NA MUHIBU SAID
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama hicho kwa ngazi zote; kuanzia msingi hadi taifa pamoja na mabaraza yake yote, utakaofanyika sambamba na operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) katika kanda 10 nchini kote Aprili hadi Desemba, mwaka huu.
Ratiba ya uchaguzi huo ni sehemu ya maamuzi kadhaa yaliyopitishwa na Baraza Kuu la Chadema katika mkutano wake maalum uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda tano, mapendekezo kuhusu maudhui na mchakato wa katiba mpya na mapendekezo ya haja ya kufanya marekebisho katika kanuni za chama na kutunga muongozo.
Ajenda nyingine ni mpango kazi, mkakati na mwendelezo wa operesheni ya M4C na bajeti ya chama kwa mwaka 2013 na mengineyo.
Maamuzi ya baraza hilo yalisomwa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.
UCHAGUZI NA M4C
Mnyika alisema uchaguzi wa misingi, matawi, majimbo na wilaya, utafanyika Aprili hadi Septemba, kupitia operesheni za M4C kwa kila kanda.
Alisema chaguzi za mikoa zitafanyika Novemba, wakati ule wa ngazi ya taifa utafanyika Desemba.
Mnyika alisema uchaguzi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) utafanyika Desemba 11 na kufuatiwa na uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) na Baraza la Wazee wa Chama hicho utakaofanyika Desemba 12.
Alisema Desemba 13 Kamati Kuu, Desemba 14 Baraza Kuu, Desemba 15 Mkutano Mkuu, Desemba 16 Baraza Kuu jipya na Desemba 17 Kamati Kuu mpya.
Pia alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa uenyekiti wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji, udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi wa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 safari hii utaanza mwaka huu.
Alisema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa juzi wa Baraza Kuu, ni pamoja na kujiwekea malengo ya kusimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kote nchini.
Mnyika alisema suala hilo litakwenda sambamba na chama kuwaruhusu wanachama wanaotaka kuwania nafasi yoyote kati ya hizo kutangaza nia mapema.
Pia Baraza Kuu limezingatia kwamba, matatizo yanayoikabili nchi kwa sasa, ikiwamo migogoro mbalimbali, ni matokeo ya sera mbovu na udhaifu wa kiuongozi wa CCM na serikali yake.
Hivyo, Mnyika alisema Chadema itaendelea kuwaongoza wananchi kuiwajibisha serikali mwaka huu, kueneza sera sahihi za Chadema na kuwaunganisha kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi zinazokuja za mwaka 2014 na 2015.
NGUVU YA UMMA
Alisema Baraza Kuu pia limesisitiza falsafa ya chama ya “nguvu ya umma” katika kuongoza utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka huu.
Pia alisema limepitisha utaratibu wa mfumo wa utendaji wa kanda kwa kuzingatia misingi ya ‘sera ya majimbo’.
Alisema katika kuonyesha kuwa wako makini na hilo, Baraza Kuu limepitisha asilimia 40 ya fedha za ruzuku ya chama kupelekwa kwenye kanda hizo kwa ajili ya kutekeleza mkakati huo.
“Chadema inakwenda kupambana na CCM kona zote. Hiyo ndiyo dawa pekee ya kuondoa matatizo nchini,” alisema Mnyika.
Alisema M4C itafanyika mfululizo ili kudhibiti nguvu, ambazo Jeshi la Polisi linaweza kujianda kuzitumia kama ilivyofanya katika operesheni zilizopita mkoani Morogoro na Iringa kujaribu kuzizuia.
PIKIPIKI M4C
Mnyika alisema ajenda kuu katika M4C itahusu katiba mpya na rasilimali za nchi na kwamba, tayari chama kimeshanunua pikipiki maalum 126 kwa ajili ya kufanikisha operesheni hiyo.
Alisema tofauti na pikipiki nyingine, ambazo zina majina ya kampuni zilikotengenezwa, pikipiki zilizonunuliwa na Chadema zina jina la M4C na zimefungwa vipaza sauti.
Mnyika alisema Baraza Kuu pia lilipokea na kuridhia taarifa ya Kamati Kuu kuhusu maoni na mapendekezo ya chama kuhusu maudhui na mchakato wa katiba mpya.
Alisema pia limezingatia kuwa katiba mpya bora ni nyezo muhimu ya ufumbuzi wa matatizo ya kiongozi na migogoro inayolikabili taifa, ikiwamo inayohusu rasilimali za nchi.
Mnyika alisema taarifa ya maamuzi ya Baraza Kuu juu ya hatua zitakazochukuliwa kuhusu maudhui na mchakato wa katiba mpya zitatolewa kwa umma.
Alisema vilevile, Baraza Kuu limepokea mapendekezo na kuridhia haja ya kufanyia marekebisho ya kanuni za chama na kutunga muongozo.
Alisema kati ya maeneo ya kanuni yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho, ni pamoja na kuweka utaratibu wa wajibu na mipaka ya mbunge wa viti maalum kuondoa migongano na wabunge wa majimbo.
Pia kuweka utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu mapema katika masuala yenye kuhitaji hatua za haraka kwa maslahi ya chama na taifa na mipaka ya wenza wa viongozi kwenye ushiriki wao katika shughuli za chama na nidhamu kuhusu muda wa mikutano.
Alisema vilevile, Baraza Kuu limeridhia kuandaliwa kwa muongozo kuhusu utaratibu wa kutangaza kusudio la kugombea nafasi za uongozi kwenye chama na katika chaguzi za kiserikali kuanzia ngazi za kitongoji, kijiji/mtaa, udiwani, ubunge na urais.
; ikiwamo maoni na
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment