NA ROMANA MALLYA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Dk. Wilbroad Slaa, ameibua tuhuma dhidi ya serikali akidai ina mkakati wa kudhoofisha upinzani ili kuhujumu uchaguzi wa 2015.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye mkutano wa wanafunzi wa vyuo vikuu Wanachadema alisema amepata taarifa za kuthibitika kuwa, serikali inaagiza mtambo mwingine mwaka ujao kwa gharama ya ya Dola 850,000 ( Sh.bilioni 1.4 ) ili kudhoofisha upinzani.
Katibu huyo alisema mtambo huo pamoja na kazi nyingine utakuwa unapata taarifa mbalimbali za kimawasiliano kudhibiti upinzani.
Alisema baada ya serikali kushindwa kukihujumu chama hicho kupitia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) ilizozibaini awali , ina mkakati wa kuagiza mtambo huo.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, baada ya kupata taarifa hizo na kampuni ambayo itaiuzia serikali mtambo huo, alimwandikia ‘bwana mkubwa’ (ambaye hakumtaja) kuhusu mpango huo.
“Nilimweleza kuwa nimepata anuani yake hiyo na kwamba na mimi nimetuma maombi.
“Ninasubiri nione kati yangu na serikali nani atauziwa mtambo huu, walijaribu awali kuhusu SMS lakini walishindwa, naona wanakuja na mbinu mpya, ninachotaka kuwaeleza ni kwamba Chadema kipo imara na tutasimamia hili, ” alisema.
Akitaja njama nyingine alisema anazo habari kutoka Usalama wa Taifa kuwa serikali itatumia mitandao ya kijamii kuwaandaa vijana na wananchi kuishughulikia Chadema.
“Kwa bahati mbaya vijana wangu mnatumika, katika hili Usalama wa Taifa umetumia mamilioni ya pesa kutushughulikia,”alisema.
Pia alisema ana taarifa kuwa chombo hicho kinashirikiana na kigogo wa CCM Bara (jina tunalo) kuandaa mkanda wa video kuoonyesha Chadema ikipanga mauaji.
AKANUSHA KUJIKOPESHA
Alikanusha madai ya kujikopesha Sh milioni 140 za chama na kueleza kuwa alijikopesha Sh. Milioni 20 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kusema ni utaratibu wa kawaida.
Alisema kashfaya mkopo huo uliotolewa na kiongozi wa Umoja wa Vijana ililenga kudhoofisha jitihada za kuikosoa serikali kupitia kauli mbalimbali wanazotoa.
MAANDAMANO YANA MAFANIKIO
Alisema maandamano ya wadau tofauti kama wanafunzi,wananchi ni mafanikio ya Chadema kupitia operesheni nyingi zilizofanyika nchi nzima kwa lengo la kutoa elimu kwa umma ili kutambua haki zake .
Dk. Slaa aliunga mkono maandamano hayo na kueleza kuwa ni hatua muhimu ya kudai haki.
“Wapo wanaosema maandamano yanachochewa na Chadema, hawa ni mbumbumbu hawajui kama wananchi sasa hivi wanajua haki zao, maandamano ya IFM, IGP na Kova walipaswa kujiuzulu kwa kutumia mabomu kwa watu waliokuwa wakitaka ulinzi wao,” alisema.
MAUAJI YA POLISI
Katibu Mkuu wa Chadema alisema ana takwimu za vifo vya raia waliouawa na polisi na kutaka kuwepo na tume ya mahakama kuchunguza na siyo Jeshi la Polisi kama inavyofanyika sasa.
Alisema Chadema imewasilisha taarifa za vifo vilisababishwa na polisi kwenye mikutano yake kwenye vyombo vya kimataifa ili vilifanyie kazi suala hilo.
MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA
Dk. Slaa alisema suala hilo halitafumbia macho na kutaka CCM ieleze imefanya nini kutekeleza ahadi hiyo . “Tutaikimbiza mchakamchaka ili waweze kuyatekeleza haya” alisema na kuongeza kuwa watafuatilia pia suala la kutekeleza ahadi ya elimu bure kabla ya mwaka 2015.
Alikumbusha kua elimu haiwezi kukua kwa kupunguza alama za mitihani kama serikali ilivyofanya.
Alisema asilimia 3.0 ya matajiri wanamiliki asilimia 97 ya rasilimali za taifa wakati Watanzania wengi wanakula mlo mmoja na wanafunzi wanakosa karo.
MCHAKATO WA KATIBA
Katibu huyo alisema Chadema hakijalala na kwamba kinajua uozo wote unaoendelea na kwamba wanasubiri rasimu ya katiba ikitoka ndipo waanze kupiga kelele.
“Mwaka jana tulikubaliana na Rais tufanye marekebisho mawili, ya kwanza muda wake umepita, marekebisho ya pili muda unaishia,” alisema.
HECHI ASEMA WAKO TAYARI KUFA
Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chadema , John Heche, kwa upande wake alisema wataendelea kulipigania taifa hata kama italazimu kupoteza uhai Hechi ambaye ni mlezi wa wanafunzi wanachama wa Chadema nchini (CHASO) aliwaambia wanachama hao kuwa Chadema itaunda dola mwaka 2015.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Mimi nadhani kwa wanaomsikia Dk. Slaa watajiuliza mambo mengi sana, lakini kama kweli ana uhakika kwamba serikali itaagiza mtambo wa mtamba wa gharama kubwa kiasi hicho cha fedha , ni kwa nini asiitaje hiyo kampuni inayihusika kwa sababu amesema hata yeye ameshaagiza mtambo huo iliaone nani kati yake na serikali atakayeuziwa
ReplyDelete