TUNAANZA kuyumba! Tunaacha hoja ya msingi ya kujenga umoja wetu kitaifa, tunakimbilia Utanganyika na udini! Tunataka tusitake, kitu muhimu si Tanzania, Tanganyika au imani zetu za kidini; ni umoja wetu wa kitaifa.
Bila umoja wa kitaifa, sote hatuko salama! Matajiri, masikini, wazee, vijana, viongozi wa dini, watawala pamoja na vizazi vijavyo hawatakuwa salama. Hata mjinga wa mwisho ni lazima aelezwe hili na kulielewa. Ikitokea tukawa na vichaa, ni lazima tutafute mbinu za kuwaeleza vichaa hawa waelewe salama ya taifa letu; ikishindikana, basi vichaa hawa wafungiwe sehemu hadi pale tutakapofanikiwa kujenga umoja wetu wa kitaifa.
Tunaposhiriki kuandika Katiba mpya, ni muhimu kusimamia na kuitetea hoja yetu ya msingi. Tusiyumbishwe na wajanja wachache wenye ajenga za siri za kuibua Tanganyika (kikiwa kisingizio chenye ushawishi mkubwa) na kujificha nyuma ya mapazia ya udini. Wachache hawa, lakini wenye nguvu za kutisha hawana nia njema kwa taifa letu. Tukisimama imara na kuuweka ujinga nyuma yetu, tutawashinda!
Baada ya Uhuru wetu, kazi kubwa ilikuwa ni kuimarisha umoja wa kitaifa, kupandikiza moyo wa kizalendo kwetu sote. Maana mkoloni alikuwa amefanya kazi ya kuwafanya Watanzania kujichukia, kuchukia mila zao, miungu wao na hata lugha zao.
Mkoloni alitawala nchi, miili yetu na fikra zetu! Jukumu hili la kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo lilikuwa ni la kila Mtanzania mwenye upeo wa kuona mbali. Mwalimu Nyerere, alijitahidi kujenga umoja na kupandikiza uzalendo. TANU na baadaye CCM, kwa wakati ule kilikuwa na picha tofauti. Kutojiunga na chama, kulionekana kama usaliti.
Sababu kubwa ikiwa kwamba wakati wa mkoloni, kuna vyama vilivyounga mkono wakoloni waendelee kutawala. Lakini pia kulikuwa na vyama vilivvyotaka Tanzania ibaki ni ya watu weusi tu! Vyama hivi vilitaka kuifuta historia.
Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, chini ya Azimio la Arusha, lengo lake lilikuwa kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo. Mwalimu Nyerere, alitaka tuutangulize utaifa, kabla ya chochote. Alitaifisha shule na hospitali za mashirika ya kidini, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki sawa. Wajinga wanaeneza propaganda kwamba Mwalimu, alifanya makosa kutaifisha mali na kuanzisha Ujamaa.
Vijiji vya Ujamaa, Jeshi la Kujenga Taifa na Azimio la Musoma, vililenga kumtengeneza Mtanzania mzalendo. Wakati ule tulikuwa na chama kimoja cha siasa. Ingawa si watu wote waliojiunga na chama cha siasa, lakini wengi walikuwa na imani juu ya nia ya chama hicho cha siasa.
Na kusema kweli chama hicho kiliangalia maslahi ya kila Mtanzania – ni tofauti kabisa na sasa hivi tunaposikia misemo ya CCM ina wenyewe na hao wanaCCM wanafikiri wao ndiyo Watanzania pekee wenye haki zaidi ya wengine!
Mwalimu, alitengeneza falsafa ya chama kimoja, akaielezea na watu wakaielewa. Wengi walipenda mfumo wa chama kimoja. Waliona umuhimu wa chama cha Mwalimu, kilicholenga kuunda umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo.
Bahati mbaya tulikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi kabla ya kuimarisha umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli. Vitu hivi viwili ni vigumu kuvijenga katika mfumo wa vyama vingi. Mfumo wa vyama vingi unafaa kwa nchi iliyokwishafanikiwa kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli, si chini ya miaka 100. Nchi changa kama yetu ni vigumu kuendesha siasa ya vyama vingi bila utengano na wakati mwingine vita au mapambano ya dola na vyama visivyo madaraka.
Wakati wa mkoloni, kigezo cha kupima uzalendo wa mtu ilikuwa ni uanachama wa chama cha sSiasa, na hasa chama kilichokuwa kikilenga kuleta ukombozi, kama TANU ambacho baadaye kiligeuka na kuwa CCM, baada ya kuungana ASP cha Zanzibar.
Mtizamo huu ambao ulikuwa na maana wakati ule, umeendelea leo hii. Watu wengi, na hasa wale wanachama wa CCM, bado wanafikiri kigezo cha uzalendo ni kujiunga CCM. Kwamba aliye nje ya CCM ni msaliti!
Tatizo hili limejitokeza kwa vile wimbi la kuanzisha vyama vingi lilikuja kabla ya wakati, bila maandalizi! Kwa upande mmoja ni vizuri na kwa upande mwingine ni vibaya. Ni vizuri kwa sababu chama kimoja, kinawafanya watu kushindwa kuona ukweli wa mambo katika jamii.
Vyama vingi vya siasa vinasaidia kufichua dosari na kukifanya chama kinachotawala kisijisahau. Lakini kwa upande mwingine ni vibaya maana, kinachotokea kuanzisha vyama vingi bila msingi imara, matokeo yake ni kuendeleza chama kimoja, kama ilivyo sasa hivi kwa CCM.
Kama tungelikuwa tumefikia ukomavu wa kisiasa, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CCM kingevunjwa kwanza, na vyama vyote vikaanza upya.
Tungeanzisha vyama ambavyo nia na lengo kubwa lingekuwa kujenga taifa katika mshikamano na uzalendo. Vyama vingekuja na sera mbalimbali kutimiza lengo hilo. Kwa vile CCM, inatokana na vyama vilivyoshiriki kumfukuza mkoloni na ni chama kilichoendelea kutawala hadi tunaingia mfumo wa vyama vingi, kinapata upendeleo wa historia.
CCM, ambayo ilitokana na TANU, lengo lake la msingi lilikuwa kupambana na mkoloni na kuleta uhuru. Kazi hii ilifanyika vizuri. Baada ya hapo CCM, iliendelea kufanya kazi ya kuimarisha uhuru wetu. Kwa maoni yangu, kazi hii ingeendelea zaidi ya miaka 50, kabla ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa. Maana, tungeanza na mfumo wa vyama vingi tukiwa na agenda tofauti na ile ya ukoloni.
Nyakati hizi tulizomo, ni vigumu chama cha siasa kujenga umoja wa kitaifa. Tunahitaji chombo cha kujenga umoja wa kitaifa, kuwakusanya Watanzania bila kujali itikadi zao za vyama. Na kwa hiyo, si muhimu sana kuwa Tanzania au Tanganyika, muhimu ni umoja wetu wa kitaifa.
Bila kuwa na lengo mmoja kama taifa, mfano kama lengo letu la zamani la kumfukuza mkoloni, ni vigumu kuyafikia maendeleo ya kweli. Ni lazima tuwe na chombo cha kutuunganisha, kiasi kwamba CHADEMA, ikiingia madarakani ifanye kazi na Watanzania wote, bila kuangalia imani zao za vyama na dini zao.
Ikitawala TLP au CUF ifanye kazi na Watanzania wote bila kuangalia imani zao za vyama na dini zao. Na ikitawala CCM, kama inavyofanya sasa ifanye kazi na Watanzania wote pia. Ujenzi wa chombo cha umoja wetu ni lazima utajwe kwenye Katiba mpya.
Tunahitaji chombo cha kututoa usingizini na kutufundisha kwamba chama cha siasa, si kitu cha kwanza katika taifa, utaifa ndicho kitu cha kwanza na vingine vinafuata. Leo hii chama ndicho kitu cha kwanza na mengine yanafuata. Huku ni kupotoka!
source; Raia Mwema: Privatus Karugendo
No comments:
Post a Comment