NI muda
mrefu sasa nimekuwa na mtazamo kuwa baada ya kuondokana na mfumo wa chama
kushika hatamu, kuna mchakato umekuwa ukiandelezwa na wajanja kadhaa katika
nchi yetu wenye nia ya kujenga mfumo mpya ambao ninaita MFUMO FISADI.
Matokeo
na mchakato wa uchaguzi wa ndani unaolekea kufikia tamati katika Chama cha
Mapinduzi una kila dalili za kufikia hatua ya juu ya mchakato huu wa ujenzi wa
MFUMO FISADI kwa kufanikisha kusimika rasmi uhodhi wa chama hicho mikononi mwa
vinara na makuwadi ama mawakala wa mfumo huo na hivyo kuwezesha kuhatamisha
mfumo huo katika uongozi wa taifa letu.
MFUMO
FISADI ni mfumo wenye nia ya kurasimisha na kuhalalisha mambo ambayo ni kunyume
kabisa na misingi ya utaifa wetu kama ambavyo ilijengwa na kuachwa na Baba wa
taifa letu Mwalimu Nyerere na wafuasi wake adhimu kuanzia alipokuwa TANU na
baadaye CCM.
Ni
mfumo ambao umekuwa ukijengwa ama kujengeka katika sura mbalimbali kama vile
kujenga mfumo wa soko huria, kuendana na uhalisia na usasa wa kukubali kuwa
hatuna ujanja isipokuwa kukumbatia misingi ya kibepari, umuhimu wa kujenga
tabaka la kati, siasa za ushindani na kadhalika.
Wengi
wetu kama si wote kwa namna moja ama nyingine tumeshiriki katika harakati hizi
za kujenga MFUMO FISADI. Ushiriki wetu upo katika ama katika kupanga ama kutekeleza
mikakati yake kwa kujua ama kutokujua, kuhalalisha mambo yake kwa kutetea ama
kuhalalisha chembechembe za ufisadi, kuwawezesha kiuchumi na kisiasa wale
vinara na mawakala wa ujenzi wa MFUMO FISADI na vinginevyo.
Naomba
niweke wazi kabla sijaingia ndani katika kuchambua na kuelezea mtazamo wangu
kuhusu hili la ujenzi wa MFUMO FISADI na hatari tunayokumbana nayo sasa ambapo
yawezekana tukawa katika hatua za mwisho katika kuusimika mfumo huu katika
hatamu za nchi yetu.
MFUMO
FISADI hauna chama wala wanachama. MFUMO FISADI hauna dini hii ama ile. MFUMO
FISADI hauna kabila hili ama lile. MFUMO FISADI hauna rika hili ama lile. MFUMO
FISADI hauna sekta moja ama nyingine. MFUMO FISADI hauna tabaka hili wala lile.
MFUMO FISADI unaratibiwa, kujengwa na kulindwa na vyama vyote, sekta zote, dini
zote, makabila yote, marika yote,matabaka yote na makundi mengine.
Kwa leo
nitaongelea mfumo huu haramu katika muktadha wa kinachoendelea ndani ya Chama
Cha Mapinduzi ambacho hivi karibuni tumekuwa tukisikia na kuona mengi yakitokea
na kusemwa katika mchakato wa chaguzi za ndani za chama hicho. Chama ambacho
hadi sasa ndio chama tawala.
Moja ya
kitu ambacho kimegeuka kama ndio kioo cha kupima mafanikio ama athari za
uchaguzi huu kimekuwa ni jinsi gani nguvu ya pesa imeweza kuonyesha makucha
yake katika uchaguzi huu.
Wengi
tumekuwa tukiuangalia, kuupima na kuchanganua uchaguzi huu kama ni kioo cha
kupima nani atakuwa mgombea na wengine hata kuamini kuwa ndiye atakayekuwa Rais
ajaye.
Wengi
tumekuwa tukiuangalia uchaguzi huu kama ishara ya ama kukirudisha chama katika
mstari ama kukiacha kiteketee kwa kukitunuku rasmi kwa wale wanaonekana ama
kujipambanua kama vinara na makuwadi wakuu wa ujenzi wa MFUMO FISADI.
Kwa
kiasi fulani kuna ukweli wake, kwani kuna wengi ama wamegombea, wamechagua ama
wamechaguliwa kutokana na kushawishiwa, kuwezeshwa ama kuahidiwa neema na ama
wapambe au vigogo wenye kuamini kuwa wakishashinda ndani ya CCM basi Urais wa
2015 ni wao na kwamba ulaji utakaokuja nao utakuwa wao wa kugawana.
Hali
hii inasikitisha na kutisha sana kwa mustakabali wa taifa letu. Inatia uchungu
na kukatisha tamaa kwa mzalendo yeyote yule awe mwanachama wa chama hiki na
hata yule ambaye sio mwanachama wake lakini anatambua umuhimu wa chama hiki kwa
taifa letu haswa wakati huu wa miparaganyiko lukuki.
Harakati
za kujenga MFUMO FISADI zimelenga katika kuwaangusha na kuwakatisha tamaa wale
wote waliokiunga mkono chama cha CCM kutokana na Misingi yake imara ya kuweka
mbele UTU wetu na kukiaacha chama mikononi mwa wale walioweka mbele IMANI YA
NGUVU ZA FEDHA.
Wakati
mwengine huwa najenga fikra kuwa yawezekana nguvu za harakati hizi za vinara na
makuwadi wa ujenzi wa MFUMO FISADI ndani ya CCM zinatokana na nia ya dhati ya
kukiondoa madarakani chama hiki. Kwao wao na wakubwa zao wanakiona chama hiki
chenye misingi na historia adhimu ya utu, usawa na ukombozi wa ndani na nje ya
mipaka yetu ni kama kizingiti dhidi ya nia yao ya kuhatamisha mfumo fisadi kwa
jina la Ubepari.
Yawezekana,
na inajionyesha wazi kuwa vinara na mawakala wa MFUMO FISADI huu ambao wengi
tayari wana mahusiano maalum na vyama mbadala katika kinyang’anyiro cha utawala
wa nchi, nia yao hasa sio kuhodhi madaraka ya chama hiki bali kukivunjilia
mbali na baadaye kutumia vyama vyenye misingi ya kibepari ambavyo sasa vimevaa
ngozi za hisia za kijamaa katika mpango kabambe wa kusimika rasmi MFUMO FISADI
katika hatamu za utawala wa taifa letu.
Na hapa
ndipo ninaona kuna tatizo kuu ya jinsi baadhi ya wanaojitambulisha kama
wapambanaji dhidi ya ujenzi wa MFUMO FISADI wanakosea katika mapambano yao.
Wengi wa wapambanji hawa, wa ndani na nje ya CCM, wamekuwa wakijikita zaidi
katika mkakati wa kupanga safu za uongozi wa chama dhidi ya washindani wao
ndani ya chama kama maandalizi ya mpambano mkuu ujao wa kumpata mgombea wa
Urais kupitia chama chao.
Kwa
kuweka mbele ushindani huu unaotegemea sana wa nguvu za fedha na sio imani ya
wanachama kwa chama na viongozi wao kundi hili la wana CCM limeweza kujenga
mazingira ambayo maadui ama washindani wao katika sakata la uhodhi wa chama
wamepata urahisi wa kipropaganda na kimkakati.
Matokeo
yake hata hao wenye kujipambanua kama CCM-Misingi ambao wakati fulani
walijulikana kama MTANDAO MATUMAINI wanalazimika katika kuamini katika nguvu za
fedha ili kupambana na washindani wao wa kundi la MTANDAO MASLAHI ambao kwao
wao nguvu za fedha ndio msingi mkuu wa mafanikio yoyote.
Na hapa
ndipo tunapokuja katika tatizo lingine katika hizi juhudi za kupambana na
harakati za MFUMO FISADI ambazo kama mambo hayajabadilika sasa na sio baadaye
basi ni wazi zitafanikiwa katika kushika hatamu za taifa letu.
Kitendo
cha wana CCM wengine na hasa wale ninaowaita CCM ASILIA, yaani wana CCM wenye
kuamini katika misingi ya chama na utaifa wetu, kuwaachia “WANAMTANDAO”
kupambana wenyewe kwa wenyewe ama kwa kudhania kuwa hayo ni ya wanamtandao
wenyewe kumalizana na kama vile hayana athari kwao ni kosa kubwa linaloendelea
ambalo nalo limewezesha ujenzi wa MFUMO FISADI na uwezekano wa mfumo huo
kushika hatamu.
Mapambano
ya dhati ya kukikomboa chama hiki ambacho kwa mtazamo wangu ni kuwa hadi sasa
kimekosa mbadala makini wa kukibadili na kutegemea ukombozi wa kweli
hayatafanikiwa kwa kuwaacha wanamtandao wenyewe kwa wenyewe kuhodhi uwanda wa
mapambano.
Zaidi
kuna uwezekano mkubwa wa hao tunaoamini kuwa wanapambana dhidi ya wingu la
vinara na mawakala wa MFUMO FISADI kutoka katika kundi la MTANDAO MATUMAINI
wakaishia kukubali kushindwa na kujiunga na timu ya ushindi ya wenzao.
Tukumbuke kuwa hawa kwa pamoja walishirikiana katika kuendesha mapinduzi ya
ndani ya chama hapo kabla na hivyo kuweka msingi wa ujenzi wa mfumo fisadi
ambao wenzao wa MTANDAO MASLAHI wameamua kuubeba hadi watakapofanikiwa
kuuhatamisha katika siasa na uongozi wan chi yetu.
Mapambano
ya dhati na yanayoweza kuirudisha CCM katika mstari na kukilinda dhidi ya nia
mbaya za vinara na wapambe wa MFUMO FISADI ni yale yatakayojikita katika ajenda
za DIRA, MISINGI na ITIKADI ya chama na sio vinginevyo.
Na hapa
ndipo wana CCM, Wazee kwa Vijana wenye kuamini katika umuhimu wa dira, misingi
na itikadi za chama hicho na taifa letu wanakuwa na umuhimu wake kwani ni wao
tu na sio wengineo ndio watakaoweza kubadili mwenendo wa mpambano huu na hatima
ya chama chao na taifa letu.
Ndani
ya kiwingu cha habari mbaya za ushindi wa nguvu za fedha katika chaguzi hizi,
pia kuna habari njema kiasi. Tofauti na chaguzi zilizopita, katika chaguzi hizi
wapo baadhi ya wagombea waliofanikiwa kushinda hivi sasa ambao hapo nyuma
walishindwa katika kila chaguzi walizokuwa wakishiriki kutokana na “ushamba”
wao wa kutokuamini katika nguvu za fedha na kujikita katika kampeni za misingi
na tamaduni za chama.
Ushindi
wa hawa ambao wanaweza kuwa kidogo lakini wenye za kimahitaji bado unaonyesha
matumaini na uwezekano wa nguvu za MISINGI ndani ya chama hiki na kutoa ujumbe
kuwa hii kansa ya nguvu za fedha haijakikumba chama kizima. Hivyo endapo wengi
zaidi wa aina hiyo wakiamua kusimama na kupambana, bado kuna uwezekano wa
mpambano wa kuzuia uhodhi na hatimaye uwezekano wa Ufisadi kushika hatamu
kufanikiwa kwa manufaa ya chama chao na taifa letu.
Ni
mapambano yaliyojikita katika nguvu za misingi tu na sio nguvu za fedha ndio
yatakayotuepusha na tishio la UFISADI KUSHIKA HATAMU na madhara yake mengineo.
Tishio ambalo kuna uwezekano mkubwa wa kurasimishwa rasmi hivi karibuni
tunapoelekea katika tamati ya chaguzi za ndani za CCM. Na kama ikishindikana
kuzuia tishio hilo sasa basi wote kwa pamoja tujiandae na hasira za wapiga kura
ambao wanaonyesha kila dalili za kukumbatia fikra ya “bora mbadala na liwalo na
liwe” kama fimbo yao kwa wasaliti wa imani yao waliyoitunuku kwa miaka mingi
ndani ya CCM.
SOURCE: RAIA MWEMA: Omar
Ilyas
No comments:
Post a Comment