Leo Waislamu wa Tanzania wanaungana na wenzao
duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitri baada ya kumaliza
mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Ni siku ya kheri na furaha siyo tu
kwa Waislamu peke yao, bali pia kwa Watanzania wote. kama vyombo vingi vya habari vilivyo tangaza na kuandika ni utamaduni wa
Watanzania kuungana pamoja kusherehekea sikukuu kama ya leo. Utamaduni
huo hakika unakuza upendo na hali ya kuaminiana na kuvumiliana miongoni
mwa waumini wa madhehebu mbalimbali katika taifa letu.
Mwezi wa Ramadhan umekwisha, lakini mengi
tumejifunza katika mwezi huu; tulifurahia amani na utulivu uliopo,
tulifurahia imani na unyenyekevu ulioonyeshwa siyo tu na waliofunga,
bali pia hata wale ambao hawakufunga. Kipindi hicho kilituonyesha kuwa
ikiwa binadamu anataka kubadilika kimatendo anaweza kufanya hivyo, si
kwa mwezi mmoja tu bali katika maisha yake yote.
Sikukuu tuliyoisubiri sasa ndio imefika. Matumaini
yetu sote ni kwamba yale mema yote tuliyojifunza na kuyatenda wakati wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan yataendelea kuakisi maisha yetu ya kila siku,
hasa kwa kudhamiria kuwa raia wema wa taifa hili ambalo tunalipenda. Ni
vyema tujikumbushe muda wote kwamba Tanzania ni yetu sote bila kujali
dini zetu, itikadi zetu za kisiasa, silika na hata mila na tamaduni
zetu, sote tunapaswa tuilinde kwa sababu nchi hii ni mama yetu ambaye
akitutoka hatuwezi kupata mama mwingine wa kuchukua nafasi yake. Hivyo
ni wakati wa kutafakari vitendo vyetu na tujiulize nini tufanye kwa
mustakabali wa nchi yetu.
Ni wakati ambao Watanzania wanapaswa waitafakari
amani yao, utulivu wao na upendo wao kwa taifa lao, isiwe imani, amani
wala utulivu wa woga, bali vyote hivyo viwe vinatokana na dhamira ya
dhati tuliyonayo mioyoni mwetu katika kuijenga nchi yetu. Hiyo ndiyo
njia pekee ya kutupeleka tunakokwenda.
Ramadhan, Eid, Krismasi, Pasaka na sikukuu nyingi
nyinginezo zipo kwa ajili ya mazingatio ya nyakati na matendo
yaliyotendeka zama zilizopita, lakini sisi wa zama hizi pia tunayo
mazingatio yetu, tunazo shida zetu na tunazo tafakuri zetu, hivyo ni
lazima tutafakari na tuzingatie yale yanayotukabili kama mtu mmojammoja
na kama taifa.
Tunapaswa tudhamirie kujiondosha kutoka katika
hatua moja ya kimaendeleo na tuingie nyingine kwa sababu tunaamini
kwamba mawazo na hata matendo ya binadamu siyo mgando, tunapaswa
tudhamirie kubadilika kwa wema na tubadilike kwa kutenda yenye manufaa
zaidi kwa mustakabali wetu kama taifa.
Vitendo vya wizi, ubadhirifu, ufisadi, uzembe na
yote ambayo tunadhani yanaturudisha nyuma kimaendeleo tudhamirie
kuyapiga vita, kwani hivyo ndivyo masomo yanayotolewa na nyakati
yanavyopaswa kuendelezwa. Kinyume cha hivyo jana yetu inakuwa haina
tofauti na leo wala na kesho, kila siku mambo yanakuwa yaleyale. Hakika
hiyo si silika njema anayopaswa kujipamba nayo mwanadamu.
Tunapaswa tuache kutenda kwa mazoea, tutende kwa
dhamira, kwamba tunafahamu fika kuwa tukitenda jambo fulani jema,
matokeo yake ni kupata jambo jingine jema zaidi kwa sababu kila jambo
katika maisha lina nyongeza au punguzo. Kwa kufanya hivyo, hapana shaka
kwamba tutakuwa tunaongeza thamani ya maisha yetu.
kuwatakia sikukuu njema na yenye baraka tele.
source Mwananchi
source Mwananchi
No comments:
Post a Comment