Ndugu zangu,
Mahusiano ni neno fupi lakini nyenye maana pana. Yaweza kuwa ya mapenzi, kirafiki, kindugu, kikazi na hata kimajiriani.
Na katika dunia hii, pesa haiwezi
kusimama peke yake kama yenyewe, lakini, mahusiano yanaweza kusimama
peke yake kama yenyewe, hata bila kutegemegea pesa.
Wanadamu tunapaswa kuyatunza na kuyadumisha mahusiano . Maana, mwanadamu ameumbwa ili ajenge mahusiano mema na wanadamu wenzake.
Pichani nimesimama na Salim ' Asas'
Abri kwenye moja ya visima vya kijamii shambani kwake. Huyu ni mmoja wa
rafiki zangu hapa Iringa ninakoishi.
Na kwa ukweli, Salim ndiye
aliyenifanya mimi na familia yangu tuchague kuishi Iringa, maana, kabla
ya kuja Iringa kutoka Sweden, mwaka 2003 nilifika Iringa kuona kama kuna
uwezekano wa kuja kufanya kazi hapa na kama kubwa kabisa, kama kuna
shule ambayo watoto wangu wangeweza pia kusoma. Shule yenye kutoa elimu
ya viwango vyenye ubora wa Kimataifa na yenye mazingira mazuri ya
kujifunzia.
Salim alikuwa Mjumbe na Mwenyekiti wa
Bodi ya shule ya Iringa International School. Alipofahamu kutoka kwa
Mwalimu Mkuu, kuwa nimekuja kuitembelea shule hiyo, basi, Salim, kama
mwenyekiti wa bodi, na hata kama hatukuwahi kukutana, alichukua jukumu
la kuniandikia email kunielezea zaidi juu ya shule hiyo na hata
kunishawishi, mimi na mke wangu, kufanya maamuzi ya kuchagua Iringa na
Iringa International School.
Hata hii leo, miaka kumi baadae, Salim
na mimi bado tuna mahusiano ya kirafiki na kushirikiana kwenye kazi za
kijamii ikiwemo kuchangia kazi hizo, hata kwa mawazo tu.
Naam, lililo jema kwa mwanadamu ni kudumisha mahusiano na si kuyabomoa.
Neno Fupi La Siku ya Leo; Mahusiano....
Maggid,
Iringa.
Iringa.
No comments:
Post a Comment