Juzi Mahakama ya Kisutu iliwatia
hatiani wahusika wa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community
Initiative (DECI) kwa kuwaadhibu kifungo cha miaka mitatu au faini ya jumla ya
shilingi milioni 21. Mmoja ameachiwa huru.
Washtakiwa hao ni Mchungaji
Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saiguran ole Loitginye na
Samwel Mtares. Pia Mahakama hiyo iliiamuru serikali Benki Kuu (BOT)
kuhakiki mali zote za DECI nchi nzima na kwarudishia wateja wanaoidai DECI
chochote.
Naam, haya ni mavuno ya aibu kwa taifa,
maana, tulichelewa kuchukua hatua za haraka kuwanusuru wanyonge wenye kupoteza
kidogo walicho nacho kutokana na hadaa ya watu wengine wenye majina makubwa. Na
wengine ni viongozi wa dini. Wote hawa wanashiriki kwenye kuwatepeli wananchi
wanyonge. Na kibaya ni kuwa utapeli huu unaendelea hata leo, kupitia migongo ya
imani.
Naam, nimepata kuandika, kuwa tunawapitisha
watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye matope. Kwa
nini?
Socrates, mwanafalsafa wa Uyunani
ya kale alipata kuonekana akimulika kurunzi mchana wa jua kali. Inaandikwa,
kuwa Socrates yule alizunguka sokoni na kurunzi (tochi) yenye
kumulika. Watu walimwuliza, kulikoni? Socrates akawajibu; ”Kwenye nuru
hii , kuna walio gizani.”
Kwa Socrates lilikuwa ni tendo la
kifalsafa lenye kuelezea hali halisi. Hata katika dunia hii ya
kisasa, bado tuna miongoni mwetu, walio gizani mchana wa jua
kali. Angalia ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo. Ndiyo, kuna waliohitaji
kumulikiwa mwanga.
Na kuna tofauti ya ujinga na
upumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma si kuufuta
ujinga, bali ni kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia
moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata profesa anaweza asijue namna ya
kuchochea kuni za kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la
saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda profesa.
Lakini, upumbavu ni ile hali ya mwanadamu
kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya
inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndiyo maana binadamu kuitwa mpumbavu ni
tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa
jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?
Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na
kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna
niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!”
Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani angetamka, kuwa angeanza
kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au
nchi kavu.
Wanadamu tumejaliwa akili ili
tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri
kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi
mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya DECI na hata ya kwa ’ Babu’ wa
Loliondo ni kielelezo cha Watanzania kuamua kuacha kufikiri. Kuna umma
uliojifunika vilemba vya ujinga. Umma uko gizani, unahitaji mwanga.
Yumkini wakatokea Watanzania wenzetu,
wakaoteshwa na Mungu juu ya dawa za tiba kwa mwanadamu. Na hapo
wakaingiza suala la imani. Na wakatokea hao wanaosema wanaweza wakafanya
maombi na miujiza ikatokea, kwa wasioona wakaona, wasiosikia wakasikia. Ni
uongo. Ni abrakadabra. Na wenye mamlaka wanawaachia watu hawa kuendelea na
abrakadabra zao. Kuwadhulumu wanyonge.
Katika dunia hii serikali hupendwa na
watu, lakini, si vema na busara, kwa serikali za dunia kutaka kujipendekeza kwa
watu. Kuna mambo yenye kupendwa na watu, na watu wakawa na haraka ya kutaka
kuyafanya. Lakini, kama serikali itahitaji kufuata taratibu ili kinachopendwa
na watu kifanyike, basi, serikali haina namna nyingine, bali kufuata taratibu.
Walau katika hili la DECI tulimwona
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisimamia taratibu. Waziri Mkuu Pinda kasimamisha
wimbi lile la DECI. Kuna wengi walishutumu, lakini , hao hao, leo wanaishukuru
Serikali. Maana, DECI nayo ilikuwa ni Abrakadabra. Na hukumu ya Mahakama ya
juzi imethibitisha hilo.
Sousrce:
www.raiamwema.co.tz: Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment