Dodoma. Mgogoro wa kidiplomasia
ulioibuka kati ya Rwanda na Tanzania, jana ulitinga bungeni huku Rais
Jakaya Kikwete, akimuomba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa
msuluhishi wa mgogoro huo.
Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alionyesha kutoafiki kuombwa kwa Rais Museveni akisema naye yuko katika kundi linaloitenga Tanzania.
Kauli ya kwamba Tanzania kupitia kwa Rais Kikwete imemuomba Rais Museveni kuwa msuluhishi wa mgogoro huo,ilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la papo kwa hapo aliloulizwa na Mbowe akitaka kupata kauli ya Serikali juu ya kuibuka kwa mgogoro huo wa kidiplomasia na dalili za Tanzania kutengwa.
Katika swali lake la msingi, Mbowe alisema mvutano huo wa kidiplomasia umesababisha Tanzania kutengwa katika shughuli ambazo zilipaswa kuwa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alikiri kuwapo kwa hali ya kutoelewana na kwamba hata baada ya kauli ya Rais Kikwete kuwa Tanzania haina uhasama na Rwanda, mvutano unaendelea.
“Mimi ninavyojua Rais (Kikwete) amemuomba Rais wa Uganda Yoweri Museveni ajaribu kuona ni namna gani jambo hili linaweza kusuluhishwa na maneno haya yakapungua,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisema anaamini busara zitatumika ili kuona jambo hilo linakwisha vizuri lakini kama litaendelea na kuonekana dalili za Tanzania kutengwa busara zaidi itahitajika. Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema kinachoonekana, Rwanda wameweza kuwavuta Waganda na Wakenya katika mikakati ya kiuchumi ambao kwa hali ya kawaida ingekuwa ni ya jumuiya
Alisema viongozi wa mataifa hayo wamekutana Kampala na Kenya bila kuwapo kwa Tanzania
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment