MASIKINI Rais Robert Mugabe wa
Zimbabwe, anaongoza taifa tajiri katikati ya miba na joto kali. Ni nani
atamwonea wivu kwa zawadi pekee ya kuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe huru?
Fikiria utata katili unaomkabili, dunia
ya nchi za Magharibi imemkaba koo kwa sababu tu ya kutenda dhambi kuu ya
kisiasa ya kushusha bendera ya Uingereza – “Union Jack” nchini Zimbabwe na
kuwaamuru walowezi weupe kwa yeye kutii na kuheshimu matakwa ya wazalendo walio
wengi, na kuendelea kuvunjilia mbali mfumo hasi na usio wa haki wa umilikaji wa
ardhi miaka 13 iliyopita.
Kuanzia hapo, alianza kuondoa taratibu
upendeleo, ulafi na maslahi ya wazungu wachache waliojiona mabwana zaidi kuliko
wazalendo. Hatua hiyo ilisababisha walowezi mamluki kuondoka kwa wingi Zimbabwe
na wale wenye nia njema kwa Zimbabwe na Wazimbabwe walibakia. Kwa hili, nchi za
Ulaya na Marekani zilimwita mtawala dikteta na adui wa demokrasia na hivyo
kuiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi. Nasi baadhi ya Waafrika, kwa ujinga
wetu na umamluki, tukaitika mwangwi huo kwa kumwona vivyo hivyo.
Mugabe, kwa kukerwa
na uzandiki huu wa nchi za Magharibi, hususan Uingereza, alijitoa kwenye Umoja
wa Jumuiya ya Madola inayoongozwa na Malkia wa Uingereza akiita kuendelea kuwa
mwanachama ni upuuzi na utumwa mambo leo.
Katika uchaguzi wa hivi karibuni,
Mugabe, mwenye umri wa miaka 89, amepata ridhaa nyingine ya wananchi wake
kuiongoza Zimbabwe. Mwangwi umesikika tena kutoka nchi za Magharibi, nasi kwa
ujinga wetu tumedakia kwamba, Mugabe, kwa vigezo vya Magharibi ni dikteta na
kikongwe asiyefaa kuongoza taifa enzi hizi za “dotikomu”.
Lakini mbona hatuwaulizi wazandiki hawa
waseme; kati ya Mugabe na Malkia Elizabeth wa Uingereza, ni nani mzee
aliyetawala muda mrefu kuliko mwenzake? Mbona dunia haimshutumu Malkia
huyo kwa kukaa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, ambao ni muda mrefu kuliko
mtawala yeyote duniani?
Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, Umoja
wa Ulaya (EU) hususan Uingereza na Marekani, zimekuwa mstari wa mbele kumhujumu
Mugabe na Serikali ya Zimbabwe tangu mwaka 2000 pale Mugabe alipotaifisha ardhi
na mashamba ya wazungu wachache na kuwagawia wazalendo walio wengi badala ya
wazalendo hao kuendelea kuwa manamba katika mashamba ya walowezi.
Ni kweli kwamba, baada ya hatua hiyo,
uchumi wa Zimbabwe umetetereka, lakini si kwa sababu ya sera za Mugabe zenye
kujali wanyonge, bali ni kutokana na uhasama wa kizandiki wa nchi za Magharibi
dhidi ya nchi hiyo kufikia hatua ya kuitenga na kuinyima ushirikiano kimataifa.
Kwa wanaoielewa vyema historia ya Uhuru
wa Zimbabwe, watanielewa ninapotumia neno “uzandiki” wa nchi za Magharibi. Na
kwa wale miongoni mwetu wanaomshutumu Mugabe kwa hilo, bora wakaacha
kujidhalilisha kwa kujifanya kenge kwenye msafara wa mamba, msafara wasioujua
wala kuwahusu.
Uzandiki wa Uingereza unaanzia Novemba
11, 1965, wakati huo huo Rhodesia (baadaye Zimbabwe) ikiwa koloni la Uingereza;
ilipomruhusu mlowezi wa Kiingereza na haini, Ian Smith, kujitangazia uhuru kwa
mabavu (Unilateral Declaration of Independence) – UDI, kuwa mtawala wa
Rhodesia. Kufuatia hatua hiyo, mwaka 1969, wazalendo wa Zimbabwe walianzisha
vita vya msituni vya ukombozi (Chimrenga) kuung’oa utawala huo wa kidhalimu.
Na pale vita vya ukombozi dhidi ya
Smith vilipopamba moto kufikia hatua ya kuung’oa utawala wake, mlowezi huyo
alibadili mbinu kutaka kukabidhi Uhuru bandia kwa vibaraka wa Kiafrika, Askofu
Abel Muzorewa na Chifu Jeremiah Chirau, na kuibatiza nchi kuitwa “Zimbabwe –
Rhodesia”. Kama isingekuwa Mwalimu Julius Nyerere kumkabili ana kwa ana
na kwa hoja pevu, Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo, Magareth Thatcher,
Uingereza ilikuwa karibu kumtambua Askofu Muzorewa kama Waziri Mkuu wa Zimbabwe
– Rhodesia “huru”.
Na katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za
Jumuiya ya Madola uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Julai 1979, Mwalimu, kwa
mara nyingine alipambana na Thatcher kikamilifu na kufanikisha kuundwa kwa
kamati maalumu iliyoandaa mapendekezo ya Katiba ya Zimbabwe chini ya Mwalimu
Nyerere mwenyewe. Mapendekezo hayo ndiyo yaliyofanikisha kutungwa kwa
Katiba ya Zimbabwe ambayo ilitoa uzito mkubwa na wa pekee kwa suala la ardhi.
Mwaka huo huo, mazungumzo juu ya Uhuru
wa Zimbabwe yalifanyika huko Lancaster House, Uingereza kwa majuma 14 na kuwa
mazungumzo marefu ya pekee katika historia ya mazungumzo kama hayo kwa nchi
huru za Afrika. Hapo, suala la Ardhi lilikuwa zito kuliko yote kuwafanya
wazalendo, Robert Mugabe na Joshua Nkomo, kusitisha mazungumzo mara mbili kuja
Dar es Salaam kupata ushauri wa Mwalimu Nyerere.
Na ilipobainika kwamba suala hilo
lilikuwa gumu kuweza kupata ufumbuzi kwa mashauriano pekee, Mwalimu alimteua na
kumtuma aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania wa wakati huo, Joseph Sinde
Warioba (ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini),
kwenda Uingereza kuhudhuria mkutano huo ili kuokoa jahazi kwa upande wa
Zimbabwe.
Baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa, ni
pamoja na Serikali ya Uingereza kuwalipa fidia katika kipindi cha miaka 20
(kufikia mwaka 2000), walowezi waliokuwa wakimiliki ardhi ili hatimaye ardhi
hiyo irejeshwe serikalini kuwezesha kugawiwa bure kwa Wazalendo.
Hii ilikuwa agenda nzito na tete kwa
Waingereza na kwa wazalendo pia, kwani kutofanya hivyo kungekaribisha vita
nyingine kwa wazalendo kurejea msituni kuendeleza mapambano waweze kunyakua
ardhi kutoka kwa walowezi hao.
Kwa upande wa pili, ilikuwa simanzi kwa
wazungu kuachia ardhi waliyomiliki kwa karibu karne nzima, na hawakuwa na pa
kwenda.
Kwa kuwa vita ilionekana kuwa na
madhara zaidi kwa wazungu na kwa Serikali ya Uingereza pia, serikali hiyo
ilichagua kukubali kulipa fidia kwa walowezi kuepuka mapambano ya silaha kwa
mara nyingine. Makubaliano mengine yalikuwa ni kutenga viti 20 vya Bunge kwa
wazungu, kwenye Bunge lenye viti 100 katika kipindi cha mpito cha miaka mitano
hadi mwaka 1985.
Kati ya makubaliano hayo mawili, ni
hili la viti 20 vya Bunge tu ndilo lililotekelezwa; na hilo la kulipa fidia
lilipuuzwa na Serikali ya Thatcher hadi alipong’atuka madarakani na nafasi yake
kuchukuliwa na Waziri Mkuu John Major wa Chama cha Conservative, ambaye naye
alishindwa baadaye na Tony Blair wa Chama cha Labour.
Blair alikataa kulipa fidia licha ya
kukumbushwa mara nyingi na Mugabe juu ya kutimiza ahadi hiyo.
Robert Mugabe, baada ya kubaini uhuni
huo wa Serikali ya Uingereza, hakuwa na subira tena, hivi kwamba miaka 20 ya
makubaliano ilipotimia mwaka 2000, alianza kuwapokonya walowezi ardhi na
mashamba na kuzua mtafaruku miongoni mwa nchi za Ulaya, hususan, Uingereza,
ikiungwa mkono na shoga yake, Marekani.
Baadhi ya hatua nchi hizo zilizochukua
dhidi ya Zimbabwe ni pamoja na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na safari za
Mugabe kwenda nchi hizo kuzuiwa au kudhibitiwa.
Hatua nyingine ya kipuuzi
iliyochukuliwa dhidi ya Mugabe, ni kuvuliwa baadhi ya shahada (Mugabe ana
shahada saba) alizopata kutoka nchi hizo, kana kwamba kufanya hivyo
kungempunguzia akili, maarifa na uwezo wa kufikiri.
Ili kuhakikisha Mugabe anaondolewa
madarakani kwa njia ya sanduku la kura na wapinzani, mwaka 2000, wazungu
walianzisha harambee ya kuchanga fedha, ndani na nje ya Zimbabwe kuanzisha
Chama cha upinzani cha “Movement for Democratic Change” (MDC), na kumpachika
uongozi wa Chama kibaraka wao, Morgan Tsvangarai, mbumbumbu mwenye elimu ya
darasa la nne na ambaye alikuwa mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi nchini
Zimbabwe kupambana na Mugabe kwenye chaguzi.
Huku kikipewa nguvu
na misaada lukuki na walowezi, MDC kilipanda chati haraka haraka na
kujidhihirisha kuwa chama kikuu cha upinzani dhidi ya ZANU – PF cha Mugabe.
Pamoja na kuwa hivyo, MDC hakijaweza kukitikisa ZANU – PF chenye mizizi sehemu
za vijijini ambako wazalendo wanyonge hawajasahau fadhila ya Mugabe kwao
kwa kuwapatia ardhi na huduma zingine muhimu za kijamii.
Lengo la MDC ni kuhakikisha walowezi
wanarudishiwa ardhi na mashamba yao yaliyotaifishwa kikitwaa madaraka. Ni
dhambi kuu hii ya MDC inayomfanya Mugabe asing’atuke madarakani kuruhusu kwa
kile ambacho amekuwa akirudia kulaani, “nchi kwenda kwa mbwa”.
Mugabe amesema mara nyingi kuwa yuko
radhi kukabidhi madaraka kwa mzalendo mwingine yoyote, lakini “si kwa huyu
(Tsvangarai) kibaraka wa wazungu”. Amehoji, kwa nini wazalendo waendelee kukosa
ardhi ya kulima ndani ya Zimbabwe yao huru? Amekejeli kwa kusema, wanaohoji
ushindi na uongozi wake wajinyonge.
Dunia ya wapenda haki, tukiwemo sisi
“Wabongo”, inapaswa kumuunga mkono Rais Mugabe, Rais pekee barani Afrika
aliyebakia, anayeweza kuyaambia Mataifa makubwa “shut up” – “nyamaza” na
yakatikisika yasimfanye kitu. Watawala dhaifu wanaokosana na mataifa hayo, mara
nyingi wamepinduliwa kwa nguvu ya mataifa hayo, kwa sababu hawana msingi au
uungwaji mkono wa watu wao; lakini si kwa Mugabe.
Mugabe ni kikongwe wa miaka 89 mwenye
kujali maslahi ya taifa la Zimbabwe na wananchi wake. Amekataa kuwa mateka wa
ukoloni mambo leo na ubeberu wa mataifa makubwa. Kwa upande wa pili, Morgan
Tsvangarai, mwenye umri wa miaka 61 ni wa damu mpya, lakini ni mateka wa
ukoloni mamboleo, ubeberu na ufisadi wa kimataifa kuweza kuuza nchi na wananchi
wake kwa nyang’au hao.
Kama uongozi ni tunu kwa taifa, heri
kuongozwa na mzee kama Mugabe kuliko kuongozwa na kijana msaliti kama
Tsvangarai. Na hili liwe somo la kutosha kwa Watanzania wakati huu wa
kinyang’anyiro cha kumpata Rais ajaye mwaka 2015.
Si hivyo tu, suala la ardhi na
rasilimali za taifa nchini Zimbabwe liwe funzo kwetu. Wakati Mugabe
anatengeneza historia chanya kwa kurejesha ardhi iliyoporwa na wageni mikononi
mwa wazalendo, sisi, kwa ujinga tunakabidhi ardhi kwa wageni kwa kisingizio cha
uwekezaji ili kukaribisha usetla utakaowageuza wananchi kuwa manamba katika
nchi yao huru.
Wakati Wazimbabwe wanawapiga mieleka
wagombea urais vijana mafisadi, vibaraka na wauza nchi, na kuchagua wazee wenye
hekima na busara kuongoza nchi; sisi kwa ujinga, tunabeza hekima, busara na
uadilifu katika uongozi kwa kutekwa na ubeberu wa mitaji, umamluki na usaliti
kwa taifa.
Niambieni, kama leo Mwalimu angefufuka
na kusimama kugombea urais, nani angethubutu kujilinganisha naye na kutoa
changamoto bila kujiaibisha? Je, Mwalimu ni kijana?
Niambieni, kama Edward Moringe Sokoine
angefufuka leo na kugombea urais, nani kati ya hawa wa enzi za “dotikomu”
angejilinganisha naye kutaka kugombea bila kuanguka kabla ya kusimama?
Kwa jinsi ambavyo imekuwa rahisi kwa
mataifa ya kibeberu kushinikiza na kuamuru hatima yetu kisiasa na kiuchumi
kupitia viongozi mamluki, ndiyo kunakofanya uhuru wetu kuwa kichekesho. Lakini
si kwa kiongozi kama Rais Mugabe ambaye daima amesimama kutetea uhuru wa nchi
yake.
Na kwa udhaifu huu wa viongozi,
tumegeuka kichekesho na jamvi la wageni; tunalilia umoja, lakini tunatenda kwa
utengano; tunalilia uhuru kama taifa, lakini tunajenga utegemezi kwa mataifa ya
kibeberu.
Tunapenda kuona ustawi wetu na wa
taifa, lakini tunatumikia umasikini wa kujitakia. Tumegeuka taifa la ombaomba
katikati ya utajiri tulioruhusu kuporwa chini ya sera za uwekezaji usiojali.
Lakini si kwa kiongozi kama Rais Mugabe, aliyeweka mbele maslahi ya taifa
badala ya maslahi kwa wageni.
Wakulima na wafanyakazi wetu
wanagharimia uzandiki huu kwa jasho na machozi kuneemesha tabaka la watawala wasiotaka
kuona ukweli wa maisha duni ya wanyonge hao. Tabaka hili la watawala limepofuka
kwa hofu, hofu ya kuwaogopa watu wao wenye njaa, wenye kuvaa matambara na umma
unaofupika umri wa kuishi kwa umasikini, kwamba siku moja watasema “imetosha”
na kutenda yasiyotarajiwa.
Haya yote hayaonekani machoni, wala
kusikika masikioni mwa viongozi wenye ukwasi wa kupora, kwa sababu
wamehakikishiwa “usalama” na dunia ya ubeberu wa mitaji kuwa, “msihofu enyi
kundi dogo, kwa kuwa baba yenu (ubeberu) amekwishawapa ule ufalme wa ulaji”.
Kwa kundi hili na mabwana zao, kiongozi
kama Rais Robert Mugabe, mwenye kusimamia na kutetea maslahi ya nchi na
wananchi wake ni “gaidi”. Na kwa nini tumekubali kutunga sheria ya ugaidi hapa
kwetu bila kutafiti mantiki yake na hatima ya uhuru wetu, chini ya sheria hii
ya kibabe?
source://www.raiamwema.co.tz:
Joseph Mihangwa
No comments:
Post a Comment