MBUNGE wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan,
ambaye jina lake limetajwa kuhusika na biashara haramu ya dawa za kulevya,
amepata utajiri wa ghafla, akitokea kuwa teksi dereva, Raia Mwema limeelezwa.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi nchini
limekuwa ‘bubu’ kuzungumzia sakata hilo la Azzan pamoja na watu wengine
waliotajwa kuhusika na biashara hiyo hivi karibuni.
Azzan (48) ametumikia kwa muda wa
vipindi viwili ubunge wake wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuanzia
mwaka 2005, lakini tuhuma za sasa ni mtihani mkubwa zaidi kwake kisiasa ingawa
amekumbwa na masahibu mengine katika maisha yake hayo mafupi ya kisiasa.
Kwa mujibu wa mazungumzo ambayo gazeti
hili limefanya na baadhi ya watu wanaomfahamu mwanasiasa huyo kwa karibu, Azzan
amedaiwa kujihusisha na biashara mbalimbali, lakini zaidi ni kumiliki vyombo
vya usafiri.
“Unajua kesi ya Azzan ni ya kushangaza
kidogo. Miaka 20 tu iliyopita, alikuwa dereva teksi wa kawaida. Leo hii ni
tajiri mzuri. Ana majumba, magari ya kifahari na ni mbunge.
“Si hali ya kawaida na pengine ndiyo
maana anazua maswali mengi,” alisema mtu huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake
kwa sababu za wazi kabisa.
Kabla ya kuwa mbunge, Azzan alikuwa
kiongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na anatajwa
kuwa miongoni mwa viongozi waliochochea maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu
kwa wanawake mkoani Dar es Salaam.
Hata hivyo, taarifa nyingine kumhusu
Azzan ni zile zinazohoji kuhusu eneo analoishi jijini.
Azzan anaishi Magomeni jirani na kituo
cha kwa Bibi Paka ambako nyumba yake pengine ndiyo nzuri kuliko nyingine zote
zinazomzunguka.
“Watu pia wanajiuliza, inakuwaje mbunge
aishi Magomeni? Ana uwezo wa kujenga nyumba mahali popote jijini Dar es Salaam
na akaishi.
“Lakini yeye ameamua kuishi Magomeni
ambako ni miongoni mwa maeneo yaliyokithiri kwa biashara ya dawa za kulevya,”
kilisema chanzo kingine cha habari.
Raia Mwema limeelezwa pia kwamba Azzan
ametajwa kuwa na uhusiano wa karibu na waigizaji wa tasnia ya filamu na muziki
wa kizazi hapa nchini- tasnia ambazo zimedaiwa kuingia kwa nguvu katika
biashara hiyo katika siku za karibuni.
“Ni jambo la kawaida kuona waigiza
filamu wakiigizia kwenye nyumba ya Azzan. Yaani pale kwa Iddi ni kama sebuleni
kwao.
“Wanaigiza, wanakula, wanakunywa
wanavyotaka. Sasa kwa sababu nao siku hizi wanakamatwa kamatwa hovyo, nadhani
ndiyo maana na Azzan naye anatajwatajwa,” kinadai chanzo kingine.
Azzan alichukua ubunge wa Kinondoni
mwaka 2005 kutoka kwa Peter Kabisa, na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
taasisi ya Twaweza katika kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2012, alikuwa
mbunge wa 200 kwa uchapakazi bungeni miongoni mwa wabunge 344 waliopo bungeni.
Katika kipindi hicho bungeni, Azzan
aliuliza maswali ya msingi matatu, ya nyongeza sita na akachangia katika
mijadala mbalimbali mara 24.
Katika barua inayodaiwa kuandikwa na
vijana wa Kitanzania ambayo imesambazwa kwa vyombo mbalimbali vya habari
Tanzania kupitia mtandao wa internet kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita, Azzan
na watu wengine wametajwa kuhusika na biashara hiyo.
Vijana hao wamedaiwa kusota katika jela
zilizoko Hong Kong, China, kutokana na kukamatwa wakiwa na dawa za kulevya
wakiwa wametokea hapa nchini.
Akizungumzia tuhuma hizo dhidi yake,
Azzan amesema hahusiki na madai hayo na kwamba yuko tayari kuchunguzwa na
vyombo vya dola kuhusiana na tuhuma hizo na endapo atakutwa na hatia, ataachia
nafasi zake zote za uongozi alizonazo.
“Ukisoma barua iliyosambazwa mtandaoni,
utaona barua yenyewe ina upungufu mwingi sana. Kwanza wenyewe hawajataja majina
yao.
“Wana nini cha kuficha wakati tayari
wamekamatwa? Ndiyo maana nahisi ni wapinzani wangu kisiasa wenye nia ya kutaka
kunichafua.
“Tayari nimepeleka ripoti polisi. Niko
tayari kuchunguzwa wakati wowote na popote. Kama nitakutwa na hatia, nihukumiwe
tu kama wananchi wengine,” alisema Azzan.
Hii ni mara ya pili kwa Azzan kuingia
kwenye tuhuma za kuhusika na biashara hiyo haramu kwani kwa mara ya kwanza
ziliibuliwa na aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es
Salaam, Kilumbe Ng’enda.
Ng’enda alidaiwa kutoa kauli hiyo ndani
ya vikao vya ndani vya CCM katika wilaya ya Kinondoni Juni mwaka juzi, wakati
Azzan alipokuwa akidai kwamba uongozi wa chama hicho mkoani Dar es Salaam unapaswa
kuachia ngazi kutokana na kufanya kwake vibaya kwenye chaguzi mbalimbali.
Azzan mwenyewe alipata kutoa madai ya
kutaka kuwekewa dawa za kulevya kwenye gari lake na wale aliowaita wapinzani
wake wa kisiasa, na taarifa hizo alizipeleka Polisi jijini Dar es Salaam mwaka
juzi.
Akichangia kuhusiana na sakata hili la
Azzan, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Kabwe Zitto, alisema mbunge
mwenzake huyo anatakiwa awaridhishe Watanzania kwamba hajihusishi na biashara
hiyo.
Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa
Twitter, Zitto alisema, “Nimeona kuna mbunge mwenzangu ametajwa. “Nilikuwa na
Idi (Azzan) kwenye mafunzo ya JKT katika kambi ya Mgambo hivi karibuni.
Haonyeshi dalili za kuhusika na dawa za kulevya.
“Lakini namtaka aturidhishe kwamba
hahusiki na biashara hiyo ya dawa za kulevya.
“Akubali kuchunguzwa na vyombo husika
na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani,” aliandika Zitto.
Katika maelezo yake, Zitto amependekeza
kwamba kila mwanasiasa nchini ambaye amewahi kutajwa kuhusika na biashara hiyo
apigwe marufuku kushiriki katika siasa na pia atangazwe kuwa mtu hatari.
Alisema Watanzania wamechoka kuzika
ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na kueleza
kwamba kwa hali ilivyo sasa, ni wazi kwamba tatizo la dawa za kulevya ni janga
la kitaifa.
Akizungumzia tuhuma hizo dhidi ya
Azzan, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alimtaka
mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa
za Kulevya, Godfrey Nzowa, ili apate taarifa zaidi.
Hata msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,
Advera Senso, aliliambia Raia Mwema kwamba atakuwa tayari kulizungumzia suala
hilo pale atakapokuwa amepewa taarifa na wahusika.
Kamishina Nzowa hakuweza kupatikana
hadi tunakwenda mitamboni.
Lakini kwa upande wake, Shirika la
Polisi la Kimataifa (Interpol), limesema bado halijapokea rasmi tuhuma dhidi ya
Azzan na hivyo hakuna uchunguzi wowote unaofanyika dhidi yake.
Mkuu wa Interpol tawi la Tanzania,
Gustav Babile, ameliambia Raia Mwema Jumanne wiki hii, kwamba ingawa tuhuma
dhidi ya Azzan zimetoka nje ya nchi na linaweza kuchukuliwa kuwa ni la
kimataifa, bado hana taarifa zozote kutoka nje au
ndani ya nchi kuhusu suala hilo.
“Kusema ukweli sina taarifa zozote
kuhusu Iddi Azzan. Hii maana yake ni kwamba taarifa zake hazijaingia katika
duru za Interpol. Hilo ndilo pekee naweza kukwambia kwa sasa,” alisema.
Source:
http://raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment