NIMESEMA huko nyuma kwamba tumejenga
nakisi kubwa ya uongozi, na matokeo yake ni jamii yetu, kwa kiasi kikubwa,
inaendeshwa na maofisa, watu waliokabidhiwa ofisi. Hawa ni tofauti kabisa na
viongozi, kwa sababu, kama ambavyo nimeeleza mara nyingi, inawezekana kiongozi
akawa pia ni mtawala, lakini si kila mtawala ni kiongozi.
Kiongozi ni yule anayeonyesha njia, kwa
maneno yake, tabia yake na matendo yake, hata kama hana ofisi na hajakabidhiwa
kazi inayoitwa ya “uongozi” kama ambavyo tumezoea nchini mwetu. Haiwezekani
kwamba kila anayeteuliwa kuwa mtendaji wa kata, au mkuu wa wilaya, au mkuu wa
mkoa, waziri, akawa ni kiongozi kwa sababu tu kateuliwa kushika ofisi hiyo.
Uongozi ni zaidi ya ofisi.
Kila medani ya maisha ya kijamii inao
viongozi wake, na wingi wao wala hawajachaguliwa kwa kura na wala hawajateuliwa
na yeyote. Wengi pia hawalipwi mshahara na hawapokei posho, lakini ni viongozi
kwa sababu wanaonyesha njia na wenzao wanawafuata.
Kiongozi hujitokeza, hateuliwi. Katika
jamii za jadi wazazi na wakuu wa jamii waliweza kumtambua mtoto ambaye angekuja
kuwa kiongozi. Kwa mfano kuna mashindano ya mchezo kama soka. Timu mbili
zinashindana na zinahitaji mwamuzi lakini hakuna mtoto anayekubali kuacha
kucheza ili awe mwamuzi.
Watoto wenyewe wanaamua kumpata mwamuzi
ambaye ni mchezaji wa mojawapo ya timu mbili zinazoshindana. Wanamkubali
kuwa mwamuzi ingawa anaichezea timu yake kwa sababu wanamjua ni mtenda haki.
Anachezesha mechi na inapobidi anachukua uamuzi dhidi ya timu yake mwenyewe.
Huyo ni kiongozi; atafaa kuwa hakimu.
Mtoto mwingine atajipambanua na wenzake
kwa ujasiri wa kukabiliana na tishio linalomkabili yeye na wenzake, na
atawaongoza wenzake katika kukabiliana na hatari yoyote ile, akiwaelekeza
kuhusu mbinu za kutumia kupambana na adui. Huyo naye ni kiongozi; atafaa kuwa
kamanda wa kijeshi au mtaalamu wa usalama.
Mwingine ataonyesha umahiri mkubwa
katika kufanya biashara na kutengeneza faida kwa kujinyima na kuwekeza vyema.
Huyo naye atakuwa kiongozi, na ataweza kuilekeza jamii katika masuala ya
kiuchumi.
Watoto huonyesha dalili hizi wazi wazi,
na wakuu wa jamii wenye maono ya kiuongozi huwatambua watoto wa aina hiyo
wakiwa bado wadogo, na kisha huwaelekeza kwa kuwasaidia kukuza vipawa vyao.
Katika marika ya jando na unyago watoto
wenye mwelekeo wa uongozi walitambuliwa kirahisi zaidi na walijitokeza
kuwaongoza wenzao katika mitihani mingi waliyokabiliwa nayo. Katika unyago kwa
kisasa, ambayo ni elimu ya shule, kiongozi wa aina hiyo hujitokeza na kuwa ama
kiranja au kiongozi wa migomo pale wanafunzi wanapohisi kwamba hawatendewi
haki.
Ni hususan shuleni (pamoja na vyuoni)
wanapochomoka viongozi wa baadaye. Katika shule za kimapokeo (za kizamani)
walimu waliwateua watoto wakubwa wa mwili na wakali wa tabia kuwa viranja na
monita. Katika shule za kisasa wanafunzi wenyewe huchagua viranja wao na
kuwaheshimu badala ya kuwaogopa kama ilivyo kwa shule za kizamani.
Inapotokea kwamba wanafunzi wanahisi
kwamba wanaonewa kwa njia yoyote ile, viongozi wa wanafunzi hujitokeza na
kuongoza ama majadiliano baina ya wanafunzi na utawala wa shule, ama mgomo wa
wanafunzi pale majadiliano yanapokuwa hayana tija. Viongozi wa migomo shuleni
mara nyingi hukua na kuingia katika harakati za kisiasa ama za vyama vya
wafanyakazi; aghalabu huwa ni watu wa kudai na kutetea maslahi ya wenzao.
Kama vile ambavyo viongozi wa wanafunzi
wakati wa migomo na misuguano baina ya wanafunzi na walimu hujikuta mara kwa
mara wanapewa adhabu, pia viongozi wa kisiasa nao hujikuta wakikamatwa,
wakipigwa au hata kuuawa.
Kama ilivyo mtaani na shuleni wakati wa
utoto, pia katika umri mkubwa (ofisini, kiwandani, majeshini, katika biashara)
kiongozi ni mtu anayesema wazi kile anachokiamini na kukitetea bila kutafuna
maneno. Kiongozi ni mtu wa kujitolea nafsi yake, wala si mtu wa kutumia nafasi
ya uongozi kupata faida binafsi juu ya wengine.
Anaposafiri nchini na kuona hali duni
ya maisha ya watu wake, kiongozi anasononeka na anazidi kukuna kichwa akitafuta
namna ya kuwaokoa watu wake watokane na umasikini huo. Akikuta eneo ambako
wananchi wake wana neema anafurahi kuwaona walivyonawiri, mashamba yao
yalivyostawi, mifugo yao ilivyonona; hatafuti njia za kuwanyang’anya kwa ujanja
mashamba yao au mifugo yao. Ukwasi wa raia ndiyo furaha ya kiongozi, si ukwasi
wake binafsi.
Tukizirejea sifa hizi za uongozi,
tutang’amua kwamba kama tunao viongozi basi wataenea katika kiganja cha mkono.
Katika maeneo mengi, katika nafasi nyingi, katika ngazi zote za maisha
tumeelemewa na watu wanaopenda kujiita viongozi lakini hawana hata chembe ya
uongozi.
Walio wengi ni watu wema, waungwana,
wapole, watu ambao ungependa kuwa nao mtaani kama majirani. Lakini hawana sifa
za uongozi; ni wema na waungwana tu, basi, lakini si viongozi kwa sababu
hawajui ni wapi wanataka kuipeleka jamii.
Mbali ni hawa, wako wachache ambao si
tu kwamba hawana sifa za uongozi lakini kibaya zaidi ni kwamba ni majambazi,
wazandiki, wanafiki na madhalimu waliojiingiza katika nafasi za “uongozi” kwa
kila aina ya hila, na ambao wanatumia nafasi zao usiku na mchana kuiba,
kudhulumu, kupora, kunyang’anya na kukwapua.
Tukichanganya wale wema wasio na sifa
za uongozi na hawa majangili tunachopata ni jumla ya uongozi dhaifu usioweza
kuonyesha mafanikio ya kweli katika kuboresha maisha ya wananchi, hata pale
ambapo ni dhahiri kwamba uwezo wa rasilimali ni mkubwa. Sifa moja ya uongozi
mbovu ni pale watu wanapokufa kwa kiu huku wamezungukwa na maji.
Source:www.raiamwema.co.tz:
Jenerali Ulimwengu
No comments:
Post a Comment