- WASOMI WASEMA SULUHU HAIPATIKANI KWA MTUTU
- WASEMA RAIS AMETUMIA LUGHA YA KIDIPLOMASIA
Rachel
Balama na Goodluck Hongo
WASOMI na
wanasiasa nchini wameunga mkono msimamo wa Tanzania uliotolewa na Rais Jakaya
Kikwete kuhusiana na chokochoko zinazoanzishwa na Rwanda na wamemtaka Rais wa nchi
hiyo, Paul Kagame, kukaa meza ya mazungumzo na waasi wa nchi hiyo walioko
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani amani haiwezi kutafutwa kwa njia
ya mtutu wa bunduki.
Akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu jana Mhadhiri wa Chuo cha St. Agustino, katika
kitivo cha sayansi ya siasa, Prof. Mwesiga Baregu, alisema ushauri alioutoa
Rais Kikwete kwa Rais Kagame ni mzuri, hauwezi kuleta athari zozote tofauti na
kutumia mtutu wa bunduki kukabili waasi.
"Mimi nikiwa kama mtaalam wa kutatua migogoro
suala la mazungumzo ni njia moja ambayo huwa inatumika mara kwa mara na
inasaidia kuleta amani," alisema na kuongeza;kutumia mtutu wa bunduki haileti tija kwa mataifa yote mawawili, hivyo
ni busara itumike njia ya mazungumzo."
Alitoa mwito
kwa nchi jirani kushirikiana kutatua mgogoro uliopo kwa njia ya mazungumzo
baina ya Rwanda na DRC.
Kwa upande wake
Mkuu wa Kitivo cha Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Kitila
Mkumbo, alisema anakubaliana na kauli ya Rais Kikwete na anashangazwa na Rais
Kagame ni kwa nini anachukizwa kuambiwa azungumze na waasi.
"Maana
yake inaonekana hataki kushauriwa...ushauri huo ni kitu kizuri kinaweza kuleta
maelewano," alisema Dkt. Mkumbo. Alisema Rais Kagame, anaonekana kama
dikteta kutokana na kukataa kuambiwa ukweli na viongozi wenzake.
Alisema kauli
ya Rais Kikwete, aliyoitoa kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa saba
hakugusia masuala ya vita na anaamini kwamba kwa karne hii sio mwafaka nchi
kuingia kwenye vita kwani nchi zina matatizo mengi ambayo yanahitajika kupatiwa
ufumbuzi.
"
Alichoongea
Rais Kikwete, ni msimamo unaotakiwa kuungwa mkono na Watanzania kwani yeye
ndiye Amiri Jeshi Mkuu na hiyo ndiyo kauli ya nchi...hivyo alichosema ni
sawa," alisema Dkt. Mkumbo.
Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alisema ameridhishwa na kauli ya Rais
Kikwete, kwani ametumia lugha sahihi katika kueleza hali halisi, hivyo
Watanzania wote wanatakiwa kumuunga mkono.
Alisema kwa
hali ilivyo ni lazima Watanzania waungane katika masuala kama hayo ili kuleta mshikamano
wa nchi. Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustino Mrema, alisema
anamuunga mkono Rais Kikwete, kwa kauli yake hiyo.
Alisema Rais Kagame ameanza chokochoko dhidi ya
Tanzania na kwamba hivyo, ndivyo alivyoanza hata Idd Amin. "Siungi mkono
vita vitokee, lakini kama atatuchokoza basi tuwe wa mwisho kujibu mapigo,"
alisema Mrema.
Aliyekuwa Mhadhiri UDSM, Dkt. Azaveri Lweitama, amezitaka nchi za Afrika
Mashariki kukaa chini ili kuangalia jinsi ya kutatua mgogoro huo.
Alisema kuipiga
Rwanda ni kazi ndogo sana, lakini hauwezi kumaliza tatizo kwa kutumia bunduki
na badala yake ni vyema nchi hizo zikaangalia namna ya kumaliza mgogoro.
"
Unajua
mnaweza kuingia katika vita mkamuondoa Rias wa Rwanda, lakini bado mkatengeneza
matatizo mengine kwa rais ajaye," alisema.
Alisema Kongo
kuna waasi wa Rwanda na hata Rwanda pia kuna waasi wa kutoka Kongo, hivyo ni
lazima kutafuta njia nzuri ya kutatua tatizo hilo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Lweitama,
alivitaka vyombo vya habari kutopotosha taarifa zinazozungumzia vita vikitokea
hakuna mtu atakayebaki salama.
"Vyombo vya habari vijitahidi
kuandika habari zisizo za uchochoezi, kwani hata ninyi pia ni Watanzania,
naamini vita ikitokea hakuna mhariri wala mwandishi atakayebaki salama,"
alisema.
Alisema vyombo vya habari pia vina nafasi
ya kukaa chini na kutafakari namna ya kumaliza mgogoro kwa kuwa vina nafasi
kubwa kwa mustakabali wa taifa.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda unaelekea
kupata mtikisiko baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza
na mahasimu wao. Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nia njema kwa kuwa bado
anaamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni
vyema itumike.
Ushauri ule aliutoa pia kwa Serikali ya
Kongo na kwa Serikali ya Uganda. ambapo katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni
wa Uganda aliunga mkono kauli hiyo.
Tangu
atoe ushauri huo viongozi wa Rwanga wamekuwa wakitoa kauli za kejeli dhidi ya
Tanzania na Rais Jakaya Kikwete. Katika hotuba yake Rais Kikwete, alisema
uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika kipindi kigumu.
source ya habari: majira
No comments:
Post a Comment