NA WAANDISHI WETU
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema anaendelea kutishiwa kuuawa na vyombo vya usalama na kwamba njama zote zinazopangwa dhidi yake amezibaini.
Hata hivyo, Dk. Slaa amesema hataacha siasa kutokana na vitisho hivyo na yupo tayari kufa kwa ajili ya kutetea umma wa Watanzania katika kupata haki yao ikiwamo kunufaika na rasilimali zao ambazo zinanufaisha watu wachache.
Aliyasema hayo katika viwanja vya Railway, Manispaa ya Moshi jana na katika viwanja vya Kwasa Kwasa mjini Same wakati wa mikutano yake ya hadhara.
“Nimetishiwa kuuawa zaidi ya mara tatu na hadi sasa wahusika wanaendelea na mipango ambayo yote inavuja na kutufikia Chadema,” alisema na kuongeza: “Sitaacha siasa kwa vitisho vyao ndiyo kwanza nasonga mbele nimejitoa maisha yangu.”
Aliongeza kuwa bahati mbaya mipango inayopangwa imekuwa ikivuja kwa kuwa nyumba yao inavuja na hivyo wenye uchungu na nchi wamekuwa wakitoa taarifa hizo.
Alililaumu Jeshi la Polisi kwamba linaminya demokrasia kwa kutolea mfano kitendo cha Jeshi hilo kuwazuia vijana kutundika bendera za Chadema katika pikipiki juzi katika Manispaa ya Moshi na jana mjini Same.
KAULI YA POLISI
NIPASHE ilipomtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, kuzungumzia madai ya kiongozi huyo, alisema hajapata taarifa na kutaka apelekewe ushahidi ofisini kwake.
“Mimi na wewe tuko Dar es Salaam, sasa tunayajuaje mambo yanayoendelea huko Kilimanjaro?” Senso alihoji na kuongeza:
Kama wewe una ushahidi kuhusiana na taarifa hizo, ninaomba uniletee document (nyaraka) kesho (leo) asubuhi ofisini kwangu zikiwa zinaonyesha alizungumza wapi na tarehe ngapi.”
Licha ya NIPASHE kumsisitizia kwamba Dk. Slaa alitoa kauli hizo katika mikutano ya hadhara ambayo wengi walisikia, lakini hakukubali na kusisitiza kwamba apelekewe nyaraka hizo ofisini kwake.
“Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao na ofisi zao zipo wazi saa 24 nchi nzima, hivyo kila mtu anaruhusiwa kutoa taarifa,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa wewe unataka kutoa taarifa, ninamuomba aje ofisini kwangu asubuhi,” alisisitiza.
Dk. Slaa alipoulizwa na NIPASHE jana mjini Same kama amewahi kuripoti matukio ya vitisho dhidi yake kwa vyombo vya dola, alisema hatakwenda katika chombo chochote cha dola kwa kuwa hao hao ndiyo wanaotaka kumdhuru.
KADI YA CCM
Alisema wanaoeneza propaganda za kuwa ana kadi mbili ikiwamo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni wapuuzi na wamekosa cha kuzungumza.
Alifafanua kuwa ni hiari ya anayejiunga na chama kingine kuamua kadi ya chama cha awali aliyonayo aifanye nini.
Kuhusu mauaji ya watu katika mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Tabora, Kamati Kuu ya Chadema imetoa muda (hakusema siku ngapi) kwa serikali kuhakikisha inachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuunda tume ya kimahakama ya uchunguzi wa mauaji hayo.
“Tumeipa serikali muda wa kuunda tume hiyo na kuchukua hatua stahiki, vinginevyo nchi haitakalika, viongozi wanahubiri amani ya kinafiki huku watu wakiuawa kama kuku, hadi leo wameendelea kumkumbatia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, ambaye alikuwa umbali wa mita kumi wakati mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi, anauawa,” alisema.
Alisema kutokana na kelele za viongozi wa Chadema, dunia nzima imejua juu ya mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na Japan, wamejua na wanafuatilia kwa karibu.
Alisema uwezekano wa baadhi ya viongozi kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi ni mkubwa na hawataacha kupiga kelele kwa kuwa raia wanauawa hovyo.
“Tumeitaka serikali kuwachukulia hatua mafisadi wote, vinginevyo hatutakuwa na muda wa kuhurumiana wala kubembelezana, Katiba imetamka wazi kuwa jukumu la kusimamia rasilimali za taifa ni la wananchi na si serikali, hivyo tutasimamia na wanaosema wamechoka kusikia suala la mafisadi, wakae chonjo kwani mpambano ndiyo kwanza umeanza,” alisema.
Dk. Slaa alisema kuanzia Januari 26 hadi 28, mwaka huu, Kamati Kuu, Baraza Kuu la Chadema, wataanza kutoa matamko makali dhidi ya serikali ya CCM kulaani mambo ya ufisadi, mauaji ya raia na mengine ambayo yanairudisha nchi kwenye umaskini wa kutisha.
UFISADI NA MAFISADI
Alisema suala la kukwapuliwa kwa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sh. bilioni 133 na mabilioni ya Tangold, ambazo zilichukuliwa na CCM kwa ajili ya kampeni za mwaka 2005, hawataacha kulizungumzia kwani ushahidi wa fedha hizo kukwapuliwa na wachache kwa manufaa yao upo wazi kabisa.
“Tunaitaka serikali kuutumia Usalama wa Taifa na Polisi kulinda rasilimali zetu zisitoreshwe nje ya nchi kama inavyofanyika kwenye sekta ya madini na wanyama, badala ya kupoteza muda mwingi kuwafuatilia Chadema,” alisema. Alidai shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa hivi karibuni nchini China, ikiwa ni mali ya kiongozi mmoja wa ngazi za juu kwenye CCM, ambaye hakumtaja kwa jina, ni ushahidi tosha kuwa ndani ya chama hicho hakuna aliye msafi, bali wanaendelea kutafuna nchi huku Watanzania wengi wakiteseka kwa umaskini wa kupindukia.
Alisema watatumia nguvu ya umma kuhakikisha fedha zilizoporwa zinarejeshwa na ndipo watatoa elimu bure kwa kila mtoto wa Kitanzania na kulipa mishahara ya walimu na watumishi wengine.
Alitumia mkutano huo kujibu hotuba ya Meya wa Manispaa ya Moshi, Michael Jaffary, aliyemtaka kuzungumzia suala la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, Mkuu wa Wilaya, Dk. Ibrahim Msengi, kuingilia kazi za Baraza la Madiwani na Mkurugenzi wa Manispaa, Benadetha Kinabo, kukataa kutekeleza maagizo ya baraza.
Alisema Sheria namba 19 ya mwaka 1999 inaeleza RC na DC ni wahamasishaji kwenye halmashauri na vyombo vyenye maamuzi ya kisheria ni Bunge kwa ibara ya 63 na halmashauri za wilaya kwa ibara ya 45 na 46 na ndiyo maana vikao vya viongozi hao ni vya mashauriano na haviwezi kuwa juu ya vikao vya kisheria.
“Baraza la Madiwani ni Bunge kwenye eneo husika na watatunga sheria zao, mna haki ya kusimamia haki za wananchi bila kuyumbishwa, kama wanaendelea kuwasumbua, niiteni nije tuwashikishe adabu kama nilivyofanya kwenye Halmashauri ya Karatu,” alitamba Dk. Slaa.
Alisema suala la Mkurugenzi kukataa kusaini kutolewa kwa Sh. milioni 216 kwa ajili ya kulipia ada ya watoto wa watu wasiojiweza wapate elimu, ni maamuzi ya madiwani na kama Mkurugenzi huyo analipinga, wamfungie nje bila kumuonea haya.
Awali, Mbunge wa Arusha Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Godbless Lema, alisema dhambi ya woga inaitafuna Manispaa hiyo na Tanzania kwa ujumla kwani kama Mkurugenzi anawasumbua wanaweza kumchukulia hatua kwa kuwa ni Katibu kwenye vikao vya madiwani na anafanya kile anachoelekezwa na Baraza linaloongozwa na Meya na theluthi ya madiwani wanatoka Chadema.
Meya Jaffary katika taarifa yake, alisema Manispaa imefanikiwa kuongeza mapato ya halmashauri hiyo kutoka Sh. bilioni 1.8 mwaka 2009/10 hadi Sh. bilioni 4.1 mwaka 2012/13 kwa kuziba mianya ya wizi iliyofanywa huko nyuma na fedha imeelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Meya huyo alimuomba Dk. Slaa, kuhakikisha suala la mamlaka za chini za serikali zinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na si kwa matakwa ya chama tawala kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo anakataa kutoa fedha hizo kwa madai kuwa siyo sera ya CCM.
Hivi karibuni, uliibuka mvutano baina ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na madiwani wa Chadema kwa madai kuwa wanaingilia utendaji wa Manispaa hiyo.
Pia madiwani hao wamekuwa wakivutana na Mkurugenzi wa Manispaa kwa madai kuwa anakaidi kutekeleza maagizo ya Baraza la Madiwani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment