MIONGONI
mwa mambo mengi yanayodhihirisha msigano baina ya taifa dogo na taifa kubwa ni
upeo wa mwangalio.
Taifa dogo litakuwa na watawala na wananchi ambao wote
wanaangalia vitovu vyao; wakijitahidi sana wataona ncha za vidole vyao vya
miguu. Taifa kubwa litakuwa na watawala, viongozi na wananchi wanaoangalia upeo
wa macho; wanaangalia makutano ya mbingu na ardhi, kisha wanainua macho na
kuangalia anga.
Taifa dogo litakuwa na watu wa kufanya mambo haraka haraka, huku
wakilipua, alimradi watimize ngwe. Mipango yao ni ya muda mfupi; wanachopanda
ni kile watakachokula ndani ya wiki tatu, kwa hiyo watapanda mchicha na bamia
na baada ya wiki nane watakuwa hawana kitu.
Watawala na viongozi wa taifa kubwa watawahimiza na kuwafundisha
watu wao (na watu wao wataelewa) kufanya mambo yao kwa mipango ya muda mrefu,
mipango ya kimkakati; mazao yao yatakuwa ya kudumu na yaliyofanyiwa utafiti wa
muda mrefu ili kuwa na uhakika wa tija katika mavuno. Mipango yao itakuwa ya
kuangalia, si tu faida ya leo na kesho na kesho kutwa, bali faida watakazokuta
watoto, wajukuu, vitukuu na vilembwe, hadi miaka milioni ijayo.
Tukiangalia mataifa ya Uropa, tunalazimika kukubali kwamba haya
ni matafia makubwa, na pia tunakubali kwamba yamekuwa mataifa makubwa kwa muda
mrefu, ingawaje yapo baadhi yake yaliyopungukiwa na ukubwa yaliyokuwa nao huko
nyuma. Hatuna budi kuona haya kwa kuona ni nini walichofanya binadamu wenzetu
na kukilinganisha na upuuzi tunaofanya sisi, kana kwamba sisi si binadamu
kamili.
Tunaona kwamba mababu na mabibi zao waliweza kuwaza kwa masafa
marefu na kujenga juu ya msingi wa mawazo hayo, na leo bado tunayaona matunda
ya mawazo hayo kila tunaponagalia majumba yaliyodumu karne kadhaa na bado ni
imara na kila tunapoangalia barabara pana na imara zilizojengwa karne zote hizo
zilizopita na leo bado zimesimama imara.
Tunaangalia jinsi wanavyohangaika kuboresha huduma zao za elimu,
afya na huduma nyingine za kijamii (ambazo tayari ni nzuri) wakati sisi tukiua
hata zile tulizokuwa nazo.
Tunaposafiri Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na
kwingineko tunaona ushahidi wa mataifa makubwa yanavyofikiri, lakini kwa sababu
tumejifunga katika udogo wetu mpendwa hatupati funzo lo lote linaloweza
kutusaidia kufikiri kikubwa pindi tunaporejea nyumbani. Sana sana tutapoteza
muda wetu na fedha kununua vijitakataka na upuuzi mtupu ili kuwakoga wenzetu,
kama vile kununua masuti ghali ambayo wala hatujui yanavyovaliwa.
Taifa kubwa litakuwa na watawala na viongozi wanaotaka kuona
maendeleo ya wakati wote, na ambao hawakubali kitu cha leo kiwe duni kuliko cha
jana. Kwao, maendeleo ni ile hali inayotokea wakati kitu cha leo ni bora kuliko
cha jana, na cha kesho kitakuwa bora kuliko cha leo. Daima mwendo ni kuelekea
mbele.
Baba atakuwa na elimu bora kuliko babu, lakini mjukuu atakuwa na
elimu bora kuliko baba. Baba atakuwa na siha ya kuridhisha kuliko babu, lakini
afya ya mjukuu itakuwa ni bora kuliko ya baba; hata ukubwa na urefu wa kimwili
unatakiwa uende ukiwa bora zaidi kwa kila kizazi kipya kijacho. Jamii inayozaa
watoto wenye maumbile madogo kuliko wazazi wao ina tatizo.
Sisi, katika udogo wetu, tunaenenda vipi?
Katikati ya miaka ya 1970 serikali iliamua kujenga barabara ya
njia nne kutoka Ubungo hadi Bandarini jijini Dar es Salaam. Hiyo ndiyo leo
inaitwa Nelson Mandela, iliyotufungulia maeneo kama Riverside na Tabata.
Ndiyo hiyo pia barabara kuu inayohudumia bidhaa nyingi
zinazosafirishwa kwenda hadi mipakani mwetu (zikisafirishwa kwenda Zambia,
Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda) hivyo ni kitegauchumi muhimu kwa nchi yetu.
Lakini miaka 30 baadaye tunachofanya ni kwenda kuiparura
barabara ile ile kwa upana ule ule, na kuipaka rangi nyeusi, huku tukishuhudia
jinsi msongamano wa magari unavyozidi kughasi, kukera na kusumbua. Huu ni udogo
wa mawazo unautusmbua, ingawaje kila siku tunapata kauli za kujisifia kwa
ujenzi wa ajabu tulioufanya.
Tumeliacha Jiji la Dar es Salaam lioze katika sehemu nyingi
katikati kabisa ya jiji. Iko mitaa inayotia kinyaa ukipita, kwa sababu ujenzi
unafanywa holela, takataka zimezagaa kila mahali, na maji yametuwana yakiwa
yamechanganyika na kila aina ya uchafu wa kuchefua roho. Inaelekea, pamoja na
maneno yote yaliyosemwa kuhusu tatizo hili, tumeshindwa kushughulikia suala la
plastiki ambazo sasa zimezagaa kila mahali, zikichafua mazingira na kuumiza
ardhi yetu.
Watawala na watu wanaoangalia mbali labda wangeamua kuvunja
sehemu kubwa ya jiji hili na kulijenga upya. Wangetafuta pia namna ya kulifanya
lipumue kwa kusambaza huduma zinazokimbiliwa katikati ya jiji na kuzipeleka
katika viunga vya mji, ambavyo vingefikika kwa urahisi kwa kujenga barabara za
upana wa mita hadi 60 na zaidi.
Hapana, sisi tunataka tubanane hapa hapa, katikati ya jiji hili
chafu linalonuka maji-taka. Tumeendelea kuishi katika mazingira finyu, machafu
na yaliyojaa ndwele kama vile kipindupindu hadi sasa tunaelekea kukubali kwamba
hivyo ndivyo tunavyotakiwa kuishi.
Rai yangu hapa ni kwamba udogo tulionao ni udogo wa kujivisha
sisi wenyewe, si udogo wa kupewa na Mungu. Mataifa yaliyodhihirisha ukubwa,
kadhalika, hayakuvishwa na Mungu bali yalijivisha ukubwa huo yenyewe, kwa
kufikiri kikubwa na kutenda kikubwa.
Ukubwa unaohitajika ili tuondokane na udhalili huu tunao ndani
yetu; tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta, kuubaini, kuuibua na kuutumia ili na
sisi tuweze kutamba mbele ya mataifa mengine kama taifa kubwa.
Niseme ukweli: Inaudhi kuendelea kuwa mdogo wakati ukijua kwamba
uwezo wa kuwa mkubwa unao ila hujui namna ya kuutambua na kuutumia.
source: Raia Mwema: Jenerali
Ulimwengu
No comments:
Post a Comment