WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, January 14, 2013

MAFANIKIO ZAIDI KUPATIKANA ZANZIBAR ENDAPO WANANCHI WATADUMISHA MSHIKAMANO


14 edae4

Na: Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar    

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amesema mafanikio yote yaliyopatikana Zanzibar katika kipindi cha miaka 49 na miaka ijayo kwenye nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa msingi wake mkubwa ni Mapinduzi ya Januari 1964. Amesema mafanikio zaidi yatapatikana iwapo Wananchi wataendelea kudumisha mshikamano na amani iliyopo Zanzibar pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuiletea maendeleo Zanzibar.

 Rais Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akilihutubia Taifa katika kilele cha sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar kilichofanyika Uwanja wa Amani mjini Zanzibar.
 Amesema ushirikaiano wa Serikali na wananchi umeipatia Zanzibar mafanikio mazuri katika kuimarisha uchumi wake ambao mwenendo wake umeliwezesha pato la Taifa kufikia Shilingi Bilioni 1,198 mwaka 2012 kutoka Bilioni 946 mwaka 2011.
 Amefahamisha kuwa mafanikio hayo yametokana na kukua kwa Sekta ya Uvuvi, Biashara na ujenzi wa Mahoteli na Mikahawa jambo ambalo limesaidia Serikali kupunguza mfumko wa bei kutoka asilimia 20 mwaka 2011 hadi asilimia 4.2 mwaka 2012.
 Kuhusu Kilimo Rais Shein amesema Serikali yake inaendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kukiendeleza kilimo ikiwemo kuimarisha Miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha kuwa Hekta 8,521 za Unguja na Pemba zinatumika kwa ajili ya kilimo hicho.
 Aidha ameongeza kuwa Serkali inaendelea na azma yake ya kulinda hadhi ya zao la Karafuu ambapo mkakati wa kupatikana kwa Utambulisho maalum wa Karafuu za Zanzibar (Branding) upo katika hatua nzuri.
 Amewahimiza Wakulima kupanda Mikarafuu kwa wingi na kuyatunza mashamba yao na kuachana na tabia ya kuuza Karafuu kwa njia ya magendo.
 Kuhusu maslahi ya Wafanyakazi Dkt. Shein amesema Serikali inaendelea kuimarisha maslahi bora kwa watumishi wote na kuimarisha mishara na stahili nyingine za wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu ili kuendesha vyema maisha yao.
 Kuhusu Muungano Dkt. Shein amewahakikishia wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza Muungano huo na kuwatumikia wananchi wote.
 Akitoa salamu zake Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe hizo ambaye pia Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd amesema jumla ya Miradi ya kimaendeleo 53 yenye thamani ya Shilingi 97.4 Bilion imezinduliwa katika shamra shamra za kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Awali Rais Shein alipokea Salamu za Rais na Gwaride maalum kutoka Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja Vikosi vya SMZ, Maandamano ya Wananchi na Taasisi mbalimbali za Serikali ambapo pia Jumla ya Mizinga 21 ilipigwa kuhanikiza sherehe hizo.
 Sherehe hizo zilihudhuriwa na Viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete,Makamo wa Rais Dkt. Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad,Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd, Marais wastaafu, Mawaziri, Mabalozi, Viongozi mbalimbali na Wananchi wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment