Dar es Salaam. Baada ya kukaa kimya muda mrefu,
mwanasiasa mkongwe nchini, Kingune Ngombale-Mwiru, ameibuka na kuwatupia
lawama viongozi wa CCM, kwa kutaka kupenyeza suala la uraia wa nchi
mbili ndani ya Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam jana, Kingunge alisema baadhi ya ‘wakubwa’ ndani ya chama hicho wanataka kuliingiza suala la uraia wa nchi mbili kwenye Katiba Mpya kwa masilahi yao binafsi, bila kuwashirikisha wanachama.
Alisema anashaanga namna ambavyo suala hilo limeingizwa kwenye kitabu kiitwacho ‘Ufafanuzi wa rasimu ya Katiba Mpya’ kilichoandikwa na chama hicho, kwa kuwa halikuwahi kujadiliwa katika mikutano ya wanachama.
“Lipo jambo limenikera sana, napenda niliseme na lieleweke vizuri linahusu uraia. Nimearifiwa kuwa kwenye kikao cha Kamati Kuu walikuwa wakijadiliana, mimi nastaajabu kweli kwa chama changu kuliingiza suala hili,” alisema Kingunge.
Alisema yeye analipinga kwa sababu lingekuwa kubwa lingejadiliwa na wanachama ambao ni wenye nchi.” Alisema anapinga pendekezo la Watanzania kuruhusiwa kuwa na uraia wa nchi mbili kwa sababu hoja zilizotolewa, hazina nguvu.
“Tunaambiwa eti Watanzania wengi wako Marekani na Ulaya na huko wana fursa nyingi, eti wakipata uraia wa pili watafaidi vizuri fursa hizo. Wanaosema hivyo wana matatizo kidogo, wanataka uraia wa nchi yao na uraia wa nchi nyingine,” alisema.
Akizungumzia rasimu ya Katiba Mpya, Kingunge alisema mapendekezo ya kuwa na Serikali tatu yanaleta mkanganyiko kwa wananchi na kwamba hilo ni tishio tu la kutaka kutoka kwenye Muungano sahihi.
Wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimetamba kukusanya maoni ya watu 3,5 milioni kuhusu rasimu
ya Katiba Mpya kwenye ngazi mbalimbali ya mabaraza.
Chama hicho kimesema leo kinatarajia kukabidhi rasmi maoni hayo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Willibrod Slaa
alitamba kuwa maoni hayo wameyakusanya kwa uwazi kutoka kwa wananchi
katika ngazi ya wilaya, majimbo, kata na kwa njia ya simu,
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri ya Chadema, John Mrema, alisema chama chake kinahofia CCM inaweza kuchakachua maoni ya Katiba, hasa kama Bunge la Katiba litakuwa na idadi ya wabunge wa sasa.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu wa
Tanzania (Bakwata), limesisitiza kutambulika kwa Mahakama ya Kadhi
kwenye Katiba mpya.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Bin Simba, alisema
licha ya kutuma maoni ya kutaka kuwepo kwa mahakama hiyo wakati wa
kukusanya maoni, inashangaza kuona kuwa katika rasimu ya katiba maoni,
hayakuwekwa.
“Kwa kuwa ukusanyaji maoni bado unaendelea sikuona sababu ya kususa au kukasirika, mimi na jopo langu tumeandika upya na kupeleka tena kwenye Tume tukilidai hilo,”alisema Simba.
Mufti Simba alitoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazowafanya Waislamu kuidai mahakama hiyo kuwa ni kutaka kusimamia haki zao ikiwemo ya kumiliki makaburi ya Waislamu ambayo sasa yanamilikiwa na manispaa.
“Kwa Waislamu kudhuru makaburi ni ibada na hata katika vitabu vya dini imeandikwa, hivyo sisi kama Waislamu, tunataka kutetea haki zetu ,”alisema Simba.
Imeandaliwa na Goodluck Eliona, Kalunde Jamal na Beatrice Moses
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment