Ndugu zangu,
Katika dunia hii kila jambo
hutanguliwa na ishara. Nimepata kuandika, kuwa Afrika mvua hainyeshi
ghafla, utaziona ishara za mawingu.
Na nchi nayo ni hivyo hivyo, ishara za
nchi inayoelekea kubaya huonekana mapema. Wahenga walituambia, kuwa
ukiona zinduna na ambali iko nyuma. Zinduna ni mti na ambali ni harufu
itokanayo na mzinduna.
Naingiwa na mashaka juu ya kuongezeka kwenye jamii kwa
kauli zenye kuashiria shari zaidi
kuliko maridhiano. Na wananchi hawako katikati ya hili, bali baadhi ya
wanasiasa na wakati mwingine viongozi wa dini.
Ukweli Watanzania walio wengi
hawajachoka kuishi kwa amani, bali, kuna baadhi ya wanasiasa na hata
viongozi wa dini, kwa kutanguliza maslahi yao, wanahangaika kupandikiza
mbegu za chuki miongoni mwa Watanzania. Kwamba Watanzania wabaguane kwa
misingi ya udini, siasa na hata ukabila.
Juzi hapa nimeandika makala kuzungumzia hatari ninayoiona katika hili la vyama
vya siasa kuanzisha vikosi ama vikundi vya ulinzi. Na ukweli huko nyuma
niliandika juu ya hatari hii katika makala zaidi ya mbili, ni kuanzia
mwaka 2001 pale CUF na CCM Zanzibar walipokuwa kwenye msuguano mkubwa.
Nikaandika tena baada ya Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki pale CCM na
Chadema walipokwaruzana.
Na hapa nitarejea moja ya mazungumzo
muhimu ya kihistoria kupata bahati ya kuyafanya; ilikuwa ni jioni ya
Januari 24, 2012 pale nilipokutana na Marehemu Mama Mosi Tambwe (
Pichani) nyumbani kwake Tabora Mjini.
Mosi Tambwe aliingia TANU akiwa na
miaka 18. Ni moja wa wanawake mahiri sana kisiasa wa enzi hizo. Mosi
Tambwe alinisimulia, kuwa alianzia kwenye TANU Bantu Group, hiki
kilikuwa ni kikundi cha vijana ndani ya TANU ambacho baadae kikawa TANU
Youth League.
Kwa kirefu kabisa Mosi Tambwe
aliniambia majukumu yao kama vijana kwa wakati huo. Ni wakati nchi
ikiwa chini ya mkoloni. Akabielezea pia majukumu hayo yalivyobadilika
baada ya uhuru. Enzi hizo vijana walikuwa wakiandaliwa kupitia TANU
Youth League ili waje kuwa makada wa chama, hivyo basi, viongozi wa
wananchi walionolewa vema. Walijengewa uwezo wa kujenga hoja.
Ni enzi hizo, baada ya kutoka
Chipukizi, hatua iliyofuata ni Tanu Youth League. Wengine wakaenda JKT
na hata Jeshini. Azma kubwa ilikuwa kujenga Uzalendo na Umoja wa
Kitaifa.
Tumekosea wapi?
Jibu; ni pale, kwa shinikizo la
mabadiliko ya dunia , na kwa shingo upande, Chama tawala kiliporidhia
kuanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. CCM ikasahau kuratibu
mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yalipaswa yaendane na mabadiliko
hayo ya kimfumo.
Kimsingi, hali tuliyo nayo sasa ya kuchanganyikiwa hata kwenye hili la
vyama kuunda vikosi au la, inatokana na makosa makubwa, kama taifa,
tuliyoyafanya mwaka 1992. Maana, ‘ Green Guards’ katika mfumo wa
Chama kimoja haikuwa tatizo.
Nimeandika mara kadhaa, kuwa historia
ni mwalimu mzuri, lakini, wakati ni mwalimu mzuri pia. Tujifunze
kutokana na mabadiliko ya wakati. Katika wakati tulio nao sasa, vyama
vya siasa havipaswi kujiundia vikundi vya ulinzi vyenye kupata hata
mafunzo ya kijeshi. Ni ujasiri, kama viongozi wa sasa watazipa mgongo
fikra hizi za kizamani na kuendana na mabadiliko ya wakati.
Tufanye nini?
Kama ningeombwa ushauri hii leo, basi,
ningevishauri vyama vya siasa, kuwa kwa haraka sana, viachane na
harakati za kuunda vikosi au vikundi vya ulinzi. Jukumu hilo liachiwe
vyombo vya usalama, hususan jeshi la polisi, na hata makampuni ya
ulinzi yenye kutambulika kisheria.
Na vile vilivyopo vivunjwe. Maana,
vikundi hivi vya ulinzi ambavyo kimsingi ni vikundi vya wanamgambo wa
vyama ni maafa tunayoyaandaa wenyewe. Kama hatutanguliza busara na
hekima, basi, itakuwa ni suala la wakati tu kabla hatujajikuta kwenye
dimbwi la maafa makubwa. Tumeshaziona ishara.
Majuzi hapa nilikuwa Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam kufuatilia kongamano la Amani ya Nchi yetu kwa miaka 50
ijayo. Kwa masikitiko makubwa, ukumbi ule wa Nkrumah haukujaa vijana.
Kwa vyama vya siasa, badala ya kutumia
muda na rasilimali zao kufyeka mapori ya kuwaweka vijana kwenye ‘
makambi ya ukakamavu’, umefika wakati sasa wa kubadilika, kuachana na
fikra hizo za kijima zenye kuturudisha nyuma miaka 50.
Huu ni wakati wa kuwajengea vijana wa
vyama ‘ ukakamavu wa akili’. Na mahali kama pale Nkrumah Hall ndipo
vijana wa vyama walipaswa wahamasishwe waende wakanoe akili zao. Waende
wakajifunze kujenga na kubomoa hoja za wengine kwa nguvu za hoja na si
hoja za nguvu.
Zimepita, zama za ‘ Umkhoto we Sizwe’. Hizi ni zama za ‘ Umkhoto we Mitwe’- Ni mapambano ya kutumia vichwa kwa maana ya akili.
Naam, ukiona zinduna na ambali iko nyuma.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment