KUMEKUWA na mjadala juu ya dhana ya
vyama vya siasa kuunda vikosi vyake vya ulinzi. Hivyo basi, kuunda vikosi vyake
vya wanamgambo.
Inavyoonekana, kama nchi, kuwa tungali
kwenye ile hali ya delirium ambayo nilipata kuielezea ni hali ya
mwanadamu kuwa katika mkanganyiko (kuchanganyikiwa). Ni maradhi.
Tunayoyashuhudia sasa ni dalili za kuwa tumo kwenye hali ya Mkanganyiko-
Delirium.
Naam, kama nchi inatupasa
tukae chini na kuitafakari nchi yetu na mustakabali wake. Maana tumeanza
kushindwa kutofautisha kati ya chama cha siasa na chama cha ukombozi. Mathalan,
TANU ilikuwa Chama cha Ukombozi. TANU ilipigania uhuru wetu.
TANU chini ya utawala wa ukoloni
ilihitaji kuunda kikosi cha vijana wake kwa madhumuni ya kuwalinda viongozi
wake na hata kuwaandaa kuwa makamanda kwenye mapambano. Ndipo kukawa
kilichoitwa “TANU Youth League” na humo ndani kukawa na vijana wenye
majukumu ya ulinzi kwa chama na viongozi wake.
Sasa basi, nchi inapokuwa huru hakuna
haja ya vyama vya siasa kuwa na vikosi vyake vya ulinzi. Kazi hiyo inaachwa kwa
vyombo vilivyoundwa kwa kazi hiyo. Kinachotaka kutokea kwa nchi yetu kwa sasa
ni jambo la hatari sana. Kwamba tunafikiri kuruhusu vyama vya siasa kuwa na
vikosi vyake vya kujilinda.
Na huu ni wakati, kwa Watanzania, bila
kujali tofauti zetu za kiitikadi, kidini au rangi, tukemee kwa sauti moja
jambo hili. Kamwe tusikubali ikawa ni vitu vya kawaida kwa vyama kuwa na vikosi
vya vya wanamgambo.
Maana, uzoefu unatuambia, kuwa harakati
za vikosi vya wanamgambo wa vyama huambatana na vitendo vya kulipiza kisasi. Na
hilo ni jambo baya sana.
Maana, hapo ndipo chuki inapozaa chuki
na hatimaye Watanzania kuanza kuchinjana wenyewe kwa wenyewe. Yale tuliyokuwa
tukiyasikia yakitokea kwenye nchi za wenzetu tutaanza kuyaona nchini mwetu.
Tunaamini, Watanzania kwa ujumla wetu
ni watu tunaopenda amani na utulivu. Hata hivyo, kundi linaloweza kwa haraka
kuvuruga amani na utulivu wetu ni kundi la wanasiasa.
Tunaona sasa, dalili ya baadhi ya
wanasiasa, hata kwa kuvihusisha vyama vyao, kuwa tayari kutumia risasi na mapanga
ili mradi wafanikishe malengo yao ya kisiasa.
Watanzania tunapaswa kuwa makini.
Tunachopitia sasa ni kipindi kigumu sana. Kuna walio tayari kupandikiza
chuki miongoni mwetu ili tuanze kuchinjana wenyewe kwa wenyewe kwa kisingizio
cha tofauti zetu za kiitikadi, kidini, kikabila na hata rangi zetu.
Tufanye nini? Hakika, tutafanya makosa
makubwa kama kuna watakaodhani, kuwa madhara ya harakati za wanamgambo wa
vyama vya siasa hayatawahusu wao.
Vyama vya siasa vilivyo makini na
vinavyoitakia mema nchi yetu, vianze sasa kuachana na utamaduni wa kuwa na
wanamgambo- ama vikundi vya vijana wanaopewa mafunzo ya kijeshi kwa masuala ya
ulinzi.
Historia inatufundisha kuwa Afrika
‘Parties militia guards’ ama vikundi vya wanamgambo vya vyama vya siasa
huwa chanzo cha kuharakisha vurugu za kisiasa za wenyewe kwa wenyewe katika
nchi na hata kuwa chanzo cha mauaji. Tumeona Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kongo
na kwingine Afrika.
Ni vikundi hivi vya wanamgambo wa vyama
ambavyo hutumika na vyama, wanasiasa, au hujituma vyenyewe kufanya kazi ya
kulipiza visasi vya kisiasa kwa kutumia silaha.
Hapa kwetu tayari, vyama vikubwa vya
siasa vina vikundi vya aina hiyo; CCM wana ‘Green Guards’, CHADEMA wana ‘Red
Brigade’ na CUF wana ‘Blue Guards’.
Katika nchi ya kisasa si busara kuwa na
utaratibu unaoruhusu vyama vya siasa kuwa na vikundi kama hivyo vya vijana
vyenye kupata mafunzo ya kijeshi.
Na hakika, Katiba yetu ijayo itusaidie
kuondoa utaratibu kama huo wa ‘kijima’ kwa kuweka marufuku ya vyama vya siasa
kuunda vikosi vya vijana vyenye kukaa kambini na kupata mafunzo ya kijeshi,
vikosi ambayo, vinaweza kuja kutumika vibaya na kutusababishia madhara makubwa
kama taifa.
Kama vyama vitahitaji ulinzi kwenye
shughuli zake, basi, viombe ulinzi kwenye kampuni za ulinzi zinazotambulika
kisheria na zisizofungamana na siasa za vyama.
Vinginevyo, tuhakikishe jeshi letu la
polisi linaimarishwa na linakuwa chombo cha usalama kinachoaminika na umma,
kisichoegemea kwenye itikadi za vyama katika kufanya kazi yake. Vivyo hivyo,
kwa vyombo vingine vya usalama katika nchi ikiwamo Idara ya Usalama wa
Taifa. Vifanye kazi zao kwa kutanguliza maslahi ya taifa na si ya
wanasiasa au vyama vyao. Ni rai yangu.
No comments:
Post a Comment