NA SOMOE NG`ITU
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba wameanza vibaya mechi zao za kirafiki nchini Oman baada ya kukubali kichapo cha goli 1-0 kutoka wa timu ya taifa ya wachezaji waliyoshiriki Olimpiki ya Oman katika mechi yao iliyofanyika jana mchana jijini Muscat.
Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Talib Hilal, aliiambia NIPASHE kutokea Oman jana kuwa katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo iliyochezwa mchana lakini hali ya hewa ikiwa ni baridi, matokeo yalibaki kuwa 0-0. Wenyeji walipata goli lao katika kipindi cha pili.
"Tumepoteza mechi lakini vijana wamecheza vizuri... wachezaji wa U-20 wa Oman wamejitahidi sana na ni timu inayoonekana kuwa na mafanikio katika siku zijazo," alisema Hilal ambaye ni mmoja wa wadau waliosaidia maandalizi ya kambi ya Simba huko Oman.
Kocha wa Simba, Mfaransa, Patrick Liewig, aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi hiyo kuwa ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na kwamba mchezo huo ulikuwa wa kushambuliana kwa zamu.
Alisema kuwa kila timu ilitengeneza nafasi mbalimbali za kufunga lakini Simba haikuwa na bahati ya kufunga na hiyo ndiyo soka ilivyo.
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, ndiye aliyekuwa langoni huku baadhi ya nyota walioanza katika kipindi cha kwanza wakiwa ni pamoja na Paul Ngalema, Shomari Kapombe, Komalbil Keita, Haruna Moshi 'Boban', Mwinyi Kazimoto na Ramadhan Singano 'Messi'.
Mabingwa hao watetezi watashuka tena dimbani kesho kuivaa timu ya taifa ya jeshi la Oman na Jumapili itacheza mechi nyingine na itarejea jijini Dar es Salaam Jumatano ya Januari 23 kuanza mzunguko wa pili wa Ligi ya Tanzania Bara.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment