Release No. 133
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Agosti 16, 2013
KAMATI YAPITIA USAJILI, NGASA KUCHEZEA YANGA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa
wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa
kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
P.T
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya
Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba
mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam)
ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na
fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za
mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa
fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa,
hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Vilevile Kamati imepitia pingamizi
zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya
wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi
Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni,
Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho
wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work
permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa
(Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe
zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande
ambazo hazikuafikiana.
UCHAGUZI TFF SASA KUFANYIKA OKTOBA 27
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo katika
kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za TFF inasogeza mbele tarehe
ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba 20 mpaka Oktoba 26 na 27 mwaka huu.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni
kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na
shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo
haitawezekana kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati
mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa
Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa
viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama
ilivyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na
waandishi wa habari Agosti 24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika wote
watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu
utakaosababishwa na mabadiliko hayo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
source: mjengwa blog
No comments:
Post a Comment