Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa mtindo wa kufanya fujo na kusambabisha uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha dini nchini, ni biashara inayolipa sana na ndiyo maana wakereketwa wa kufanya fujo hizo hawaishi.
Aidha, Rais Kikwete amesema ni jambo la kushangaza mno kuwa zipo jitihada kubwa za kutumia dini kuinyumbisha nchi kwa sababu ya kisingizio kwamba Tanzania imekuwa na amani kwa muda mrefu sana.Hata hivyo, amesema Serikali yake haitayumba wala kusita kupambana ipasavyo na wafanya fujo za kidini kwa sababu kama kuna jambo moja linaloweza kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania, ni fujo za kidini na kuwa jambo hilo linahitaji kuchukuliwa maamuzi na hatua za busara.Rais Kikwete alizungumzia fujo za kidini alipowasilisha utetezi wa kuvutia na maelezo ya kina kuhusu Ripoti ya Mchakato wa Nchi za Afrika Kujithamini Zenyewe katika Nyanja za Demokrasia, Utawala Bora na Uchumi (APRM) iliyowasilishwa kwa wakuu wa nchi wanachama wa APRM kwenye mkutano uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia usiku wa Januari 26, mwaka huu.Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema Rais Kikwete aliwaambia wakuu wenzake wa nchi kwenye mkutano huo ambako Ripoti za APRM za Tanzania na Zambia ziliwasilishwa kuwa: “Nakaribisha kwa mikono miwili pendekezo la APRM kuwa serikali isimamie kwa uangalifu tofauti za kidini nchini. Kama mnavyojua, Tanzania imekuwa na amani na utulivu kwa sababu tumekuwa na bahati kutokuwa na ugomvi wa kikabila, kidini ama yale ya kutokana na rangi za watu. Hali hii inatokana na ukweli kuwa tumetunga na kuwa na sera zisizokuwa za kibaguzi kwa wananchi wetu kwa misingi ya kabila, dini, rangi ama sehemu anakotoka Mtanzania. Ni sera nzuri na tutazidumisha.”Aliongeza: “Uzuri kuhusu dini katika Tanzania ni kwamba tunaamini na kudumisha uhuru wa kuabudu kwa kila mtu. Serikali haina dini. Lakini tunajua fika kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na wanasiasa na viongozi wa dini wenye malengo ya kuchochea fujo za kidini. Hatutayumba wala kusita kupambana ipasavyo na watu wa namna hiyo. Pale ambako uchochezi wa kidini unafikia kiwango cha kuhatarisha amani ya nchi ama uvunjifu wa amani na sheria, dola ina haki ya kuingilia kati.”Rais Kikwete pia alitumia muda mwingi kuelezea jinsi Serikali ya Tanzania inavyoheshimu na kudumisha haki za binadamu na pia alisema amefurahishwa kuwa Ripoti ya APRM imeelezea hatua ambazo Tanzania imekuwa ikichukua kustawisha na kuendeleza haki za binadamu katika miaka 50 ya uhuru wake.Alitoa mifano ya jinsi Tanzania inavyodumisha haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa kipengele cha kulinda haki za wananchi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1994.
No comments:
Post a Comment