Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill
Clinton, hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili
za kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC.
Kwa muda wa miezi takriban minne
kumekuwa na maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika
maneno hayo yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi
za juu katika Serikali yake
Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais
Jakaya Kikwete kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu
waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa
kufanya mauaji ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.
Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu
800,000 wenye msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu
hizo zina utata, kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa
na idadi ndogo ya watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.
Pia, wapo wale ambao wanaweza
kushangaa kwa nini Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania,
nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya
1960 na kwa nini Rais Kikwete alitoa ushauri huo.
Kagame hakupendezwa na ukweli huo
kwani kila mara amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano
yanayoendeshwa na vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila
inapotokea hali kutulia.
Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa
muda mrefu kwani amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka
kumi na amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila
mafanikio kwa sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na
kudai kuwa kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho
kinaanzisha mapambano dhidi ya serikali.
Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa
Umoja wa Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo
kabla hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea
Rwanda baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake
ulirushiwa nyanya.
Hiyo ilikuwa ni kama kumpa ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati ule Watutsi walipouawa na Wahutu mwaka 1994.
Masikini! Annan angefanya nini wakati
alipokuwa akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji
kila moja lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa
uchelewashaji wa makusudi.
Baadaye Annan alipokuwa akigombea
Ukatibu Mkuu wa UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo
iliyopinga na hata alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo
iliyokuwa kinara wa kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa
yakifanyika wakati huo Kagame alikuwa akiyajua.
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda,
Meja Jenerali Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC) akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa
vikundi vyote vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha
kuwa Wahutu na jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa
linaundwa na waliokuwa vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.
Kwa maneno mengine, Kagame ameifanya
ardhi ya DRC kama uwanja wa mapambano kati yake na wapinzani wake ambao
wako mashariki mwa nchi hiyo.
Jenerali Nyamwasa, ambaye kabla ya
kukimbilia Afrika Kusini alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India anasema
kuwa Kagame ndiye aliyeamrisha kutunguliwa kwa ndege iliyokuwa imebeba
ujumbe wa nchi hiyo pamoja na Rais Juvenal Habyarimana na Cyprian
Ntyaramira wa Burundi ambao ulikuwa umetokea Tanzania kwenye mkutano wa
kujadili amani ya nchi hiyo.
Baada ya vita kumalizika na hatimaye
RPF kuchukua uongozi, Ufaransa, mtawala wa zamani wa Rwanda ilimtuhumu
Kagame kwa kusababisha mauaji ya kimbari kwani Wahutu wasingianzisha
chinja chinja ya Watutsi kwa wakati huo kwani mazungumzo yale yalikuwa
yanaelekea ukingoni na hatua ya mwisho ingekuwa kwa RPF kuwa chama cha
kisiasa ambacho kingeshiriki kwenye uchaguzi.
Nia ya Kagame ilikuwa ni kuchukua
uongozi Rwanda kwa nguvu kwa sababu kwa mizania ya siasa za nchi hiyo
ambazo zimejikita zaidi kwenye ukabila ingekuwa vigumu kwa Watutsi walio
wachache kushinda.
Sababu ya pili ambayo ndiyo
iliyowafanya RPF wakatae au watumie nguvu ilikuwa ni juhudi ya Marekani
ambayo ilikuwa mfadhili mkuu wa RPF kuhakikisha kuwa ushawishi wa
Ufaransa katika eneo la Maziwa Makuu unaondoshwa kwa gharama yoyote.
Hii inathibitishwa katika kitabu
Global Intelligence; the world's secret services today ambacho
kimeandikwa na waliberali, Paul Todd na Jonathan Bloch.
Waandishi hao wanabainisha kuwa wakati
huo kulikuwa na vita vya kijasusi baina ya Marekakani na Ufaransa
ambavyo baadaye vilibadilika na kuwa ni vita vya kijeshi.
Kagame alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na RPF.
Ufaransa ikimsaidia Habyrimana na
Marekani ikiwasaidia RPF ambao tayari walikuwa wakisaidiwa na Uganda
walijipatia taarifa za kijasusi kutoka kwa Serikali ya Rwanda na
wapiganaji wake.
Majasusi wa Marekani ambao walikuwa
wakitumia njia za kijasusi za siri za kunasa taarifa za mawasiliano
katika eneo la Afrika Mashariki walifanikisha mipango ya RPF katika
uwanja wa mapambano.
Marekani ilikiri kuwa kuanzia 1994
ilikuwa ikiwasaidia RPF kwa kuwapatia silaha na Kagame alipewa simu ya
satelaiti aina ya Motorola INMARSAT ambayo licha ya kufungwa kitaalam
(encryption) ili mawasiliano yake yasinaswe na wapiganaji wa Serikali ya
Rwanda au yeyote yule, kwa bahati mbaya shirika la Ujasusi la Kimataifa
la Ufaransa, DGSE (Direction Generale de la Securite Exteriure)
lilifanikiwa kunasa mawasiliano yale na Ufaransa iliituhumu Marekani kwa
kutoa kombora lililoiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana.
Kwa maana nyingine, ni kuwa Kagame
hawezi kukwepa mkono wa sheria wakati utakapofika kwani taarifa muhimu
za namna mambo yalivyokuwa yakienda katika uwanja wa mapambano,
mawasiliano yake yamehifadhiwa na taasisi hiyo ya kijasusi ya Ufaransa.
Waandishi hao wamebainisha kuwa kwa
kuwa Rais Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC) alikuwa akimsaidia Jonas
Savimbi ambaye Wamarekani walikuwa wameishamchoka na walimtaka aache
vita ili utulivu urejee Angola, nao wavune madini na mafuta huko wakiwa
na sababu ya kumwondoa Mobutu madarakani ili kukata mizizi ya usaidizi
aliokuwa akiupata Savimbi, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa UNITA,
iliyokuwa ikipigana vita vya msituni dhidi ya Serikali ya Angola chini
ya MPLA.
Sababu nyingine ilikuwa kwa Mobutu
kuwasaidia Wahutu ambao walikuwa kipenzi cha Ufaransa ilibidi aondolewe
ili kuhakikisha kuwa Wamarekani wanalishika na kulidhibiti eneo lote la
Maziwa Makuu.
Ikumbukwe kuwa wakati huo Rais Bill
Clinton ambaye hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma
zinazomkabili za kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC, ndiye
aliyekuwamadarakani wakati huo na alifanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa
shughuli za kijasusi zinaendeshwa katika mtindo ambao utakuwa na
manufaa zaidi kiuchumi na siyo kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa vita
baridi.
DRC ilikuwa muhimu kwa majasusi wa
Marekani, hasa kwa uzarishaji wa madini ya coltan ambayo hutumika
kutengenezea simu za mkononi, madini hayo hayapo sehemu nyingine yoyote
duniani zaidi ya DRC.
Clinton alihakikisha kuwa anafanya
kila awezalo kuondoa ushawishi wa Ufaransa nchini Sudan kwa kuwataka
viongozi wa SPLA wakati huo, Kanali John Garang na wengine wadai uhuru
kamili na siyo utawala wa shirikisho kutoka Sudan ili mradi Ufaransa
ikose mafuta yaliyokuwa yakichimbwa kutoka Sudan Kusini.
Waandishi hao wamebainisha kuwa
Marekani ilitoa dola 100 milioni ili kumsaidia Laurent Kabila kuanzisha
jeshi la watoto waliokuwa wakijulikana kama Kadogoo wakiwa na malengo ya
kumwondoa Mobutu.
Kufikia mwaka 1997, Shirika la
Kijasusi la Marekani (NSA) lilikuwa imejenga vituo vya kuendesha
shughuli za kijasusi ili kunasa taarifa za mawasiliano kupitia simu,
nukushi, redio katika sehemu mbalimbali za eneo la Maziwa Makuu kama
vile, Fort Portal nchini Uganda, Kigali Rwanda na Kongo Brazaville.
Ufaransa ambayo ilikasirishwa na jinsi
Marekani ilivyofanikisha kuwaondoa vibaraka wake katika DRC na Rwanda
ilihakikisha kuwa inawaandaa wanajeshi ambao walimpindua Rais Pascal
Lissouba wa Congo Brazaville ambaye alikuwa ni kipenzi cha Marekani.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment