ilihali wenye mamlaka wanasema ‘vurugu za Mtwara zitakimbiza wawekezaji’.
Nani anayetumika na wawekezaji katika hali hiyo. Ndani ya vyama vya siasa nako kauli hizo hizo za watawala zinanunulika kwa maneno ya ubinafsi, kiherehere, kutafuta umaarufu, badala ya kutumia fursa za viongozi wenye kubobea kwenye masuala hayo kuongoza kuweka sawa ajenda ya wananchi.
Koffi Olomide amewahi kuimba ‘Lokuta eyaka na ascenseur, kasi verite eyei na escalier mpe ekomi’ ambayo ina maana ‘uongo hutumia lifti kupanda gorofa; ukweli hutumia ngazi lakini utafika tu. Ukiona uwezo wa viongozi wetu kufanyia kazi habari za uongo au hata wenyewe kutengeneza uongo, utajiuliza sana ubora wa uamuzi wao kuhusu nchi yetu. Viongozi wanasahu kuwa uongo huwafikia haraka sana kabla ya ukweli na hivyo wanapofanya uamuzi kutokana na uongo, ukweli ukifika inakuwa ‘too late’.
Naamini Ali Kiba au MwanaFA wataimba ‘ukweli hautengenezwi bali hutafutwa’.
Mahathir alifukuzwa uanachama wa UMNO kwa kosa moja kubwa sana, mawazo yake huru. Indira Gandhi alifanyiwa hujuma na wazee wa chama chake kwa kosa moja kubwa sana, mawazo yake huru. Wote walishinda na kuongoza nchi zao. Walivuka mitihani mikubwa.
Wakati mwingine ni vema kuwapa maadui zako watakacho na wewe kubakia ‘mwananchi, mwanasiasa wa kitaifa na mpinzani wa ‘status quo’.
source: Raia mwema Zitto Kabwe
No comments:
Post a Comment