UCHAGUZI katika kata 29 umehitimishwa wiki iliyopita, na matokeo
kujulikana ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda katika kata 22 (75.8%),
CHADEMA kata 5 (17.2%), huku TLP na CUF wakishinda katika kata moja
moja (3%).
Kwa tathmini ya juu juu, ni rahisi kufikia hitimisho kwamba CCM
kimeshinda kwa kishindo na kuwagaraza vibaya wapinzani wao, na hasa mahasimu
wakubwa kisiasa, CHADEMA. Aidha kwa matokeo haya, viongozi, wanachama na
wapenzi wa CCM watarukaruka kwa furaha wakishangilia si ushindi tu, lakini kile
kinachoonekana kuwa ni kuendelea kupendwa pamoja na kwamba chama chao
kimevurunda vibaya katika kila nyanja.
Matokeo haya pia yanaweza kuwanyong’onyesha baadhi ya viongozi,
wanachama na wapenzi wa CHADEMA, kwamba pamoja na juhudi zote walizofanya
katika kampeni, na muonekano wa nje wa kuchokwa kwa CCM, wameweza kuambulia
kata tano tu!
Matokeo haya pia yana hatari kisaikolojia kwa upande wa
upinzani. Hii ni kwa sababu wananchi wapenda mabadiliko wanaweza kurudi nyuma
wakiamini kwamba kama kwa mazingira ya sasa CCM inaweza kushinda uchaguzi kwa
kiwango cha asilimia 75, basi pengine chama hiki haking’oleki kutoka
madarakani, na hivyo kuanza kuwa na mtazamo wa ‘kukubali yaishe’.
Hata hivyo, katika kufanya tathmini ya matokeo ya uchaguzi huu
ni muhimu kuelewa vizuri mantiki ya uchaguzi mdogo kabla ya kufikia hitimisho.
Mantiki ya uchaguzi mdogo ni fursa ya kutetea ushindi uliopata katika uchaguzi
uliopita na kujipima nguvu upya kwa chama ambacho kilishindwa katika uchaguzi huo.
Kwa hivyo, unapofanya tathmini ya matokeo katika uchaguzi mdogo
jambo la kwanza la kuangalia ni je vyama shindani vimeweza kutetea viti
walivyokuwa navyo awali?
Ndiyo maana katika chaguzi za namna hii vyama vilivyoshinda
awali hupigana kufa na kupona kama tulivyoona CCM ilivyopambana katika chaguzi
za Igunga na Arumeru Mashariki. Ndivyo vile vile tutakavyoona jinsi CCM
itakavyopigana katika Jimbo la Sumbawanga na ambavyo CHADEMA itapigana katika
Jimbo la Arusha Mjini kama uchaguzi utarudiwa pia katika jimbo hili.
Sasa katika uchaguzi wa kata hizi 29 ni muhimu kukumbuka kuwa
CCM ilikuwa imeshinda katika kata 26, CHADEMA kata mbili na TLP kata moja.
CHADEMA na TLP wamefanikiwa kutetea kata zao walizoshinda awali huko Rombo na
Mtibwa (CHADEMA) na Kilema (TLP). Zaidi ya kutetea kata zake ilizoshinda awali,
CHADEMA pia wameongeza kata nyingine tatu za Daraja Mbili huko Arusha, Ipole
huko Tabora na Malangali huko Ludewa, Iringa.
Ndiyo kusema, kitakwimu, CCM wamepoteza ushindi walioupata awali
kwa asilimia 15.4 na CHADEMA wameongeza ushindi walioupata awali kwa asilimia
150! Kwa hiyo, kwa lugha ya kitakwimu, hakuna shaka kwamba CHADEMA wamepanda na
CCM wameshuka.
Namna nyingine ya kuangalia matokeo haya kitakwimu ni idadi ya
kura ambazo vyama hivi viwili wamepata. Katika ujumla wake, CCM wamepata kura
29,558 na CHADEMA wamepata jumla ya kura 20,884, ambayo ni tofauti ya kura
8,710 ambayo ni sawa na asilimia 17.3. Hii si tofauti ya kura ambazo CCM
wamekuwa wakijivunia huko nyuma. Hii maana yake ni kwamba CCM hawawezi tena
kushinda uchaguzi wowote kwa kishindo, na hiyo ni hatua muhimu katika kuelekea
kifo chake.
Hata hivyo, kihesabu ni kwamba CCM wamepoteza viti vinne tu
dhidi ya vile walivyoshinda awali, na CHADEMA wameongeza viti vitatu pekee. Kwa
hiyo kwa mantiki ya kihesabu ushindi wa viti vitatu ni mdogo mno ukilinganisha
na mvuto ambao CHADEMA inayo sasa hivi kwa jamii ya Watanzania. Vile vile
kupoteza viti vinne kati ya viti 26 vya awali sio jambo la kutisha kwa chama
kilichochokwa kama CCM.
Hivyo hitimisho ambalo tunalipata kwa matokeo haya ya udiwani ni
kwamba CHADEMA inakua na CCM inasinyaa, lakini kwa kasi ndogo. Kwa kasi hii ya
ukuaji wa CHADEMA na kusinyaa kwa CCM inaweza ikachukua muda mrefu wa kuing’oa
CCM madarakani kuliko ‘wapenda mabadiliko’ walivyofikiria.
‘Wapenda mabadiliko’ nina maanisha wale Watanzania wanaoamini
kwamba CCM ni kikwazo katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo ya dhati na
katika kujenga taifa linalokua kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni, na
hasa taifa linalokumbatia demokrasia na utawala wa sheria kiukweli na
kiuhalisia. Binafsi siamini hata kidogo kwamba inawezekana taifa letu
likayafikia mambo haya kama CCM itaendelea kuwa madarakani.
Funzo tunalolipata katika matokeo haya ni kwamba mvuto na kura
si lazima viendane, hasa katika mazingira ambamo wapiga kura wachache
hujitokeza kwenda vituoni kupiga kura.
Chama cha siasa hupitia hatua kuu nne katika kufikia hatua ya
kushinda uchaguzi. Hatua ya kwanza ni ya kisheria ambapo chama kinatambulika
kisheria kwa kusajiliwa rasmi na kuruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa.
Hatua ya pili ni kujulikana kwa wapiga kura, kwamba kuna chama
cha siasa na kina viongozi fulani. Juhudi za viongozi katika kukiuza chama chao
hukifisha chama hicho katika hatua ya tatu ambayo ni ufuasi. Ufuasi wa chama
cha siasa huonekana katika mazungumzo ya kila siku ya wananchi na kwa jinsi
wananchi hao wanavyoitikia mikutano na shughuli nyingine za umma kama vile
kukichangia chama hicho.
Hatua ya mwisho ni kubadilisha idadi fulani ya wafuasi kuwa
wafia chama, ambao ndio wanaoweza kukipatia chama ushindi, hasa katika
mazingira makali ya ushindani.
Kwa sasa hivi hakuna shaka kwamba CHADEMA wameweza kupata
wafuasi wengi kama inavyoonekana katika mazingira mbalimbali. Katika mazungumzo
ya kila siku linapokuja suala la siasa unaona hamasa ya Watanzania kwa CHADEMA.
Kwa wale waliowahi kusafiri na gari mpya za CHADEMA (M4C)
watakumbuka jinsi ambavyo wananchi huhamasika barabarani mara wazionapo gari
hizi kwa kuonyesha vidole viwili. Madereva wa malori na mabasi ya abiria hawasiti
kupiga honi mara wazionapo gari hizi, na hata baadhi ya askari wa barabarani
hudiriki kuonyesha vidole viwili mara wazionapo gari hizi zikipita.
Mikutano ya CHADEMA imebadilika kabisa kutoka enzi za akina Mzee
Mtei kuhutubia ‘miti’ na sasa mikutano hiyo ikijaza maelfu kwa maelfu ya
wananchi waliojaa hamasa na hamu kubwa ya mabadiliko.
Hata hivyo, bado CHADEMA hawajifikia hatua ya nne, ambayo ni
muhimu sana katika kujihakikishia ushindi. Hatua hii ni ile ya kupata wafia
chama. Ili kujihakikishia ushindi ni muhimu kabisa chama cha siasa kiwe na
wanachama wafia chama.
Hawa ni aina ya wanachama ambao watakipigia kura wakati wowote
iwe mvua, iwe jua. Hili ni kundi muhimu sana kujihakikishia ushindi katika
mazingira ambayo wananchi wengi hawajitokezi kupiga kura, ambalo limeanza kuwa
jambo la kawaida katika chaguzi zetu.
Ni kundi hili ndilo ambalo limebaki kama mpira wa kupumulia kwa
CCM. Hawa ni watu ambao hawatakuja kamwe kugundua ubaya wa CCM hadi
kitakapotoka madarakani na ni kundi hili ambalo limeiwezesha CCM kushinda
katika uchaguzi wa madiwani uliokamilika wiki jana, ambapo katika baadhi ya
kata idadi ya wapiga kura waliojitokeza walikuwa chini ya asilimia 20.
Nahitimisha kwa kutoa wito kwa wapenda mabadiliko. Kwamba
kupenda na kutamani tu mabadiliko hakutoshi, inabidi kushiriki katika kuyasaka
hayo mabadiliko. Tabia ya baadhi ya wapenda mabadiliko kudhani kwamba kikundi
fulani cha watu katika chama fulani ndio wenye jukumu la kuleta mabadiliko
itatufanya tukae katika mfumo wa utawala tuliouchoka kwa muda mrefu.
source Raia Mwema: Kitila Mkumbo
No comments:
Post a Comment