Dar es Salaam. Yanga imeng’arisha nyota ya
mwanzo wa msimu wa baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0 katika mechi ya
kibabe kuwania Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jana, Dar es Salaam.
Shujaa mechi hiyo kwa upande wa Yanga alikuwa Salum Telela aliyefunga bao pekee mwanzoni mwa mchezo na kupeleka hoihoi nzito Mtaa wa Jangwani
Ushindi huo unaifanya Yanga kuweka rekodi ya kutwaa mara tatu taji hilo.
Ilianza kulitwaa mwaka 2001 walipoifunga Simba 2-1, mwaka 2010 wakiifunga tena Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya 0-0.
Azam ndiyo timu pekee haijawahi kutwaa taji kati ya zilizowahi kucheza mechi ya Ngao ya Jamii. Mwaka jana walifungwa mabao 2-1 na Simba, Mtibwa walikuwa washindi wa mwaka 2009 walipoifunga Yanga 2-1.
Kocha wa Azam, Stewart Hall alikubali matokeo hayo na kusema, timu yake ilipoteza mchezo huo baada ya kushindwa kuwa makini dakika tano za mwanzo za mchezo, na kuisifu Yanga kwa kusema ilicheza vizuri.
Kwa upande wake, kocha wa Yanga Ernest Brandts
alikisifu kikosi chake na kusema kilicheza vizuri na pia amefurahi kuona
wachezaji wake wanazidi kuimarika kila siku.
Iliwachukua Yanga dakika mbili tu kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Salum Telela aliyeunganisha mpira wavuni akimalizia kazi nzuri ya Didier Kavumbagu.
Katika mchezo huo, Yanga iliwakosa wachezaji wawili kutokana na kuumia, akianza beki Kelvin Yondan aliyeshindwa kuendelea na mchezo kufuatia kugongana na John Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Mbuyu Twite.
Kipa Ally Mustapha naye alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Deogratius Munishi baada ya kuumia kwenye piga-nikupige langoni kwa Yanga katika dakika ya 19.
Azam nao walimkosa mshambuliaji wao Bocco aliyelazimika kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Mwaipopo baada ya kugongana na Twite katika dakika ya 73.
Azam wangeweza kusawazisha katika dakika ya 30,
kama siyo shuti kali la mshambuliaji, Kipre Tchetche kugonga mwamba wa
Yanga na mpira kutoka nje, huku Jerry Tegete akipaisha juu shuti lake
dakika ya 57
Telela naye alipoteza nafasi nzuri ya kuimarisha ushindi wa
Yanga baada ya kupiga nje ya lango mpira kufuatia kazi nzuri iliyofanywa
na Haruna Niyonzima.
Mchezo huo ulijaa ubabe na rafu zisizo na ulazima
kiasi cha Twite kushonwa mdomoni baada ya kupigwa kiwiko na Gaudence
Mwaikimba wa Azam, huku Aggrey Morris akimchapa kiatu Kavumbagu
mshambuliaji wa Azam mwishoni mwa mchezo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadik
aliwakabidhi Ngao ya Jamii, mabingwa, huku George Mkuchika akiwavisha
medali wachezaji wa Azam.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment